Na Catherine Sungura,TimesMajira online,Morogoro
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ameagiza majengo yote ya vituo vya kutolea Huduma ambayo bado hayajaanza kutoa Huduma za afya kote nchini kuanza Mara moja kutoa Huduma za mama na mtoto ikiwemo utoaji wa chanjo ili kupunguza changamoto za afya.
Dkt.Gwajima ameyasema hayo jana mkoni Morogoro wakati akifungua maadhimisho ya wiki ya chanjo ambayo Kitaifa yamefanyika Kwenye viwanja vya Chamwino.
Dkt. Gwajima amesema kuwa yapo majengo mengi yamejengwa lakini hayajaanza kutoa huduma za Magonjwa ya nje (OPD) na kuagiza yaanze Sasa kutoa huduma za mama na mtoto ikiwemo Chanjo ili kuwapunguzia mwendo mrefu akina mama wajawazito na Watoto.
Kwa upande wa maadhimisho ya wiki ya Chanjo Dkt. Gwajima amesema madhumuni ya wiki hii ni kuhamasisha na kuelimisha Jamii kuhusu umuhimu wa huduma za Chanjo Katika kukinga Magonjwa yanayozuilika kwa Chanjo na kuepusha vifo vinavyoweza kuzuilika kwa Chanjo.
“Ninawahimiza familia kuwapeleka Watoto wote wanaostahili kupata Chanjo Katika vituo vinavyotoa huduma za afya vya Serikali na binafsi ili Watoto wapate chanjo” amesema.
Ameongeza kuwa chanjo ni mkakati muafaka Katika kutokomeza Magonjwa na kupunguza vifo hususan vya Watoto wa chini ya miaka mitano na hivyo kupunguza gharama kubwa ambazo familia zetu na Taifa kwa ujumla ingetumika Katika kutibu maradhi yatokanayo na Magonjwa yanayozuilika kwa Chanjo.
Dkt. Gwajima ameyataja Magonjwa yanayokingwa ni pamoja na Kifua Kikuu,Dondakoo, Kifaduro, Polio, Surua, Rubella, Pepopunda, Hima ya Ini, Homa ya Uti wa Mgongo,Pepopunda,Nimonia/Kichomi, Kuhara na Saratani ya mlango wa kizazi.
“Chanjo huzuia takribani vifo milioni 2 Hadi 3 kila mwaka kutokana na maradhi yanayozuilika kwa Chanjo duniani,na hapa nchini mafanikio ya chanjo tumefanikiwa kutokomeza Ndui,Dondakoo,Kifaduro,Polio na Pepopunda na wodi za wagonjwa wa Surua zimefungwa” ameongeza Dkt.Gwajima.
Aidha, ametaja takwimu za hivi karibuni zinaonesha kwa miaka mitano mfululizo kiwango Cha uchanjaji Kitaifa ni zaidi ya asilimia 95 na hivyo kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri Katika utoaji wa huduma za Chanjo.
“Kiwango hiki Cha uchanjaji hapa nchini pamoja na Afua zingine na kuwezesha nchi kufikia lengo Namba 4 la Malengo ya Mikenia(SDG 4) kwa kupunguza vifo vya Watoto chini ya umri wa miaka mitano kwa theluthi 2/3” amesema.
Hata hivyo Dkt. Gwajima amesisitiza kila mwananchi anawajibu wa kuhakikisha mtoto wake mtoto wa jirani ambaye hajapata au kukamilisha chanjo anapata chanjo kulingana na ratiba kwani mtoto asiyepata chanjo ni hatari kwa afya yake na afya ya Jamii inayomzunguka sababu anaweza kuambukizwa Magonjwa na kuambukiza wengine sababu ya kukosa Kinga.
Maadhimisho ya wiki ya chanjo huadhimishwa kila mwaka kuanzia Aprili 24 hadi 30 na kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Jamii iliyokingwa, Jamii yenye afya Bora” .
More Stories
Gavu aanika miradi iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita Geita
RC Makongoro: Samia aungwe mkono nishati safi ya kupikia
TAKUKURU,rafiki yanufaisha wananchi Mwanza