Na Esther Macha, Timesmajira Online,Mbeya.
MKUU wa Mkoa wa Mbeya ,Juma Homera amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya bil. 3 kwa ajili ya ununuzi wa mashine ya kisasa ya uchunguzi wa magonjwa (MRI)ambayo italeta mabadiliko makubwa katika huduma za afya na kuimarisha uwezo wa hospitali .
Amesema pia mashine hiyo ya kiuchunguzi itawafanya wataalamu kutoa huduma bora kwa jamii na kupunguza gharama za kusafiri kwenda jijini Dar-es-Salaam kuifuata huduma.
Homera amesema hayo mara baada ya kumaliza ziara yake katika hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ambapo ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa wa mashine hiyo ambayo imekua hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya na upatikanaji bora wa vipimo vya kisasa kwa wananchi.
“Tunamshukuru sana Rais kwa kutoa zaidi ya bilioni 3 kwa ajili ya kufanya uwekezaji huu katika Mkoa wa Mbeya ambapo kufanya kazi kwa mashine ya MRI italeta mabadiliko makubwa katika huduma za afya na kuimarisha uwezo wa hospitali yetu na wataalamu wetu kutoa huduma bora kwa jamii na kupunguza gharama za kusafiri kwenda Dar-es-Salaam kuifuata huduma hii,” amesema Homera.
Hata hivyo Homera ameishukuru Wizara ya Afya chini ya Ummy Mwalimu pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwa jitihada kubwa zilizofanyika hadi kufanikisha shughuli za usimikaji wa mashine hiyo ambayo itakuwa na uwezo wa kuhudumia takribani wakazi wa mikoa 7 ya Nyanda za Juu Kusini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Dkt. Godlove Mbwanji amesema uwepo wa mashine hiyo utawezesha shughuli za huduma hospitalini hapo kufanyika kwa ubora zaidi kwa kuwa hapo awali wataalamu walikuwa wakilazimika kutoa rufaa kwa wagonjwa kwenda Dar-es-Salaam kufuata kipimo cha MRI.
“Tunaweza kupima wagonjwa ambao wana matatizo ya saratani au uvimbe wa aina tofauti tofauti kwenye mwili, pia tunaweza kupima mabadiliko yanayoendana na umri,”.
Akizungumza mara baada ya kupata huduma za uchunguzi kupitia mashine ya MRI, Reinfrida Kayombo mkazi wa jijini Mbeya, ameishukuru serikali kwa kuwaletea huduma hiyo karibu na kuwasaidia wakazi wa Nyanda za Juu Kusini ambao hapo awali walilazimika kutumia gharama kubwa kuifuata huduma hiyo mbali.
“Tunamshukuru sana mama Samia kwa kutuletea huduma hii maana hapo awali tulikuwa tunapata gharama kubwa kusafiri lakini kwa sasa tumeletewa huduma hapahapa,” amesema Kayombo.
Mashine ya MRI ni teknolojia ya hali ya juu ambayo inatumika kuchunguza na kutoa picha za mwili wa binadamu kwa kutumia mawimbi ya umeme na magneto na inatoa maelezo ya kina pia inaweza kuchunguza hali mbalimbali za kiafya, kama vile matatizo ya ubongo, saratani, magonjwa ya moyo, na matatizo ya mfumo wa musculoskeletali.
Uwepo wa mashine hiyo utasaidia wakazi Mikoa saba ya Nyanda za Kusini ikiwemo Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Ruvuma, Njombe na Iringa pamoja na nchi za jirani kupata huduma za kibingwa za uchunguzi na tiba kwa haraka Jirani na maeneo waliyopo.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa