December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilemela nyama choma festival, yazinduliwa 

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza 

Tamasha la Ilemela nyama choma(Ilemela Nyama Choma Festival),limezinduliwa huku likitarajiwa kuinua kipato cha wananchi na wafanyabiashara wilayani Ilemela  na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla.

Tamasha hilo ambalo limeandaliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,ambalo litakuwa linafanyika kila Jumamosi kwa lengo la kuwakutanisha watu mbalimbali mkoani Mwanza.Huku Halmashauri hiyo ikiombwa kuboresha miundombinu ya uwanja wa Nyamh’ongolo eneo ambalo linafanyika tamasha hilo.ili liwe bora zaidi.

Akizungumza Novemba 16,2024,wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo,ambalo linafanyika uwanja wa Nyamh’ongolo wilayani Ilemela,Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda,amesema matarajio ni kuimarisha uwanja huo na  kuweka miundombinu mizuri ili watu wasinyeshewe na mvua pindi itakaponyesha.

“Kila Mtanzania akija Mwanza,ajue siku ya Jumamosi huduma ya nyama choma inapatikana hapa Nyamh’ongolo,kama ilivyo maeneo ya mikoa mingine ikiwemo Dodoma ukitaka nyama choma unaenda Mnadani.Tamasha hili linafaida kwa jamii yetu ya Ilemela,wanamwanza pamoja na wageni kutoka sehemu mbalimbali,”amesema Mtandao na kuongeza:

“Litainua kipato cha watu ambao wanafanya biashara katika eneo hili,itakuwa sehemu ya mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.Pia kuimarisha uhusiano na umoja, kwani litawakutanisha watu wa makundi tofauti tofauti na kubadilishana mawazo,”.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Ummy Wayayu,amesema,aliamua kuja na wazo hilo ili watu wapate eneo la kuweza kutafakari kutuliza akili,kupumzika na kubadilishana mawazo ili kuondokana na msongo wa mawazo.

“Pato la Halmashauri litaongezeka,na afya za wananchi zitaimarika kwani watu wanakumbwa na mambo mengi ambayo yanasababisha msongo wa mawazo”stress”,tunaona vifo vya ajabu,lakini ukitoka kule wiki nzima ukija hapa, utakutana na watu tofauti,mawazo tofauti,kwaio ni tiba.Kwa kushirikiana na wadau kadri tunavyoenda tutaboresha na mbeleni tutafanya tutawashindanisha wachoma nyama,watu wa ngoma na kutakuwa na live band,”.

Katibu wa wadau wa nyama choma,Ezra Shandu,ameomba miundombinu ya eneo hilo iendelee kuboresha hasa katika kipindi  cha mvua ili kuwalinda wateja na vifaa vya.Pia matangazo kuhusiana na tamasha hilo yaendelee kutolewa ili wananchi waweze kufahamu uwepo wa tamasha hilo.

“Wadau wa nyama choma tuendelee kushirikishwa siku zote kwenye maboresho ili kufanya tamasha kuwa bora zaidi na lenye mvuto,kwani tunajua mahitaji ya wateja wetu,”.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula,ametoa pongenzi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwa ubunifu huo,hivyo wanatarajia siku za baadae kutakuwa na nyama pori kwa sababu zinawapenzi wengi,na ni sehemu ya kufanya biashara na kuweka mikakati.