December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilala yatenga Bilioni 11 za Mikopo ya Halmashauri

Na Heri Shaaban , TimesMajira Online

MKUU wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo ,amesema Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam imetenga shilingi bilioni 11 kwa ajili ya mikopo ya asilimia kumi inayotolewa ngazi ya Halmashauri ili kuwawezesha wajasiriamali wa Wilaya hiyo waweze kukuza mitaji yao .

Mkuu wa Wilaya Edward Mpogolo ,alisema hayo wakati wa Kongamano la Wanawake wa jimbo la segerea la miaka mitatu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, Kongamano lililoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la segerea Bonnah Ladslaus Kamoli.

“Halmashauri ya jiji imetenga shilingi Bilioni 11 za mikopo ya ngazi ya Halmashauri na katika akaunti kwa sasa kuna Bilioni 8 ifikapo mwaka 2025 Halmashauri hiyo itakuwa na Bilioni 46 za mikopo ngazi ya Halmashauri “alisema Mpogolo.

Edward Mpogolo aliwataka wanawake wa Jimbo la Segerea waandae Utaratibu wao wa kuweza kupata pesa za mikopo na vikundi vyao vinavyotambulika na kufamiana .

Aidha alisema katika mikopo hiyo ya Serikali ya asilimia kumi kuna makundi matatu Vijana,Wanawake na Makundi Maalum na kila kundi wanawake wapo hivyo lazima wawezeshwe .

Akizungumzia mikopo ya ngazi ya Halmashauri ya asilimia kumi pesa zilizokopeshwa awali Bilioni 27 na pesa zilizorejeshwa ni Bilioni 6 bado Bilioni 21 Halmashauri hiyo ya jiji inaendelea kufatilia kwa ushirikiano wa Madiwani wa Ilala ili wananchi waliochukua pesa hizo ziweze kurudi wengine waweze kukopa na kuzirejesha .

Alimpongeza Mbunge wa jimbo la segerea Bonnah Ladslaus Kamoli kwa kuandaa Kongamano la miaka mitatu la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo amesema Mbunge Bonnah ni Mchapakazi atashirikiana naye kwa ajili ya maendeleo.

Katika hatua nyingine Akizungumzia uchaguzi wa Serikali za mitaa Mpogolo aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea muda ukifika wasirudi nyuma kwani wanawake wanaweza .

Aliwataka wanawake wa Segerea kuonyesha umoja na mshikamano kwa upendo na kupendana ili wajenge umoja .