January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Igunga watakiwa kujitokeza katika kliniki ya madaktari bingwa

Na Lubango Mleka, Timesmajira Online, Igunga.

WANANCHI wilayani Igunga mkoani Tabora wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika kliniki ya Madaktari Bingwa kutoka hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Nkinga ambao wapo katika hospitali ya Wilaya hiyo kwa siku tano ili kufanyiwa uchunguzi wa kina na kupatiwa matibabu.

Magonjwa ambayo yatachunguzwa na kupatiwa tiba ni upasuaji, magonjwa ya ndani, magonjwa ya kina mama na uzazi, macho,masikio,pua na koo ambapo Madaktari hao watatoa huduma hiyo ambayo imeanza kutolewa Julai 24,2023 hadi Julai 28,2023.

Mganga Mfawidhi hospitali ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora Melchedes Magongo akizungumzia huduma ambazo zinatolewa na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na hospitali ya Rufaa Nkinga ambao wanatoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa siku tano kwa wananchi wa wilaya ya Igunga na maeneo ya jirani.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mganga Mfawidhi hospitali ya Wilaya ya Igunga Melchedes Byabato Magongo amesema kuwa walibaini changamoto na kugundua kuwa wanauhitaji mkubwa wa huduma za kibingwa hivyo wakaanzisha ushirikiano na hospitali zenye madaktari bingwa watakao weza kutoa huduma hizo katika hospitali ya Wilaya hiyo ambapo wananchi wamekuwa wakizifuata katika wilaya na mikoa ya mbalimbali.

“Tulifanya mawasiliano na wenzetu wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na hospitali ya Rufaa Nkinga ambayo ni ya binafsi iliyopo wilayani Igunga na tumefanikiwa,wamefika leo na wameanza kutoa huduma hizi za kibingwa kwa awamu ya kwanza na watatoa huduma hizi kwa siku tano yaani Julai 24,2023 hadi Julai 28,2023,”amesema Magongo.

Kwa awamu hiyo ya kwanza ambayo tumeona kuanza nayo ni huduma kutoka kwa madaktari bingwa katika vitengo vya madaktari wa upasuaji, madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani, magonjwa ya kina mama na uzazi, madaktari bingwa wa macho, madaktari wa masikio na koo.

Baadhi ya wauguzi katika hospitali ya Wilaya ya Igunga wakitoa huduma ya upimaji kwa wagonjwa waliofika kupatiwa huduma ya matibabu ya kibingwa.

Aidha, amebainisha kuwa kwa siku ya kwanza muitikio wa wananchi kujitokeza kupima, kuchunguza na kupatiwa matibabu ya kiafya umekuwa mkubwa sana hivyo amewataka wananchi wilayani Igunga na maeneo jirani kujitokeza ili kuweza kuonana na madaktari hao bingwa.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya kina mama na uzazi kutoka hospitali ya Rufaa ya Nkinga Gilbert Ng’wamkai, amesema kuwa lengo kuu la kufika katika hospitali ya wilaya ya Igunga ni kuboresha mahusiano mazuri waliyonayo kwa lengo la kusaidia wananchi kupata huduma za kibingwa karibu na kuwataka kujitokeza kwa wingi ili kuweza kupatiwa huduma za matibabu hayo.

“Huduma hizi hazipo kibiashara, tupo hapa kuwasaidia wananchi wa Igunga na maeneo ya jirani, kwa hiyo tunawahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuja kupata fursa hii ya matibabu bora na kwa urahisi zaidi,” amesema Ng’ wamkai.

Naye Diwani Vitimaalumu Kata ya Igunga Happy Nyabukika,ni mmoja wa wagonjwa waliofika kupatiwa huduma ya matibabu ya kibingwa, amesema kuwa watu wengi wilayani hapa wanapata tabu sana kwenda kupata huduma hizo hospitali zingine au katika mikoa ya mbali.

Ambapo asilimia kubwa ya wananchi hushindwa kumudu gharama za matibabu, nauli au malazi, hivyo ameiomba Serikali kupita Wizara ya Afya kuipatia hospitali ya Wilaya ya Igunga madaktari bingwa ikiwa ni pamoja na vifaa vya kisasa zaidi ili kuwasaidia wananchi wenye vipato vya chini kupatiwa matibabu ya kibingwa kwa ukaribu.

” Mimi ni mwanafunzi wa sekondari ya St. Marigaret Maria alakok, nimekuja kupima macho, nashukuru huduma ni nzuri nimehudumiwa kwa wakati ninaomba watufikie katika shule zetu ili kutupatia huduma hizi za kibingwa, kwani wanafunzi wengi tuna magonjwa mbalimbali kwa kutufikia watakuwa wametusaidia kutambua na kuyatibu magonjwa yetu mapema,” amesema Sara Ibrahim.

Huku Anthony Salumu akimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo, uongozi wa hospitali ya Wilaya ya Igunga, Madaktari wote bingwa na wauguzi kwa kujitoa na kufanikisha jambo hili la kutoa huduma za matibabu hayo kwa wananchi.

Pia ameomba uongozi kuongeza muda zaidi kwani itasaidia kuwafikia wananchi wengi hasa wa vijijini ambao kwa namna moja ama nyingine hawajapata taarifa ya ujio wa madaktari hao bingwa.