November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilemela kuendelea kulipa fidia wananchi

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 imelipa fidia bilioni 1.3, huku ikisisitizz ikuendelea kulipa fidia wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa na Halmashauri hiyo kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kadri itakavyokusanya.

Huku imejipanga kununua magari matano kwa ajili ya uzoaji taka ili kutatua changamoto ya wananchi kukaa na uchafu muda mrefu bila ya kuondolewa katika maeneo yao hali ambayo inaweza kuhatarisha afya zao.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Wakili Kiomoni Kibamba,wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Baraza la Madiwani cha kupokea taarifa ya robo ya pili mwaka wa fedha 2023/2024 kilichofanyika Februari Mosi mwaka huu katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.

“Kwani maeneo ambayo tumeyahodhi ni kwa manufaa ya umma na jamii kwaio tutaendelea kulipa fidia hivyo wananchi wawe na subira , tutaendelea kuwalipa kwa kadri tunavyokusanya
kwani mpango wetu tunalipa fidia kila mwaka tunatenga bilioni moja,kwa mfano mwaka huu wa fedha tumelipa fidia kiasi cha bilioni 1.3,”ameeleza Kibamba.

Hata hivyo ameeleza kuwa mradi wa viwanja vya Nyafura una faida ya bilioni 7, kama watu wote watalipa viwanja vyote maana yake ni kwamba ile faida ya kule itatusaidia kupunguza kero ya wananchi kwenye fidia pamoja na mapato ya ndani.

Sanjari na hayo Kimbamba ameeleza kuwa Halmashauri inakabiliwa na changamoto ya vitendea kazi kwa ajili ya uzoaji taka mitaani na haina gari hata moja kwani kwa sasa wanakodi magari ya watu kwa ajili ya shughuli ya ukusanyaji taka kutoka kwenye nyumba za watu mitaani.

“Tumekodi magari matatu ya kampuni ya Razak ambayo yanatusaidia kubeba lakini Halmashauri inampango wa kununua magari matano kwa ajili ya uzoaji wa taka, kuna fedha kutoka Serikali Kuu na nyingine tutakopa kutoka benki tukipata kibali hivyo tutanunua magari matano na adha hiyo ndani ya miezi mitatu itakuwa imeisha moja kwa moja,”ameeleza Kibamba.

Aidha ameeleza kuwa katika kuboresha masoko Halmashauri hiyo inatarajia kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa soko kuu la Kirumba ambalo litagharimu kiasi cha bilioni 14 na sasa wameisha tangaza zabuni na wanatarajia kuifungua Machi 5,2024.

“Machi 5,2024 tutafungua zabuni ya ujenzi wa soko kuu la Kirumba na sasa hivi tumeamua kuweka mkazo ama msisitizo katika soko hilo hivyo wafanyabiashara wa soko la Kiloleli waondoe shaka wafanye biashara zao kwa uhuru ,amani lakini walipie kodi ya Halmashauri na serikali kama itabidi kuwaondoa tutawaondoa kwa kukaa nao na kufanya mazungumzo na kujadiliana hadi tufikie muafaka wapi tutawapeleka kwa muda watupishe tupaendeleze pawe nadhifu warejee,”.

Vilevile ameeleza kuwa Ilemela imepokea ushauri wa ujenzi wa majengo ya kwenda juu(ghorofa) kwani ardhi ni chache ingawa changamoto ni uchumi ambapo ujenzi darasa moja gharama yake inakadiriwa kuwa na takribani milioni 50 licha ya kuwa inatunza ardhi hivyo wamependekeza kuanza na ujenzi wa madarasa ya ghorofa kwa shule ya sekondari Kata ya Buzuruga na Ilemela kwa shule moja.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ilemela Willbard Kilenzi amesisitiza Halmashauri kutoachia maeneo ambayo umeisha chukua kwa maslahi ya maendeleo ya wananchi na badala yake wawe na mpango mzuri wa kulipa fidia kwa awamu hii kulipa fidia wananchi wa eneo fulani na awamu nyingine eneo jingine.

“Tuendelee kulipa kidogo kidogo fidia na kuwapa watu matumaini mfano awamu hii tumelipa Kayenze fedha ijayo tufidie Kitangiri,”.

Hata hivyo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilemela Yusuph Bujiku ameelekeza migogoro na malalamiko ya viwanja ,hati na malipo ya viwanja Kata ya Ilemela yafanyiwe kazi haraka na wananchi wanaohitaji hati wape wapimiwe na kama kuna migogoro imalizwe.

“Viongozi wanahusika na jambo hilo akiwemo Mkurugenzi naomba taarifa ya umaliziaji wa migogoro ya viwanja Kata ya Ilemela na kiseke ifike mezani kwenye ofisi ya CCM Wilaya ya Ilemela,” ameeleza.