June 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Idadi ya Watalii wa Kimataifa yazidi kuongezeka nchini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kwa siku kama ya leo hii inaweza kuitwa “Mkono wa Eid” Ripoti ya mwezi Mei, 2024 ya Benki Kuu ya Tanzania iliyotolewa jana inaonesha sekta ya utalii “haikamatiki” kwa jinsi inavyoendelea kuweka rekodi za juu kwa idadi ya watalii wa kigeni wanaofurika kuja nchini na pia mapato kama ifuatavyo:

👉🏼👉🏼Watalii waendelea kumimika nchini: Ripoti hiyo ya BoT inaonesha kwa miezi iliyotambulika huko nyuma kama “low season” yaani Machi na April, kwa mwaka huu wa 2024 watalii wa kimataifa wameongezeka kwa asilimia 21.9 na 21.8 mtawalia ikilinganishwa na miezi kama hiyo mwaka jana. “Hali hii ni matokeo ya kuendelea kuimarika kwa sekta ya utalii nchini na duniani.”

Sekta ya Utalii Yaendelea Kuwa Mhimili Fedha za Kigeni: Ukiachilia mbali “mafuriko” hayo ya wageni, katika miezi hiyo pia sekta ya utalii imeendelea kuonesha kuwa mhimili wa fedha za kigeni ikiingiza Dola za Marekani Bilioni 3.58 na 5.75 mtawalia kwa Machi na April mwaka huu 2024 kutoka Dola Bilioni 2.7 na 2.8 kwa miezi kama hiyo mwaka jana 2023. Sekta zinazofuatia ni madini iliyofikia Dola Bilioni 3.1 Aprili mwaka huu na Uchukuzi Dola Bilioni 2.5.

Filamu aliyoshiriki Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya “Tanzania: The Royal Tour” na mwamko wa jumla wa Serikali na wadau wa sekta binafsi katika kujitangaza kimataifa, vinatajwa kuwa msingi wa mafanikio haya.

“Mafanikio na kuimarika kwa sekta ya utalii pia kutaendelea kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa kufikia asilimia 6.3 mwaka huu” anatabiri mwandishi Zephania Ubwani wa gazeti la The Citizen katika makala yake ya Machi mwaka huu yenye anuani isemayo: “Rebound in Tourism Expected To Fuel Tanzania’s Economic Growth To 6.3 Percent”

Ripoti ya BoT inaonesha kuunga mkono utafiti mwingine uliofanywa na Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) kwa robo ya mwezi Januari-Machi, 2024, ambapo kwa ukuaji unaoendelea sasa wa sekta ya utalii nchini Tanzania ilishika nafasi ya kwanza Afrika na ya nne duniani kwa ongezeko kubwa la watalii ikilinganishwa na kabla ya Uviko-19 yaani mwaka 2019.