December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu

Idadi ya waliopona Corona yaongezeka

Na Penina Malundo

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema wagonjwa wengine wawili wamepona Corona nchini, hivyo kufanya idadi ya waliopona ugonjwa huo kufika watano, huku kifo kikiwa ni kimoja.

Amesema kati ya wagonjwa hao Dar es Salaam amepona mmoja na Arusha mmoja, hivyo kufanya Mkoa wa Arusha kuwa hauna mgonjwa hata mmoja mwenye maambukizi ya COVID-19.

Waziri Ummy aliwataka Watanzania waendelee kuzingatia maelekezo ya Wataalam wa Afya ikiwemo kuepuka mikusanyiko na misongamano isiyo ya lazima.

Wakati huo huo, Waziri Ummy amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda vifaa mbalimbali 350 vya kutakasa mikono ikiwemo ndoo za maji, madumu, masks na dawa za kuchanganya kwenye maji kwa ajili ya kuwakinga wananchi dhidi ya vimelea wa virusi vya Corona.

Akipokea vifaa hivyo Dar es Salaam jana, Makonda alisema atahakikisha vinapelekwa sehemu mbalimbali ikiwemo vituo vya daladala, sokoni na sehemu zenye mizunguko ya watu ili waweze kusafisha mikono kabla ya kufanya jambo lolote.

Makonda aliwaelekeza wakurugenzi wote wa Manispaa za Jiji hilo kuhakikisha maji yenye dawa hayamaliziki kwenye ndoo za kunawa mikono.

Pamoja na hayo Makonda amewahimiza wananchi kuendelea kuchukuwa tahadhari dhidhi ya ugonjwa huo akiwaomba viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa.

Msaada huo wa vifaa 1,000 umetolewa na mfanyabiashara Subash Patel chini ya Umoja wa Wafanyabiashara Wazawa kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, ambapo kwa Dar es Salaam wamekabidhi vifaa 350 na vifaa vingine 650 vilivyosalia vitasambazwa nchi nzima.

ATC-WAZALENDO WAJA KIVINGINE

Katika hatua nyingine Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Maalim Seif Sharif Hamad, wameunda timu ya ufuatiliaji ugonjwa wa Corona nchini.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Chama hicho, Ado Shaibu, wajibu wa jumla wa timu hiyo ni kufuatilia kwa karibu shughuli za Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa Corona.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo timu hiyo ina wajumbe na kwamba itakuwa na jukumu la kutoa ushauri kwa Chama kuhusu namna bora ya kuhamasisha umma kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo na kuratibu mikakati yote ya Chama kwa ajili ya kukabiliana na Corona.

“Kutokana na madhara ya Corona kuwa makubwa tumeona ni muhimu kuwa na uratibu wa suala hili. Tumeamua kuwa na timu itakayofuatilia masuala haya yote,” alisema Ado

Taarifa hiyo ilieleza kwamba timu hiyo itaongozwa na Dorothy Semu na Juma Duni Haji. Kwa mujibu wa taarifa hiyo watu hao wamechaguliwa kutokana na uzoefu wao, kwani Duni Haji Duni aliwahi kuwa Waziri wa Afya katika Serikali ya Zanzibar na Semu aliwahi kuwa mfanyakazi wa Wizara ya afya Tanzania Bara.

Wajumbe wengine ni Janeth Fusi, Salim Bimani,Pavu Abdallah,Janeth Rithe na Mbarala Maharagande, huku Issa Kheri na Seif Abalhassan wakitangazwa kuwa makatibu wenza wa timu hiyo.

TAMWA YAJITOA VITA YA CORONA

Wakati huo huo, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), kimeihadharisha jamii juu ya ongezeko la ukatili wa wanawake na watoto unaoweza kukithiriwa katika janga la ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na kirusi aina ya Corona.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Rose Reuben alisema kutokana na Serikali kufunga shule na watoto kubaki nyumbani wakati huu wanatakiwa kuangaliwa kwa umakini zaidi.

Alisema wazazi au walezi ambao hawatakuwa makini kipindi hki huenda wakasababisha watoto wao wakaathirika na ubakaji na kupata mimba za utotoni.

Alisema katika kipindi hiki ambacho macho na masikio yapo katika kudhibiti virusi vya Corona watu wengine wanaweza kutumia nafasi hiyo kuwafanyia watoto vitendo vya ukatili .

“TAMWA inaipongeza Serikali kwa kuchukua hatua za haraka za kufunga shule ili kupunguza msongamano unaoweza kusababisha maambukizi,hata hivyo ni muhimu kuihadharisha jamii kuhusu ukatili wa kijinsia,” alisema Reuben

Alisema endapo wazazi au walezi hawatawasimamiwa vizuri watoto katika kipindi hiki cha siku 30 zilizotolewa na Serikali kupitia Waziri Mkuu,Kassimu Majaliwa nchi inaweza kutengeneza kizazi kingine kilichoathirika na ukatili wa aina mbalimbali ikiwamo ubakaji,ulawiti na mimba zisizotarajiwa.

“Ni muhimu kwa wazazi na walezi kuwalinda watoto na virusi vya Corona, lakini wakati huo huo tuangalie madhara wanayoweza kuyapata watoto wa kike na wakiume wanapokuwa nyumbani au mitaani,”alisema na kuongeza;

“Tunapaswa kujiuliza iwapo watoto wetu kama wapo salama wawapo nyumbani au mitaani wanapotembea wakati huu wa likizo ndefu kama watu wenye tabia mbaya hawawanyemelei, ndugu na jamaa wanaobaki na watoto hawa wanawalinda au wanawaharibu?Je watoto hawa hawatakuwa katika hatari ya kuozwa mapema?” Alihoji Reuben

Alisema TAMWA inaiomba Serikali, wadau na watunga sera kwanza,kutosahau hatari nyingine zinazoweza kuwapata wanawake na watoto katika kipindi cha janga la Covid-19.

Reuben alisema wadau wa afya,elimu na watoto kutoa mafunzo kuhusu namna ya kujilinda na ya kuripoti kuhusu ukatili kwa watoto wakati huu wa mlipuko na kuongeza upatikanaji wa taarifa na misaada mingine kwa watoto.

Pia alisema huu ni wakati wa kubuni mfumo wa kuwapa watoto elimu wawapo nyumbani na wahudumu wa afya wanawake wawekewe mazingira salama ya kutoa huduma ili wasiathirike.

DALADALA 35 MBARONI

Mkoani Morogoro, Mwandishi Wetu, Severin Blasio, Morogoro anaripoti kuwa Polisi wamekamata daladala 35 kwa kosa la kukiuka agizo linalowataka wamiliki wa magari hayo kuweka vifaa kinga vya ugonjwa wa Corona.

Magari hayo yalikamatwa kufuatia operesheni ya kushtukiza iliyoendeshwa na Polisi ili kuhakikisha kila daladala inakuwa na vifaa hivyo, ambavyo ni ndoo yenye maji na sabuni ili kuwakinga abiria na maambukizi ya Corona 19 .

Akitoa ufafanuzi baada ya magari hayo kukamatwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mtafungwa, alisema magari yaliyokamatwa ni yale yanayofanya safari kutoka katikati ya mji kuelekea Kihonda, Mkundi ,Azimio, Yespa na Manyuki.

“Leo (jana) tumefanya operesheni ya kushtukiza kwa ajili ya kukagua daladala kama zinatii agizo la Serikali la kuhakikisha kila gari linakuwa na vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa virus vya Corona kwenye operesheni hiyo tumebaini na kukamata magari 35 ambayo yameonekana kukiuka agizo la Serikali,” alisema Kamanda Mtafungwa.

Kufuatia kukamatwa kwa magari hayo Kamanda Mtafungwa alitoa wito kwa vyombo vyote vya usafiri kuhakikisha vinatimiza agizo hilo kuepuka mkono wa sheria.

Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Manispaa ya Morogoro, Andrew Msofe, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo huku akiwasisitiza madereva wa daradara kuhakikisha wanatimiza maagizo ya Serikali kuepusha usumbufu wa kukamatwa.