December 31, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

IGP Sirro ashuhudia gari la RPC Geita likiteketea kwa moto

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro akutana na ajali ya gari la Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita katika eneo la Makurugusi wilayani Chato huku likiungua moto.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi Mwandakizi Henry Mwaibambe amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Amesema, gari hilo lilikuwa likitokea Mjini Geita kuelekea Chato likiwa limebeba afisa mmoja na dereva.

Afisa huyo na dereva wamejeruhiwa na kutibiwa katika Hospitali ya Wilaya Chato na kuruhusiwa.

RPC Mwaibambe amesema kuwa, gari hilo liligongana na mwendesha bodaboda aliyekuwa amebeba madumu mawili yenye mafuta aina ya Dizeli yenye lita 50 kila moja na kulipuka.

Amesema kuwa,gari la RPC, gari la abiria aina ya Hiace iliyokuwa imepaki pembeni,pikipiki,pamoja na mwili wa mwendesha bodaboda vimeteketea kwa moto palepale.

Majeruhi katika ajali hiyo jumla ni 16, ikiwa ni askari 2 na raia 14.

RPC Mwaibambe amesema kuwa, IGP Sirro amekuta ajali hiyo imetokea na amesaidia kuwasiliana na mamlaka za zimamoto na nyingine.