November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilemela na mkakati wa kutumia Ziwa Victoria kukuza uchumi kupitia ufugaji wa samaki njia ya vizimba 

Judith Ferdinand, TimesMajira Online

Imeelezwa kuwa asilimia 73.3,ya eneo la Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ni maji kutokana na kuzungukwa na Ziwa Victoria kwa sehemu kubwa.

Hivyo halmashauri hiyo imekuja na mkakati wa kutumia rasilimali ya Ziwa Victoria kwa ajili ya kukuza uchumi wa halmashauri hiyo,Mkoa na taifa kwa ujumla.

Akizungumza na TimesMajira Online,Mchumi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Herbert Bilia,mara baada ya kongamano la majadiliano juu ya mada zinazohusu utekelezaji wa mipango mikakati ya halmashauri nchini yalioandaliwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI,Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.

Majadiliano hayo yalifanyika kwa siku mbili jijini Mwanza Machi 9 hadi 10 mwaka huu, kupitia mradi wa Uendelezaji Miji (Green and Smart Cities Sasa ” project) ambao nchini hapa unatekelezwa katika Halmashauri za Jiji la Mwanza na Tanga pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

Mchumi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Herbert Bilia

Bilia anaeleza kuwa,watatumia rasilimali ya ziwa kuhakikisha kwamba wanakuza uchumi wa halmashauri,Mkoa na taifa, miradi ikifanikiwa kukamilika itasaidia kuongeza pato la halmashauri ambapo bajeti ya iliopo sasa ni bilioni 13.5 hivyo wanategemea kwa bajeti ijayo ya 2023/2024 wafikie bilioni 16.2.

Ambapo kupitia ufugaji wa samaki wa vizimba ndani ya Ziwa Victoria ni fursa kubwa ambayo wakiitengeneza vizuri itakuwa chanzo kizuri cha uchumi na kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana, wanawake na jamii kwa ujumla.

“Rasilimali yetu Ilemela ni Ziwa Victoria tunaamini tukienda nalo vizuri wananchi watapata uchumi mkubwa na taifa litapata mapato ya kutosha,wenzetu Japan walibuni mbinu ya bidhaa moja uzalishaji mmoja,yani unaangalia ni rasilimali gani unaweza kuifanya kwa tija zaidi na kusimamia na kuibeba hiyo hiyo na ikakutoa na kukufikisha tofauti na tulivyozoea unabeba vitu vingi na unakuta hakuna kinachokutoa,”anaeleza Bilia.

Anaeleza kuwa kwa mwananchi mmoja mmoja wamejipanga kwa kila mwaka kutenga fedha kwa ajili ya kuwakopesha vijana, wanawake na walemavu,ambapo kupitia mikopo hiyo kuna vikundi vya vijana ambao wameweza kufunga samaki kwa njia ya vizimba(fish cages), ndani ya Ziwa Victoria.

“Mwaka jana halmashauri yetu ilitoka milioni 100, kwa ajili ya kukopesha kikundi cha vijana ili liweze kufanya shughuli za ufugaji wa kisasa wa samaki katika Ziwa Victoria,kupitia ufugaji wa samaki wa vizimba ni fursa kubwa ambayo tukiitengeneza vizuri itakuwa chanzo kizuri cha uchumi na ndio tulichojadili katika kongamano hilo na kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana, wanawake na jamii kwa ujumla,”anaeleza Bilia.

Kujipanga katika kutatua changamoto za ufugaji wa samakiBalia anakiri kuwa ni kweli changamoto ya ukosefu wa chakula cha samaki wanaofugwa ni kwa nchi nzima ambapo vyakula vinavyopatikana havina protein ya kutosha ili kuwezeshwa mvuvi mfugaji kuweza kupata matokeo mazuri.

Ambapo hakuna kiwanda nchi nzima kinachozalisha chakula bora cha samaki,hivyo kama halmashauri kwao ni fursa watajipanga kuona namna ya kuita wawekezaji na ikiwezekana waweze kufanya utaratibu wa kufanya tafiti.

“Kwanza tuone chakula hicho kinatengenezwa kwa mfumo upi,ili sasa tuweze kuita wawekezaji na ikiwezekana tutengeneze ubia tujenge kiwanda kizuri ambacho kwanza kitaajiri watu na kupata chakula kwa ajili ya wafugaji wa samaki na kuongeza kipato pia ni fursa kwa wananchi pia siyo kwa chakula cha samaki lakini pia chakula cha mifugo pia bado ni changamoto,”.

Akizungumzia mradi wa Green and Smart Cities katika halmashauri yao unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya ambao umelenga kuongeza mnyororo wa thamani wa chakula ( food value chain) na mfumo wa kibiashara ( trade systems),unaotekelezwa katika Halmashauri tatu nchini hapa ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Jiji la Mwanza na Tanga.

Bilia anaeleza,kuwa Ilemela ni moja ya halmashauri ambayo itanufaika na mradi wa Green and Smart Cities Sasa,ambao umelenga sana halmashauri zinazopatikana rasilimali za maji(ziwa na bahari),Ilemela wana Ziwa Victoria ambapo halmashauri yao asilimia 73.3 ya eneo ni maji.

“Sisi Ilemela ni moja ya halmashauri tulioitwa hapa chini ya mradi wa Green and Smart Cities,tumeona ili mipango mikakati yetu iweze kufanyika vizuri tunahitaji rasilimali fedha,kwa halmashauri yetu rasilimali fedha yetu sehemu kubwa ni ziwa,”anaeleza Bilia.

Bilia anaeleza kuwa kupitia mradi huo Ilemela wana miradi mitatu ambayo imejikita katika mnyororo wa ongezeko la thamani kwenye rasilimali za masoko upande wa ziwa.

“Lengo moja wapo la programu ya Green and Smart Cities,wafadhili wanasema kwanza kuongeza thamani katika mnyororo mzima wa mazao hususani mazao ya uvuvi,hivyo wakaangalia uhalisia wa rasilimali husika ni zipi hivyo waliweza kuja Mwanza kwa sababu kuna Ziwa,”.

Miradi mitatu itakayotekelezwa Ilemela

Bilia anaeleza kuwa mradi wa kwanza ni uimarishaji wa Mwalo wa Kirumba,ambao unachangia zaidi ya milioni 700 hadi bilioni 1,kila mwaka hivyo wakiuimarisha wataweza kupata mapato zaidi ya hapo.

“Umoja wa Ulaya umeisha tembelea eneo hili la mwalo wa Kirumba na sasa wanaenda kufanya uchambuzi yakinifu pia wameuchagua kuwa ni mradi ambao utatekelezwa,”anaeleza Bilia.

Mradi wa pili ni kuboresha Mwalo wa New Igombe,ili miundombinu iwe rafiki kwa maana ya samaki na dagaa waweze kutunzwa vizuri,wasiharibike na waweze kuongeza thamani katika mnyororo mzima wa mazao ya uvuvi.

Mradi wa tatu ni kuboresha soko la Buswelu ili liwe la kisasa na hata mazao yanayotoka kwenye ziwa wanapo kuja nchi kavu wakutane na mazingira mazuri na wanufaika wengine ambao hawahusiani na ziwa waweze kunufaika pia.

“Kwaio hii ni miradi mitatu ambayo itakuwa chini ya programu ya Green and Smart Cities,katika halmashauri yetu ya Ilemela,ili tuweze kutumia vizuri asilimia 73.3 ya eneo letu lote ambalo ni maji kwanza ni kuboresha mialo,ili Ilemela iwe kituo cha mazao ya uvuvi,watu kutoka Kenya,Uganda waje wapate samaki wazuri,dagaa wazuri na ufugaji wa kisasa,”anaeleza Bilia.

Katika kulinda rasilimali za ziwa

Halmashauri ya Manispaa yetu kwa mwaka huu na mwaka ujao imetenga fedha kwa ajili ya kununua boat mbili milioni 90, kwa ajili ya kufanya doria kuzuia uvuvi haramu pamoja na uvuvi ambao hauna tija kwenye ziwa lao.

“Hili suala la uvuvi haramu na kulinda rasilimali za Ziwa Victoria,zinahitaji muunganiko wa sekta mbalimbali siyo halmashauri pekee yake,tunatoa wito kwa sekta nyingine zinazonufaika na rasilimali hizi ziweze kutoa ushirikiano katika kudhibiti uvuvi haramu na kulinda rasilimali yetu,”anaeleza.

Sekta binafsi katika kuunga mkono mikakati ya halmashauri sekta ya uvuvi Mkurugenzi wa Mtendaji wa Kampuni ya Myfish Tanzania Mpanju Elpidius, anaeleza kuwa sekta binafsi zinaweza kushirikiana na halmashauri kutengeneza mpango mkakati kwa sekta binafsi kuhusishwa moja kwa moja katika utungaji wa sera kwani moja ya mtekelezaji na mlaji ni sekta hiyo.

Mkurugenzi wa Mtendaji wa Kampuni ya Myfish Tanzania Mpanju Elpidius akizungumza na TimesMajira Online mara baada ya kumaliza kwa kongamano.

Mpanju anaeleza kuwa mradi wowote ambao unatekelezwa na serikali mnufaikaji mkubwa ni wananchi na taasisi binafsi, serikali anakuwa yeye ni mtekelezaji hivyo mradi huo pia wa green and smart cities utawanufaisha.

“Nikizungumzia kwa upande wangu sekta yangu ya uvuvi kwenye mradi huo kuna kipengele cha kujenga masoko ya samaki na kujenga vyumba vya barafu(cold room) ya samaki,mimi mkulima wa samaki sina cold room kwaio nimeisha jua wapi nitaenda kuhifadhi samaki wangu wasiharibike niende kuuza soko la nje ya hapa,”anaeleza Mpanju.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye kipindi hicho alikuwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo Abdallah Ulega,alipotembelea mradi wa vijana wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba uliopo Kata ya Sangabuye eneo la Igalagala, wilayani Ilemela mkoani Mwanza (picha kwa msaada wa mtandao)