September 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hivi ndivyo MSD Kanda ya Iringa inavyohudumia vituo 826 kwa asilimia 92

Na Reuben Kagaruki, Timesmajiraonline,Iringa

MTU yeyote anapopata changamoto ya kiafya akatoka nyumbani kwenda kutibiwa, kikubwa anachowaza ni kumkuta daktari, ambapo atapimwa na kupatiwa dawa.

Hakuna anayewaza hizo dawa zimeweza kufikaje kwenye kituo cha afya alichoenda kutibiwa. Hakuna anayewaza kwamba kuna watu wanatembelea usiku na msiku, wakipita kwenye maeneo magumu kuwafikishia dawa hizo.

Jambo la kujivuni ambalo linafanywa na Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) hakuna Mtanzania anayekosa dawa kutokana na changamoto za kijiografia.

Hiyo ni kwa sababu Serikali ya Rais Samia SUluhu Hassan inathamini maisha ya Watanzania ndiyo maana kupitia MSD imeboresha mfumo wa usambaza bidhaa za afya katika hospitali, vituo vya afya, zahanati pamoja hospitali za binafsi zilizoidhinishwa na Wizara ya Afya.

Kanda ya Iringa ni miongoni mwa kanda 10 za MSD ambazo zimekabidhiwa dhamana nzito na Serikali ya kuhakikisha bidhaa za afya zinafikia vituo vyote vya kutolea huduma za afya.

Mwanzoni mwa mwezi huu, wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari walitembelea Kanda ya Iringa ambayo inahudumia vituo 826 na halmashauri 17.

Pamoja na mambo mengine wahariri waliweza kujua jinsi Serikali kupitia MSD ilivyosogea huduma zake kwa wananchi, hatua ambayo imehitimisha kilio cha Watanzania kwenda hospitali na kuambiwa dawa fulani haipo.

Kanda ya Iringa ni miongoni mwa kanda za mwanzo kabisa ambazo MSD ilianza nazo ilipoanza kusogeza huduma kwa wananchi. Uamuzi huo ulifikiwa, ili kurahisisha usafirishaji bidhaa za afya, kwani haikuwa rahisi kuzitoa Dar es Salaam kwenda kuwatafuta wananchi walipo, mfano mkoani Ruvuma kwa ajili ya kuwapelekea bidhaa za afya.

Kwa kuliona hilo, MSD iliamua kusogeza karibu na wananchi walipo na hiyo, ndiyo ilikuwa moja ya sababu ya Kanda ya Iringa kuwa miongoni mwa zile za mwanzo.

Akizungumza na wahariri hao, Meneja wa MSD Iringa, Robert Lugembe, anasema kabla ya mwaka 1995, Kanda ya MSD Iriga ilikuwa inahudumia wa Iringa yenyewe, wakati huo hakukuwa na Mkoa wa Njombe.

Aidha, Kanda hiyo ilikuwa inatoa huduma Ruvuma, Mbeya na Rukwa. Kwa mujibu wa Lugembe, Kanda ya Iringa inahudumia halmashauri 17, ambapo katika Mikoa ya Iringa zipo tano na Mkoa wa Njombe nako zipo 5.

Mkoa wa Njombe una halmashauri sita, lakini kwa mujibu wa Lugembe halmashauri moja inahudumiwa na Kanda ya Mbeya.

Aidha, anasema wanahudumia halmashauri saba za Mkoa wa Ruvuma, huku wakiachia halmashauri moja ya Tunduru ambayo inahudumiwa na Kanda ya Mtwara, hivyo kufanya halmashauri zinazohudumiwa na kanda ya Iringa kuwa 17.

Anaongeza kwamba halmashauri hizo zimegawanyika makundi mawili, ambapo kuna kundi A na kundi B. “Kwa hiyo mwezi huu wa saba tunahudumia kundi A, halafu Agosti tunahudumia kundi B, kwa maana Juni tulihudumia kundi B, ndiyo maana Julai tunahudumia kundi A,” anafafanua Lugembe.

Kwa utaratibu huo, Lugembe anasema kila kundi linapata dawa kila baada ya mwezi mmoja.

Anasema kama ilivyo kwa MSD nchi nzima, na wao kila halmashauri wanafika mara sita kwa mwaka kwa ajili ya kupeleka dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma vya umma na vile vya binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya.

“Kila halmashauri tunafika mara sita kwa maana tunaruka mwezi mmoja na unaofuata tunakwenda na usambaza dawa unafanyika kwa mujibu wa kalenda kuanzia tarehe moja hadi mwisho wa mwezi,” anaeleza Lugembe.

Anasema wanapokea mahitaji ya wateja kuanzia tarehe moja hadi 10 na kuanzia tarehe 11 ni kuchakata maombi na kupeleka bidhaa za afya kwa wateja.

Kwa mujibu wa Lugembe kuanzia miaka miwili iliyopita, huduma za MSD zimeirika sana ambapo vifaa tiba na dawa wanazopeleka kwa wateja zinafika asilimia 92.

“Hiki ni kiwango cha juu sana cha utendaji katika kuhakikisha bidhaa za afya zinafika kwa wateja,” anasema Lugembe na kusisitiza kwamba kwa sasa wanafikisha bidhaa za afya kwa wateja ndani ya muda.

Anaongeza kwamba kuna wateja wanaokamilisha maombi yao ya bidhaa za afya tarehe 10 kwa mwezi na kuanza kupokea bidhaa za afya tarehe 12, na hiyo inaonesha jinsi upeleka bidhaa za afya ulivyorahisishwa na unaavyofanyika kwa haraka.

Kuhusu wafanyakazi, anasema Kanda ya Iringa ina wafanyakazi 36 ambao wanahudumia vituo 826. Anatoa mfano, akisema kama kama unatokea jijini Dar es Salaam wanaanza kuhudumia Halmashauri ya Kilolo, ukitokea Dodoma kama unakwenda Iringa, wanaanzia Halmashauri ya Iringa DC ambapo wanakwenda hadi Ruvuma ambapo wanakutana na mpaka wa Msumbiji.

Kwa upande wa Magharibi, anasema wanakutana na Ziwa Nyasa, Mkoa wa Njombe Halmashauri ya Ludewa na kwenye halmashauri ya Nyasa. Kwa mujibu wa Lugembe, Kanda ya Iringa ni kati ya Halmashauri ambazo kituo cha mwisho wanakwenda mbali sana kupeleka bidhaa za afya kilometa 750 kutoka Iringa kwenda Wilaya ya Nyasa ambapo kuna kituo cha afya kinachoitwa Mnyele na Wilaya ya Namtumbo ambapo kituo cha mwisho ukitokea Songea Mjini kipo umbali wa kilometa 300.

Kuhusu maeneo magumu kufikika, Lugembe anasema katika Halmashauri ya Ludewa wanaenda hadi ziwani ambapo inawalazimisha wakodi boti kwa ajili ya kufikisha mzigo kwa saabu vituo vya afya vipo pembezoni mwa ziwa na hakuna barabara.

Anataja eneo lingine gumu kufikika kuwa ni katika Wilaya ya Kilolo ambapo kuna milima na barabara mbaya.

“Lakini kuna vituo vichache vilivyopo Mufindi ambako hauwezi kufikisha bidhaa za afya hadi watumie treni ya Tazara.

“Kwa hiyo tunawafikishia mzigo stesheni na tunakabidhiana wafanyakazi wetu wengine ambao wanaanza safari ya kupanda juu ya mawe kupeleka mzigo hadi mlangoni kwa mteja,” anaeleza Lugembe wakati akifafanua changamoto wanazokumbana nazo wakati wa usambazaji bidhaa za afya.