March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

IAA kuwapatia vijana elimu ya fedha

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOnline,Dodoma

CHUO cha Uhasibu Arusha (IAA),kimesema changamoto kubwa inayowakabili vijana wengi nchini katika safari ya kujiajiri ni ukosefu wa elimu ya fedha na elimu ya rasilimaliwatu.

Hayo yamesemwa  jijini hapa leo Februari 20,2026 na Mkuu wa Chuo hicho Prof. Eliamani Sedoyeka,wakati akizungumza  na waandishi wa habari kuhusu miradi ya maendeleo na fursa kwa vijana ambapo amesema vijana wengi wana ujuzi wa kitaaluma na kiufundi, lakini wanakosa maarifa ya namna ya kuugeuza ujuzi huo kuwa fursa ya ajira binafsi na chanzo cha kuajiri wengine.


“Vijana wana ujuzi, lakini changamoto imebaki katika namna ya kubadilisha ujuzi huo kuwa ajira kwa kujiajiri wenyewe na hatimaye kuajiri wengine,” amesema Prof. Sedoyeka.

Kutokana na hayo Prof.Sedoyeka amesema kuwa Chuo hicho kimejikita katika kuwaandaa vijana kwa kuwapatia elimu ya fedha na ujuzi wa biashara ili waweze kujiajiri na kujitegemea.”Vijana wengi wana ujuzi  wa kitaaluma  na kiufundi, lakini wanakosa maarifa ya namna ya kuugeuza  Ujuzi huo kuwa fursa ya ajira na chanzo cha kuiiajiri,”amesema.

Hivyo Prof. Sedoyeka amesema  Chuo hicho pamoja  na kuwa  na Mitaala inayokidhi mahitaji ya wakati ya Soko la Ajira, IAA imewajengea uwezo wa wanafunzi kuanzisha miradi yao kupitia IAA kituo cha biashara ambapo baadhi ya wanafunzi wameanzisha biashara ndogo ndogo ambazo zinaendelea kukua.

Amesema katika mwakabwa masomo ulioisha wameweza kuwafikia zaidi ya vijana  8600 kati yao Vijana 1520 walibuni mawazo mbalimbali ya biashara na kufanikiwa kuanzisha biashara zaidi ya 50 ambapo katika  hizo Kampuni 12 zilisajiliwa.Katika hatua nyingine, amesema IAA ni miongoni mwa taasisi za umma zilizonufaika na Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), unaofadhiliwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka World Bank kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Amesema chuo hicho kimepata Shilingi 48,469,498,473/= kupitia mradi huo kwa ajili ya kuboresha miundombinu, kuendeleza mitaala na kuongeza fursa kwa vijana nchini.

Kwa mujibu wa Prof. Sedoyeka, fedha hizo zimeelekezwa katika maeneo ya kipaumbele ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, mapitio ya mitaala ili iendane na mahitaji ya soko la ajira, kuimarisha matumizi ya teknolojia na TEHAMA, pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa chuo.

Katika kuimarisha uhusiano kati ya chuo na sekta ya ajira, IAA imeunda Kamati ya Ushauri ya Kisekta (Industrial Advisory Committee) itakayosaidia kutoa ushauri katika maandalizi na mapitio ya mitaala ili kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi unaohitajika katika mazingira halisi ya kazi.

Aidha, chuo hicho kimesaini jumla ya Hati za Makubaliano ya Ushirikiano (MoUs) 23 na taasisi mbalimbali za umma na binafsi, ikiwemo CEOs Round Table, kwa lengo la kuwapatia wanafunzi fursa za mafunzo kwa vitendo (internship), mafunzo ya vitendo kazini (field attachment), pamoja na kushiriki tafiti zinazolenga kutatua changamoto halisi za biashara na uchumi.

Kwa upande wa maboresho ya mitaala, Prof. Sedoyeka amesema IAA imekamilisha mapitio ya mitaala 15 kwa gharama ya takribani Shilingi milioni 160, huku Shilingi 446,000,000/= zikitengwa kwa ajili ya mapitio na utengenezaji wa mitaala mipya. Mitaala iliyofanyiwa mapitio ni pamoja na Sayansi ya Kompyuta, TEHAMA, Benki, Bima, Fedha na Mikopo.

Amesema mapitio hayo yamekidhi matakwa ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kuthibitishwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTIVET).