January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilala yataja mikakati ya kuimarisha usafi wa mazingira

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametaja mikakati mitatu inayofaa kutumika ili kudumisha usafi katika Jiji la Dar-es-Salaam, ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara wadogo ‘Machinga’ kufanya biashara katika maeneo yao maalumu waliyopangiwa.

Nyingine ni kuanzishwa kwa mashindano ya usafi kwenye masoko,kila baada ya miezi mitatu na kuimarisha kampeni za upandaji miti na kufanya usafi katika fukwe za Bahari ya Hindi ili kutunza mazingira.

Mpogolo amezungumza hayo Desemba 9,2024, jijini Dar-es-Salaam,baada ya kufanya usafi katika soko la Buguruni na Ilala pamoja na kupanda miti katika fukwe za Dengu zilizopo Kata ya Kivukoni, ikiwa ni kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika.

Ambapo amesema endapo mikakati hiyo itatumika hususani katika maeneo yenye mikusanyiko kama sokoni, itasaidia kuweka mazingira safi na salama kwa afya za watanzania.

Amesema, Halmashauri ya Jiji la Dar-es-Salaam, ambayo ni sura ya Mkoa huo,ina mikakati mbalimbali ya usafi ambayo itatekelezwa ikiwemo kuweka mkazo kwa ‘wamachinga’ kutorejea katika maeneo yasiyo rasmi pamoja na upandaji miti.Huku akisisitizz kuwa hali hiyo ni kuunga mkono juhudi za Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, ambaye amekuwa akisisitiza juu ya upandaji miti.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya, amemuagiza, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, kufanya operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara wadogo waliorudi katika maeneo yaliyokatazwa na kuwarejesha katika maeneo yaliyoelekezwa.

“Nitashiriki kwenye operesheni hii, wamachinga warejee katika maeneo yao tuliyokubaliana,siyo kila eneo Dar-es-Salaam mtu anatakiwa kupanga biashara,Mkurugenzi wa Jiji na wewe ufanye operesheni hiyo ili mji wetu uwe na muonekano mzuri na uliopangika,”amesema Mpogolo na kuongeza:

“Pia Halmashauri ya Jiji la Dar-es-Salaam, kuanzisha mkakati wa kushindanisha usafi katika masoko yote yaliyo ndani ya Wilaya yetu,kila baada ya muda na soko litakaloshinda kwa usafi bora lipewe zawadi na cheti kwani kwa kufanya hivyo italeta motisha ya usafi katika maeneo yetu,”.

Sambamba na hayo,amesema Serikali inaendelea kujenga masoko ya kisasa katika Wilaya hiyo, ambapo miongoni mwa masoko yatakayojengwa ni pamoja na Soko la Ilala.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dar-es-Salaam, Elihuruma Mabelya, amesema kuwa, upo mkakati ambao utaenda kukamilika hivi karibuni wa kufunga taa za barabarani na kamera, lengo likiwa ni kupendezesha na kupandisha hadhi ya Jiji hilo na kuimarisha ulinzi.