Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Ileje
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe wamesema wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(Tasaf) wilayani humo wanalazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 100 kufuata huduma za kibenki katika Mji wa Tunduma.
Hvyo wameiomba serikali kushawishi taasisi hizo za kifedha kusogeza huduma karibu wilayani humo.
Hoja hiyo imeibuliwa na baadhi ya Madiwani wa Halmashauri hiyo Agosti 7,2024 katika kikao cha Baraza la Madiwani robo ya nne kilicholenga kujadili ajenda mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa huduma za kifedha kuwa mwiba kwa wanufaika ikichukua sura mpya.
Bahati Kyomo Diwani wa Kata ya Ndola amesema wanufaika wengi wanasafiri kwenda Tunduma kwa ajili ya kupata huduma za kibenki kwani wengi wao wamefunguliwa kadi za benki ambazo huduma hazipo wilayani humo.
“Utakuta mnufaika wa Tasaf anapata fedha 27,000_30,000 anafuata huduma katika Mji wa Tunduma akitoa fedha hiyo nyumbani anarudi na Sh10,000 sasa hii imekuwa kero tunaomba serikali itusaidie kusogeza huduma ambazo wanaufaika wanazitumia,”amesema Kyomo.
Tata Kibona Diwani wa Kata ya Ibaba amesema serikali iwasaidie kushawishi taasisi za kifedha za kibenki kusogeza huduma ili wanufaika kuanza kupata huduma karibu na fedha zao kukidhi matumizi yao.
“Tasaf hii imeanza kuwa mwiba kwa wanufaika kutokana na uhaba wa taasisi za kibenki pamoja na mawakala hali ambayo wanufaika kusafiri umbali wa kilomita zaidi ya 100 na kujikuta fedha yote anatumia kwenye nauli,”amesema Kibona.
Melise Masebo Diwani Vitimaalumu wilayani humo amesema baadhi ya mawakala wasio waminifu wanawaibia fedha wanuifaika wakidai wanawasaidi kutokana na wanufaika wengi hawajui kusoma na kuandika.
Akijibu hoja hiyo Mratibu wa Mfuko wa Maendelelo ya Jamii(TASAF),wilayani humo George Kibona amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo ambayo ilitokana na baadhi ya taasisi ya kifedha kuacha kutoa huduma kwa wanufaika na kupelekea kutafuta taasisi zingine ambazo zinapatikana Tunduma.
“Utaratibu wa malipo wa sasa kwa wanufaika ni kupitia akaunti za benki ,hivyo baada ya benki hiyo kusitisha huduma tuliaamua kuwafungulia akaunti za benki ambazo huduma zake zipo Tunduma ,ambapo zingine zina mawakala ambao wanalalamikiwa kuwaibia wanufaika,” amesema Kibona.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ubatizo Songa amesema changamoto hiyo inatakiwa itatuliwe suluhu mapema ili kuondoa adha wanayokabiliana nayo wanufaika wa Tasaf.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato