March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hospitali ya Magunga yatengewa bil.1.5 ukarabati wa majengo yake

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga kwa tiketi ya CCM CPA Charles Njama amesema Hospitali ya Wilaya ya Korogwe,Magunga inakwenda kufanyiwa ukarabati mkubwa kwa gharama ya sh. bilioni 1.5.

Pamoja na Hospitali ya Magunga, kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kunakwenda kujengwa vituo vya afya sita na zahanati saba kwenye Jimbo la Korogwe Mjini ili kusogeza karibu huduma za afya kwa wananchi.

Ameyasema hayo Oktoba 26, 2025 kwenye mkutano wa kufunga kampeni Jimbo la Korogwe Mjini uliofanyika Mtaa wa Mbeza, Kata ya Manundu, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Mjini Thobias Nungu.

“Kwa upande wa afya tunatambua kuna baadhi ya maeneo yana changamoto yakutokuwa na zahanati, na maeneo mengine tunahitaji vituo vya afya vyenye Huduma ya Mama na Mtoto. Ukienda Kata ya Old Korogwe maeneo ya Mtaa wa Lwengera- Darajani, hawana zahanati, lakini pia ukienda Mtaa wa Kwameta (Kata ya Kwamdolwa) kuna changamoto kama hiyo. Lakini habari njema, tunakwenda kujenga zahanati saba katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Lakini tunakwenda pia kujenga vituo vya afya sita, hivi vyote ni katika kuhakikisha tunasogeza karibu huduma kwa wananchi katika kata zetu. Lakini katika hiyo hiyo huduma ya afya, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya Hospitali ya Magunga. Awali ilikuwa imetengwa sh. milioni 900, lakini sasa ni sh. bilioni 1.5 ili huduma kwenye hospitali yetu ziwe bora kwa kukidhi haja, na kuendana na hadhi yetu Jimbo la Korogwe Mjini” alisema Njama

Njama amesema katika kuzunguka kwake wakati wa kampeni, amebaini upungufu wa vyumba vya madarasa kwenye shule za msingi, hivyo wanakwenda kujenga vyumba 62 vya madarasa kwenye shule za jimbo hilo kutakakokwenda sambamba na ukarabati wa baadhi vyumba vya madarasa kwenye baadhi ya shule.

“Nimepita kwenye ziara zangu, tumetambua maeneo ambayo yana uhaba wa vyumba vya madarasa, maeneo ambayo yanahitaji shule, na maeneo ambayo yanahitaji sekondari. Na ukienda Kata ya Magunga kuna changamoto kidogo, Kata ya Mtonga kuna eneo wanauhitaji wa shule ya msingi, ukienda Kata ya Kwamndolwa maeneo ya Goo wanahitaji kituo shikizi, wakati Mtaa wa Kwameta wanahitaji shule ya msingi, ukienda Kata ya Kilole kuna changamoto maeneo ya Lujewa, hizi zote majibu yake ni Dkt. Samia Suluhu Hassan” amesema Njama.

Njama amesema kwenye masuala ya kilimo, Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwenye jimbo hilo, ambapo Bonde la Kwamsisi wameletewa sh. bilioni 24.5, na Mkandarasi ameshakabidhiwa eneo la ujenzi, na anaanza kazi. Bonde la Mahenge bajeti yake imeongezwa kutoka sh. bilioni mbili hadi sh. bilioni nne (4), nia ni kuboresha mradi huo wa umwagiliaji na wakulima wengi waweze kufaidika, wakati Bonde la Kwamngumi ambalo linafanyiwa Upembuzi Yakinifu kwa sh. bilioni moja ili kuona ni namna gani litawasaidia wakulima.

“Kwa kazi kubwa hizo zilizofanyika na zitakazofanyika, utaachaje kumpigia kura Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aweze kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo ikiwemo sisi wa Jimbo la Korogwe Mjini” amesema CPA Njama.