Na Jackline Martin
Hospitali ya Aga Khan imeweka jiwe la msingi la Kituo chake cha kisasa cha Matibabu ya Saratani, ambacho kitatumika kama kitovu muhimu cha Mradi Mtambuka na wa kivumbuzi wa Saratani Tanzania (TCCP).
Mradi huu, ambao ulizinduliwa na Huduma za Afya Aga Khan (AKHS) mnamo Januari 20202 wenye thamani ya shilingi Bilioni 13.8 za kitanzania una melengo ya mbeleni ya kupunguza maradhi na vifo vya saratani katika mikoa lengwa ambayo ni Dar es Salaam na Mwanza.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa kituo Cha kisasa Cha matibabu ya Saratani, waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema jenzi wa kituo hicho umefanyika katika kipindi sahihi nchini ambapo Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya na maendeleo ya Jamii kwa watanzania wote;
“Saratani ni ugonjwa unaoathiri watu wenye umri na jinsia zote, watoto, watu wazima, wanaume kwa wanawake. Sisi sote tunawajua watu ambao maisha yao yamekatishwa na saratani. Ugonjwa huu unasababisha pia hasara kubwa kwa Taifa kwa sababu unapunguza nguvu kazi na unazorotesha maendeleo ya mtu mmoja mmoja na ya Taifa.”
“Ujenzi wa kituo hiki umefanyika katika kipindi sahihi katika nchi yetu,” aliongezea.“Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya na maendeleo ya jamii kwa Watanzania wote, ikiwemo huduma za saratani”
Waziri Ummy alisema Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa saratani 42,060 kila mwaka ikiwa sawa na wagonjwa 76 katika kila watu 100,000 huku vifo vikiwa ni 29,000 kila mwaka sawa na asilimia 68.
Aidha Waziri Ummy alisema wagonjwa wengi wa saratani wanagundulika ugonjwa ukiwa umefika katika hatua ya tatu au ya nne ambayo ni ngumu kutibika huku akitaja sababu ya kuchelewa kugundua saratani ni pamoja na kuwa na vituo vichache vinavyotoa huduma hiyo nchini.
“Kutokana na changamoto ya vituo vichache vya kupima na kutoa matibabu ya saratani nchini, Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeingia ubia na Agha Khan kutekeleza mradi huu ambao utatusaidia kuwafikia watanzania wengi kupata huduma za kupima pamoja na kupata matibabu ya saratani”. Amesema Waziri Ummy.
Mbali na hayo Waziri Ummy aliongeza kuwa kituo hicho kinatarajia kuhudumia wagonjwa wa saratani takribani 120 kwa siku na hivyo kuweza kuipungua mzigo taasisi ya saratani ya Ocean Road ambayo inahudumia wagonjwa 800 mpaka 900 kwa siku.
Pia Waziri Ummy amewataka watanzania kujitokeza mapema na kuwa na utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara ikiwemo saratani.
Waziri Ummy ametaja saratani ambazo zinaongoza nchini ni pamoja na saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake, saratani ya matiti pamoja na saratani ya tezi dume huku maeneo ambayo yanaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi ni mikoa ya kanda ya mashariki (61%), kanda ya kaskazini (17.3%) na kanda ya ziwa (9.1%).
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi