December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ICAP yampongeza Rais Samia uwekezaji elimu ya udhibiti dawa za kulevya

Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Mwanza


SHIRIKA la Kimataifa la ICAP Tanzania,limempongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika elimu ya kudhibiti matumizi na uingizaji wa dawa za kulevya nchini.

Pongezi hizo limetolewa Juni 30,2024 jijini Mwanza na Mkurugenzi Mkaazi wa ICAP nchini, Haruka Maruyama alipozungumza katika kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya kupiga vita dawa za kulevya yaliofanyika mkoani hapa.

Amesema Watanzania watakuwa salama kupitia elimu hiyo, watafahamu athari na madhara ya dawa za kulevya kiafya,kijamii na kiuchumi kwa sababu dawa hizo zina athari kwa mtumiaji.

Maruyama amesema maadhimisho ya siku ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya ni mahususi katika kutafuta changamoto na mbinu za kupambana na dawa hizo kati ya serikali na wadau.

Mkurugenzi huyo wa ICAP nchini amesema ushirikiano kati ya serikali na mashirika mbalimbali yaliyo katika mnyororo wa kupiga vita dawa za kulevya umeimarika.

Aidha ushirikiano huo umetoa fursa kwa mashirika hayo kutoa huduma za afya na elimu kwa waraibu wa dawa za kulevya ikiwemo kuwapa elimu ya ujasirimali ili wakishapona wapate kazi ya kijiingiza kipato na kukukuza uchumi wao na taifa ka ujumla.

“ICAP kwa miaka 20 tunatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii nchini Tanzania kupitia ufadhili wa CDC na PEFAR,hivi karibuni serikali imezindua taarifa ya mradi wa utafiti wa viashiria vya Ukimwi na matokeo ya Ukimwi (THIS 2020-2024) mkoani Morogoro,”amesema Maruyama.

Amesema kupitia kiliniki ya Waraibu (MAT),jumla ya waraibu 770 wamehudumiwa kupitia methadone na waliokuwa wakisumbuliwa na matatizo ya afya ya akili wengi wakiwa ni waraibu wa dawa za kulevya wamenufaika kwa kupatiwa huduma ya matibabu ambapo kwa sasa tatizo hilo limepungua.


Pia ameahidi kuwa ICAP itaendelea kushirikiana na serikali kufanya na kutafuta wafadhili ili kuunga mkono serikali ya kuleta maendeleo.