September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Igunga kuanza kunufaika na mtambo wa kutibu maji taka Oktoba mwaka huu

Na Lubango Mleka, Times Majira Online – Igunga.

WANANCHI wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Igunga na maeneo ya jirani Wilaya ya Igunga kuanza kunufaika na mtambo wa kutibu majitaka na topetaka ifikapo mwishoni mwa Oktoba, 2024.

Ikiwa ni hatua ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko yanayotokana na kusambaa kwa taka na maji taka katika maeneo mbalimbali ya halmashauri hiyo.

Akitoa taarifa mbele ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Igunga, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (IGUWASA) Mhandisi Humphrey Mwiyombela amesema kuwa, ujenzi wa mtambo huo ulianza Julai 2023 unatarajia kukamilika Oktoba mwaka huu.

” Pamoja na jukumu la kusambaza maji safi na salama ya kunywa Mjini Igunga, IGUWASA tuna jukumu jingine la kuhakikisha kuwa mazingira yanakuwa safi na salama,”amesema Mhandisi Mwiyombela.

Amesema kuwa katika kuhakikisha Mji wa Igunga unakuwa safi,mamlaka hiyo inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa mtambo wa kusafisha majitaka na topetaka unagharimu kiasi cha bilioni 1.8 fedha kutoka serikalini.

Mhandisi Mwiyombela amesema, mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 23 na kukamilika kwake kutawanufaisha jumla ya wakazi 82, 768 katika vitongoji vya Mji wa Igunga na Wilaya za jirani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Igunga, Mafunda Temanya amesema kuwa mradi huo ni muhimu kwa ustawi wa afya za wananchi wa Igunga na maeneo ya jirani ya Wilaya hiyo, hivyo amewataka IGUWASA kuhakikisha wanamsimamia Mkandarasi vizuri ili amalize mradi kwa wakati.