Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Leo, Benki ya NMB imeingia makubaliano na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kushirikiana katika uundaji na uboreshaji wa mifumo ya Tehama yenye lengo la kuimarisha uchumi wa kidijitali wa Nchi yetu.
Kupitia makubaliano haya, miongoni mwa mambo ambayo NMB watashirikiana na Wizara ni pamoja na:
➡️ Uundwaji wa “Jamii Namba” – Hii ni namba maalum kwa Mtanzania itakayojumuisha huduma mbalimbali, yaani badala ya kuwa na namba tofauti tofauti, (Leseni, Passport, Nida) tunaweza kuwa na namba moja itakayo tambulika katika nyanja hizi zote.
➡️ Jamii Data Exchange Platform – Huu ni mfumo ambao utaundwa kuunganisha mifumo yote ya kiserikali hasa ile ya malipo ili iweze kuwa na mahusiano na uwezo wa kupata taarifa kutoka sehemu moja au nyingine kiurahisi zaidi.
➡️ Uundwaji wa mifumo imara zaidi ya malipo mtandaoni ambayo inawezesha huduma salama na rahisi za miamala ya kidijitali kwa wananchi kila wanapo pata huduma sehemu tofauti za serikali.
➡️ Kutumia wataalam wa Benki ya NMB katika kuunda na kuboresha mifumo, kwani tunajivunia kuwa na vijana wazalendo wenye utaalamu mkubwa juu ya maswala ya Tehama.
➡️ Benki ya NMB itatoa jukwaa la kufanyia majaribio (pilot platforms) ya mifumo itakayoundwa, ili kuhakikisha ubora na ufanisi kabla ya kuanza kutumika.
Makubaliano haya yamesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari – Mohammed Khamis Abdulla na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB – Bi. Ruth Zaipuna, wakishuhudiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari – Mhe. Nape Moses Nnauye.
Akizungumza baada ya kushuhudia tukio hilo, Waziri Nape alisema “Ushirikiano huu utachochea na kuleta mabadiliko chanya kwenye ukuaji wa uchumi wa kidijitali katika Nchi yetu. Kwa nyakati tofauti Serikali kupitia Wizara imekuwa ikishirikiana na sekta binafsi, ikiwemo Benki ya NMB kama mlivyosikia historia hapa. Hivyo kilichoshuhudiwa hapa leo ni muendelezo wa mashirikiano katika kuhakikisha kama nchi tunapiga hatua kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia.”
“Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 79 ya pesa ziko mkononi. Sasa dunia imeshahama katika matumizi ya pesa taslimu, iko katika ‘cashless’. Tanzania hatuwezi kubaki kama kisiwa, ndio maana makubaliano haya na Benki ya NMB tunayapa uzito na thamani kubwa.”
“Makubaliano haya ya leo yanaonesha na kuthibitisha kwamba tuko tayari kukimbizana na mabadiliko ya teknolojia katika dunia tunayoiendea na Benki ya NMB iko tayari kutushika mkono kuyaendea maono haya, ndio maana tunaishukuru sana,” alieleza.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Benki ya NMB- Bi. Ruth Zaipuna alisema: “Katika makubaliano haya, miongoni mwa mambo tutakayofanya sisi NMB ni pamoja na kutumia wataalam wetu wa ndani kuunda na kuboresha mifumo ya nchi ya Tehama na kutoa jukwaa la kufanyia majaribio ya mifumo hiyo. Tunafanya haya tukiamini kuwa kuimarika kwa Uchumi wa Kidijitali ni jambo la faida sio tu kwa NMB, bali kwa Sekta ya Fedha na Taifa kwa ujumla.”
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa