Na Yusuph Mussa, Korogwe
KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Paul Makonda amehakikishiwa kuwa mradi wa maji wa Miji 28, kwa Mkoa wa Tanga wenye miji minne ya Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani, utakamilika Desemba mwaka huu badala ya Aprili, 2025.
Hayo yamesemwa Januari 21, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM) Mhandisi Yohana Mgaza wakati akitoa taarifa ya mradi huo eneo la Kwamdulu kulipowekwa mabomba ya ambapo Makonda alifika kuangalia mabomba hayo.
“Mradi huu ulikuwa ukamilike kwa miaka miwili hadi Aprili 30, 2025, lakini kutokana na kasi yetu, mradi huu utakamilika kabla ya miaka hiyo miwili,tunatarajia kukamilisha mradi Desemba 31, 2024,” amesema Mhandisi Mgaza.
Mhandisi Mgaza amesema mradi huo utakaogharimu bilioni 171 ambao utakuwa na mtandao wa mabomba utakaosafirisha maji hayo hadi kwenye miji minne wenye urefu wa kilomita 189, huku mabomba ya kusambaza maji hayo kila mji mmoja ni urefu wa kilomita 25.
Wakati bomba zitakazosafirisha maji kutoka kwenye chanzo cha maji cha Mto Pangani Kijiji cha Mandera wilayani Korogwe, yatakuwa ya inchi 20 hadi 24 huku mabomba yatakayosambaza maji kwenye miji hiyo yatakuwa ya inchi nane (8) hadi inchi 20.
“Hadi sasa mradi umetekelezwa kwa asilimia 20 na mabomba makubwa yameshalazwa kwa umbali wa kilomita 105,tayari ujenzi ukiwa kwenye hatua mbalimbali unaendelea ikiwemo ujenzi wa banio (intake) na chujio (sehemu ya kutibu maji),”.
Pia ameeleza kuwa kuna ujenzi wa matenki Vibaoni, Bongi na Michungwani Wilaya ya Handeni,Kwafungo na Kilulu Wilaya ya Muheza,Madanga, Boza na Tungamaa Wilaya ya Pangani.
Makonda ameridhika na hatua hiyo na kazi zinazofanywa kwenye mradi huo huku kusema hizo ni jitihada za Serikali ya kuwapatia wananchi maji ya uhakika.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi