November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hospitali za binafsi: Wanachama NHIF puuzeni uzushi, njooni mpate huduma

Na Penina Malundo,TimesmajiraOnline, Dar

HOSPITALI binafsi zimewataka wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kupuuza taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba hazitoi huduma kwao, kwani zimeendelea kupokea wagonjwa na hakuna changamoto au ugumu wowote wanaoupata wagonjwa kuhusiana na suala zima la kupatia matibabu.

Msimamo huo umetolewa kwa nyakati tofauti na hospitali binafsi kufuatia taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa wiki, kwamba hospitali hizo zimesitisha kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF kwa kutokubaliana na kitita kipya cha mafao cha mwaka 2023.

“Tunaendelea kupokea wateja wetu ambao ni wanufaika wa NHIF na tunawataka waendelee kufika hospitali bila wasiwasi wowote, wapuuze taarifa hizo kwamba hospitali za binafsi hazipokei wagonjwa ambao ni wanufaika wa Mfuko wa NHIF na hasa Masana.”

Kauli hiyo imetolewa jana na Daktari wa Kitengo cha Wagonjwa wa Nje Hospitali ya Massana, iliyopo Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam, Dkt. Yusuph Ngesi, alipokuwa akizungumzia madai kuwa hospitali binafsi zimesitisha huduma kwa wanufaika wa NHIF.

Dkt. Ngesi amesema taarifa kwamba hospitali binafsi zimesitisha kutoa huduma kwa wateja wa NHIF ni mpya kuisikia.

“Kiuhalisia hiyo ni habari mpya kuisikia, sisi kama watoa huduma za afya Hospitali ya Masana na hata hapa tupo katika kitengo cha wagonjwa wa nje, tumeendelea kuwapokea wagonjwa wa bima ya afya  bila changamoto yoyote na hakuna zuio lolote la kupokea wagonjwa ambao ni wanufaika wa NHIF,” amesema Dkt. Ngesi na kuongeza;

“Hata sasa hivi nimetoka kuona wagonjwa ambao ni wanufaika wa NHIF na wamepata huduma stahiki zinazotolewa na hospitali.”

Alipoulizwa hizo taarifa kwamba hospitali binafsi zimesitisha kutoa huduma kwa wanufaika wa NHIF zinaweza kuwa zimetokana na nini, Dkt. Ngesi alijibu;

“Labda kwa sababu kuna uhakiki unaoendelea unaofanywa na mfuko,  pengine kuna wapokea huduma baadhi wamekataliwa kupatiwa huduma kutokana na changamoto kwenye mifumo yao ya kadi za bima ya afya.

Nasema baadhi kwa sababu mimi hapa kwetu hatujawahi kupata changamoto hiyo, labda kuna changamoto hiyo kwa mgonjwa mmoja, wawili, lakini hamna zuio kwamba wagonjwa ambao ni wanufaika wa NHIF wasifike hospitali kupatiwa huduma za afya au wanaofika warudi, wagonjwa wote wanapokelewa na wanapatiwa huduma.’

“Tunaendelea na tutaendelea kupokea wagonjwa na hakuna zuio lolote la kutowapokea wagonjwa na hakuna changamoto wala ugumu wowote ambao wanapata wagonjwa ambao wanafika kupata matibabu,” amesema Dkt, Ngesi.

Dkt. Ngesi alipoulizwa Hospitali ya Massana kama mtoa huduma mahusiano yake na NHIF yakoje, alijibu;

“Mahusiano ni mazuri, kama kuna changamoto kuna vikao vinaendelea kati ya mtoa huduma na NHIF na vikao vinahusisha watu wawili na havitakiwi kuathiri upatikanaji wa huduma kwa mteja.

Naamini watu wameweza kuona vikao vinaendelea , tulikuwa na kikao na NIHF wiki iliyopita na hata juzi na kwa wakati wote Mfuko wa Afya unapokuwa na changamoto na hivyo vikao, wateja hawajawahi kukutana zuio lolote la kupata huduma, wanaendelea kupata huduma stahiki bila kupata changamoto yoyote.

***Hospitali ya Kairuki

Kwa upande wa Hospitali ya Kairuki, imesema taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa hospitali binafsi zimesitisha huduma sio za kweli, kwani zinaendelea kama kawaida hospitalini hapo.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Hospitali ya Kairuki, Arafa Juba, amesema;

“Hizo jumbe zinazotembea katika mitandao ya kijamii sio za kweli, kwani huduma zinaendelea kama kawaida katika hospitali yetu (Kairuki).”

Juba alizidi kufafanua kuwa; “Hizi Clip zinazotembea katika mitandao ya kijamii ni za uongo.

Hakikisha unafatilia hili, kuna watu wanapotosha haya mambo,maana hata ukienda hospitalini kwetu sisi tuna zoezi la kuhakiki kadi za NHIF pale pale hospitali na hao watu wa NHIF wapo.”

Amesisitiza kwamba wao wanaendelea kupokea kadi za NHIF kama kawaida na hakuna mgonjwa au mteja ambaye amekataliwa na kusitishiwa huduma yoyote ile.

***Dkt. Muganyizi Hospitali ya Kairuki

Kwa upande wake Dkt. Muganyizi Kairuki, amesema wanaendelea kuwahudumia wanachama kama kawaida, hivyo wafike na huduma watapata.

Alisema mazungumzo yaliyopo kati ya NHIF na watoa huduma hayana athari yoyote kwa wanachama kwenye kupata huduma.

***Hospitali ya Harmony Memorial Polyclinic

Naye Msimamizi Mkuu wa Hospitali ya Harmony Memorial Polyclinic, Khalifan Binasi, amesema katika kituo chao wao wanaendelea kutoa huduma hizo za NHIF kama kawaida na hawajasitisha huduma hiyo.

“Sisi tunaendelea na huduma ya NHIF kama kawaida hata sasa hivi unaweza kuja ukatibiwa bila shida yoyote ile,”amesema na kuongeza;

“Asilimia kubwa ya wateja wetu ni watu wanaotumia kadi za bima ya afya za NHIF, hivyo hatuwezi kusitisha kutoa huduma kwa wananchi ambao ndio wateja wetu wakubwa.”

***Legency

Mmoja wa wafanyakazi wa ngazi za juu katika Hopitali ya Legency ya Jijini Dar es Salaam, akizungumza kwa sharti la jina lake kutoandikwa amesema wao wanaendelea na huduma kwa wanachama wa NHIF kama kawaida na wanapokea kadi hizo.

Amesema watu wa mitandaoni sio watu wa kuwafuatilia, kwani ni waongo, kwani hospitali yao haijawahi kuacha kupokea kadi za wateja wa NHIF baada ya mabadiliko kwenye kitita cha kipya cha mafao cha 2023.

“Sisi hatujaacha kupokea hizi kadi na wateja wetu wanamiminika na kadi za NHIF kama kawaida na wewe ukitaka kuja njoo huduma hii ya NHIF inaendelea kama kawaida,”alisema.

***Hospitali ya Moyo Safi

Kwa upande wa Hospitali ya Moyo Safi ya Msewe, Ubungo,Micdit Polyclinic Hospital iliyopo Kimara Baruti, imeendelea kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF na mmoja wa wafanyakazi aliyezungumza na mwandishi wetu, amdsema madai kuwa hospitali binafsi zimestisha huduma kwa wanachama wa NHIF ni uchonganishe na zipuuzwe.

*** Wanachama NHIF wasema huo ni uzushi

Wanachama wa NHIF waliokutwa wakipatiwa huduma za afya katika Hospitali ya Massana na Karuki, wamesema wanaendelea kupata huduma za afya vizuri na hawajakutana na changamoto yoyote.

Akizungumza akiwa katika Hospitali ya Kairuki, Mwalimu Thecle Kasege, amesema ni nzuri.

Naye Mwanachama Viktoria Msokwa, aliwataka wanachama wa NHIF wasisikilize taarifa za mitandaoni na badala yake wafike vituoni au kuwasiliana na NHIF.

Mwanachama mwingine akizungumza akiwa Hospitali ya Masana, Shaban Rashid Abdallah, amesema; “Mfuko huu ni mkombozi kwa wananchi hivyo kila mwanachama ahakikishe anawajibika kuutunza na kuwasilisha michango kwa wakati.