Na Martha Fatael, TimesMajira Online, Moshi
SERIKALI imesema kuzinduliwa kwa huduma ya internet katika kilele Cha mlima Kilimanjaro itaongeza kasi ya watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani kupanda mlima huo.
Aidha huduma hiyo ni sehemu ya kuungwa mkono kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kufuatia filamu ya Royal tour aliyoizindua mapema mwaka huu.
Waziri wa habari, Mawasiliano na teknolojia ya Habari,Nape Nnauye amesema hayo wakati anazindua safari ya watu 41 akiwamo yeye kupanda mlima huo kuzindua internet mnamo Desemba 13 mwaka huu.
Amesema awali watalii kutoka mataifa mbalimbali walikuwa wakipata changamoto ya Mawasiliano hususani ya internet pale ambapo wanahitaji kuwasiliana na ofisi ama familia zao.
“Sasa watalii watakuwa na uwezo wa kuwasiliana na ofisi ama familia zao bila kusubiri washuke mlimani baada ya safari zao za siku sita,huu ni ushindi katika sekta ya Utalii” amesema.
Amesema internet ni sehemu ya kuifungua zaidi Tanzania katika nyanja za utalii ambapo watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani sasa wanaweza kupata Internet yenye kasi zaidi.
Katika safari hiyo Waziri anaambatana na baadhi ya watumishi kutoka wizara ya Habari, shirika la Taifa la Mawasiliano (TTCL) wageni wengine pamoja na waandishi wa habari.
Waziri Nape amesema Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kusimika huduma ya internet katika kilele kirefu zaidi barani Afrika.
Amesema mradi huo uliojengwa katika vituo vya kupanda mlima huo Kwa urefu wa Km 44.7 umetekelezwa na wahandisi wa kitanzania ulianza Julai 22 na kukamilika Disemba mwaka huu.
Mapema mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Zuhura Muro alisema kuzinduliwa kwa huduma hiyo kutawezesha watalii na wageni wengine ambao hawapati Muda wa kupanda mlima Sasa watapanda.
Kwa upande wake mkurugenzi wa TTCL, mhandisi Peter Ulanga alisema mradi ulianza mwezi Agosti mwaka huu kwa kuzindua internet katika vituo vya Mandara, Horombo na Kibo.
Amesema waliahidi kufika vilele vya Gilman s, Stella na Uhuru ambapo alipongeza wizara ya maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake kwa kukubali mitambo hiyo kufungwa katika maeneo yao.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa