Na Esther Macha, Timesmajira, Online,Mbeya
OFISA Elimu Mkoa wa Mbeya ameagizwa kumchukulia hatua za kinidhamu Mwalimu wa shule ya sekondari Loleza ,Sabina Haule kwa kosa la kuwalaza darasani wanafunzi wa kidato cha sita kwa kile anachidai ni watukutu.
Agizo hilo limetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ,Juma Homera wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika shule hiyo ya wasichana Loleza iliyopo eneo la Sokomatola mkoani hapa.
Homera amesema kuwa mwalimu huyo kwa makusudi alifunga bweni na kisha kuondoka na ufunguo pasipo kujali hali ya kiafya ya watoto hao hasa ukizingatia Mkoa wa Mbeya kuwa na baridi kali.
“Ulifunga bweni la wanafunzi hao na kisha kuamuru kulala darasani ikiwa ni sehemu ya adhabu kwa wanafunzi hao wa kidato cha sita na kuwalaza darasani ila wewe ukaenda kulala zako nyumbani,”amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha Homera amewapongeza Walimu kwa kazi nzuri wanayoifanya lakini licha ya kazi hiyo ni vyema wakawajali na kuwapenda wanafunzi.
Kwa Upande wake Mkuu wa Shule ya Loleza amesema taarifa aliipata na tayari alikuwa ameshaanza kulifanyia utekelezaji wa namna ya kulitatua.
Mwalimu Sabina Haule alipoulizwa kuhusu madai hayo ya kuwalaza wanafunzi darasani alikana madai hayo.
“Hapana Mkuu mimi sikuwambia walale darasani niliwambia wakalale kwenye mabweni mengine mkuu wale wanafunzi ni watukutu sana mara nyingi wanajifichaga uvunguni na wana vurugu sana lakini naomba unisamehe kama hilo ni kosa,”amesema Mwalimu Sabina.
Wanafunzi waliolazwa darasani ni wa kidato cha sita mchepuo wa HGL ikumbukwe shule ya sekondari Loleza ni moja kati ya shule za wasichana zinazopatikana jijini Mbeya.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM