Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa huduma ya maji inaendelea kuimarika jijini Mwanza kufuatia miradi inayoendelea kutekelezwa pamoja na kadri inavyo kamilika.
Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza(MWAUWASA) inatekekeza miradi maeneo mengine ili kuboresha huduma kwenye maeneo yake ya kihuduma ambapo kwa Jiji la Mwanza inatekeleza mradi wa kuboresha huduma ya maji kwa matokeo ya haraka (Quick Wins) wenye gharama bilioni 4.7.
Mradi huo utaongeza mtandao wa bomba kwa umbali wa kilomita 49.4 kwa maeneo ya Buswelu, Kahama na Nyamadoke wilayani Ilemela na kwa upande wa Nyamagana bomba zitalazwa umbali wa kilomita 11.58 katika eneo la Luchelele na eneo la Igudija wilayani Magu bomba zitalazwa kwa umbali wa kilomita 3.5.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) Neli Msuya wakati wa mapokezi ya shehena ya mabomba yenye ukubwa wa inchi 12 kwa ajili ya kuendeleza mtandao wa usambazaji maji kwa umbali wa kilomita 6.9 kutoka eneo la Buswelu hadi Ilalila wilayani Ilemela.
Neli amewaomba wananchi waendee kushirikiana na MWAUWASA kwani miradi ya kuboresha huduma ya maji inaendelea kutekelezwa maeneo mbalimbali na kadri inavyokamilika ndipo huduma nayo inaendelea kuimarika.
Amesema utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 53 na kwamba mtandao wa bomba umbali wa kilomita 14 umelazwa na matarajio ni kukamilisha mradi ifikapo Desemaba 15.
“Tunafanya kazi kwa kasi ili Desemba 15 tuwe tumekamilisha mradi hasa ikizingatiwa kwamba tunaelekea kwenye msimu wa mvua nasi hatutaki kuwa na kikwazo kwani fedha tayari tunayo, nguvu kazi ipo ya kutosha na tunashirikiana kwa karibu na viongozi wa maeneo husika na jamii,” amesema.
Pia amesema miradi inafadhiliwa na Serikali kwa asilimia mia moja ikiwa ni jitihada za Rais. Samia za kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wake kwa kuwapatia fedha za kuimarisha huduma ya maji kwenye maeneo wanayoyahudumia.
Sanjari na hayo amesema kwa sasa MWAUWASA itafungua Madawati ya Huduma kwa Wateja kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano na wananchi, kufikisha elimu na kutoa taarifa za hatua mbalimbali za ujenzi wa miradi kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo husika.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Shibula, Swila Dede ameishukuru Serikali kwa niaba ya wananchi wake kwa mradi wa maji ambao amesema unakwenda kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wa kata hiyo.
“Rais Samia Suluhu Hassan alituahidi na tunashuhudia anatekeleza kwa vitendo hivyo hatuna budi kumpongeza na kumshukuru kwa mengi anayoendelea kutufanyia ikiwemo hili la maji,” amesema Swila.
Diwani wa Kata ya Buswelu, Sarah Ng’hwani amesema kata yake ilikuwa ikikabiliwa na upungufu wa huduma ya maji hata hivyo anasema kupitia jitihada za Serikali zinazoendelea tayari kuna ahueni ya upatikanaji wa maji na jitihada zinaendelea.
“Tunaishukuru serikali kupitia Waziri wa Maji, kwakweli anasema na kutenda alipita hapa na alituahidi kufanyia kazi changamoto hii na hapa tumeshuhudia yakitendeka,tunasema ni Wizara inayotekekeza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)kivitendo,” amesema
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi