*Diwani Kayenze aelezea jitihada anazofanya kuhakikisha wanafunzi wanaripoti shuleni
Na Judith Ferdinand,Timesmajira Online-Mwanza
Hadi Februari 5, 2026, jumla ya wanafunzi 1,451 sawa na asilimia 13 kati ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza bado hawajaripoti shuleni.
Taarifa zinaonesha kuwa kati ya wanafunzi hao, wavulana ni 689 huku wasichana wakiwa 762,ambapo Halmashauri hiyo kwa mwaka huu wa masomo ilipangiwa jumla ya wanafunzi 11,348 na hadi Februari 5,2026,wanafunzi 9,897 sawa na asilimia 87 walikuwa wameisha ripoti.
Akizungumza na Timesmajira Online, Ofisa Elimu Maalum Sekondari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Mwalimu Mugyabuso Witness, amesema sababu za wanafunzi hao kutoripoti bado hazijabainika wazi, ingawa juhudi za ufuatiliaji zinaendelea ili kubaini walipo.
Mwalimu Mugyabuso,amesema wanashirikiana na Wenyeviti wa Serikali za mitaa kuhakikisha wanawabaini na kuhamasisha wanafunzi ambao bado hawajaripoti shuleni pamoja na kuwatumia wanafunzi ambao wameisha ripoti shuleni kupata taarifa na kuwa mabalozi wa kuwahimiza wenzao kuja shuleni.
Ameeleza kuwa baadhi ya wanafunzi wamepelekwa shule binafsi, lakini wazazi au walezi wao hawajawasilisha taarifa rasmi kwa mamlaka husika au shule waliokuwa wamepangiwa.
“Hali hii inachangia kuchelewa kupata takwimu sahihi kwa kipindi husika kwani mara nyingi wazazi hutoa taarifa pindi anapihitajika kupeleka PREM Namba katika shule hiyo binafsi kwani analazimika kuifuata shule aliyokuwa amepangiwa mtoto wake lakini muda unakuwa umeisha enda,”amesema.
Mugyabuso amesema mahitaji muhimu ya shule yanaweza kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyowafanya baadhi ya wazazi kusita kuwapeleka watoto wao shuleni.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa wazazi wanapaswa kuwapeleka watoto shule hata kama bado hawajafanikiwa kupata mahitaji kama vile sare, viatu, kalamu na madaftari.
“Serikali inatoa elimu bila malipo kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita. Hakuna mtoto wa Kitanzania anayepaswa kukosa elimu kwa kisingizio cha kukosa ada au mahitaji ya shule, kwani tumeruhusu wanafunzi kuripoti shuleni huku wazazi wakiendelea kutafuta vifaa taratibu,” amesema Mugyabuso.
Aidha, amesema hadi sasa hakuna taarifa yoyote ya mwanafunzi kushindwa kuripoti shule kutokana na sababu ya mimba katika halmshauri hiyo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kayenze, James Makambuya, amesema kata yake ina shule moja ya sekondari ambayo ilipangiwa wanafunzi 360 wa kidato cha kwanza kwa mwaka huu, lakini hadi Ijumaa ya Februari 6, 2026, wanafunzi 320 pekee ndio walikuwa wameripoti.
Amesema baadhi ya wanafunzi ambao hawajaripoti wanatokana na changamoto za wazazi, wengine wanaweza kuwa wameolewa au kuhamishwa, huku akibainisha kuwa asilimia kubwa tayari wameripoti.
Makambuya ameongeza kuwa mazingira ya ziwani yamechangia changamoto ya baadhi ya wazazi kutokuwa na mwamko wa kuwapeleka watoto shule kwa ajili ya kupata elimu.
“Kama Diwani, nimekuwa nikitumia mikutano ya hadhara kuhamasisha jamii. Juzi nilifanya mkutano wa hadhara na wazazi na jamii kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaenda shule,” amesema.
Ameeleza kuwa changamoto ni uwezo mdogo wa wazazi kumudu gharama kama sare za shule na michango mbalimbali, lakini jitihada zinaendelea kupitia mikutano na vikao na wazazi ili kuwaelekeza umuhimu wa elimu.
“Katika kikao cha wazazi na walimu wa shule ya sekondari Kayenze, tulibaini uzembe wa wazazi na watoto katika masuala ya shule pamoja na mtazamo hasi kuwa watoto wanasoma lakini hawapati ajira. Tunawahimiza wazazi waelewe kuwa mtoto akisoma si lazima aajiriwe,” amesema.
Ameongeza kuwa tayari jitihada hizo zinaanza kuzaa matunda,amepewa taarifa kuwa kati ya wanafunzi 40 waliokuwa hawajaripoti, 10 wameripoti shuleni jana Jumatatu.
Makambuya amesema anatarajia kufanya mkutano mwingine wa hadhara katika mtaa wa Kayenze ili kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaripoti na kuanza masomo, huku baadhi ya wazazi wakidai changamoto ya watoto kwenda shule bila sare huwakatisha tamaa kutokana na wenzao kuvaa sare kamili.
Naye mmoja wa wananchi wa Wilaya ya Ilemela, Grace Mariceli, amesema kuwa alichukua hatua ya kutoa taarifa kwa Mwalimu Mkuu wa shule aliyokuwa imepangiwa mtoto wake, ambaye alimpatia namba ya PREM kwa ajili ya kuwasilishwa katika shule anayokwenda kuendelea na masomo mtoto huyo.
Amesema kuwa kwa sasa mtoto wake anatarajiwa kuripoti shuleni kesho baada ya kukamilisha mahitaji muhimu, na kusisitiza kuwa ni muhimu kwa wazazi kutoa taarifa mapema wanapowahamisha watoto wao, hatua ambayo husaidia kuondoa sintofahamu kwa jamii,walimu na serikali kuhusu mahali alipo mwanafunzi husika.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina