Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
SHIRIKA la ICAP limeikabidhi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC), maabara ya lupima usugu wa dawa za kufuba Virusi Vya Ukimwi (VVU),itakayohudumia mikoa nane ikiwemo mitano ya Kanda ya Ziwa.
Mkurugenzi Mkazi wa ICAP nchini, Haruka Maruyama,amesema ICAP kwa msaada wa kiufundi kutoka Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC) na ufadhili wa Serikali ya Marekani chini ya Mfuko wa Rais wa Dharura wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR),imekabidhi maabara hiyo BMC.
Amesema kuanzishwa kwa maabara hiyo ni hatua muhimu katika kuhakikisha ubora wa huduma za VVU Kanda ya Ziwa na mikoa jirani,hivyo kitakuwa kituo cha kiwango cha juu katika kudhibiti janga la VVU.
“Ushirikiano uliopo umewezesha ICAP kusaidia kwa kiwango kikubwa maabara ya hospitali ya Bugando kuwa kitovu kikuu cha upimaji na hazina ya utafiti wa athari za VVU Tanzania,kwa uwezo wa maabara hiyo upimaji wa uchunguzi wa vinasaba kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na mingine jirani umekuwa na mabadiliko makubwa,”amesema Maruyama.
Amesema maabara hiyo mpya imefikia hatua muhimu ya kuboresha huduma ya matibabu na katika mapambano dhidi ya VVU, hivyo ICAP nchini Tanzania, kupitia msaada wa CDC,itaendelea kusaidia BMC na Wizara ya Afya katika afua mbalimbali za afya kwa umma.
Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda,ameishukuru Serikali ya Marekani kupitia PEPFAR na CDC kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kusaidia mapambano ya UKIMWI,kutoa vifaa tiba na kuboresha huduma za afya nchini hususani mkoani humo.
Amesema jitihada hizo zimewezesha kupunguza maambukizi ya VVU mkoani Mwanza kutoka asilimia 7.2 mwaka 2016/17 hadi asilimia 4.7 mwaka 2022/23 kwa mujibu wa taarifa ya utafiti wa viashiria na matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2022-2023 (THIS 2022-2023).
Mtanda amepongeza jitihada hizo za kuboresha maabara ya kupima usugu wa dawa za kufubaza VVU itakayotumika kusaidia kuboresha huduma za matibabu kwa jamii na watu wanaoishi na virusi hivyo.
Awali Mkurugenzi Mkazi wa CDC nchini,Dr Mahesh Swaminathan amesema miaka zaidi ya 15,PEPFAR kupitia CDC imesaidia BMC na kuimairisha mifumo ya afya ya maabara katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
“Ushirikiano wetu na Bugando kupitia teknolojia ya hali ya juu imebadilisha maabara hiyo kuwa chombo endelevu kinachojiendesha, kinachotoa huduma za maabara za kiwango cha juu katika mikoa zaidi ya nane na kupanua huduma kwa nchi jirani kama DRC na Burundi.Tangu mwaka 2022, PEPFAR na CDC kupitia ICAP zimetoa zaidi ya Dola za Marekani 750,000 (takribani shilingi za Kitanzania bilioni 1.942 kusaidia ujenzi wa maabara ya vinasaba ya BMC iliyoanzishwa kufanya shughuli upimaji,” Dr.Mahesh.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa, Dr.Thomas Rutachunzibwa amelishuruku Shirika la ICAP kwa kuendelea kutekeleza mradi wa FIKIA+ wa Afua za UKIMWI,unaotekelezwa katika Wilaya saba mkoani humo ili kuimarisha huduma za tiba na matunzo kwa wanaoishi na VVU.
Mkurugenzi wa BMC,Dr.Fabian Massaga amesema maabara hiyo italeta mazingira rafiki kwa wanafunzi na wanasayansi mbalimbali nchini kufanya mafunzo na tafiti zitakazoleta mapinduzi chanya katika huduma za afya na kuomba ushirikiano huo uwe endelevu katika kutoa huduma za afya na matibabu kwa jamii.
More Stories
Rais Mwinyi aipongeza NMB
Wananchi wa Ikuvilo watakiwa kujitokeza kuhakiki taarifa zao
Watanzania wahimizwa kutenda mema