November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hiki ndicho usichokifahamu kuhusu matumizi ya umeme wako

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Dar es Salaam

NCHI yoyote duniani yenye dhamiria kukuza uchumi wake huanza kwa kuweka mazingira bora yanayoshirikisha sekta mbalimbali na wataalamu kwa kuweka msukumo mkubwa katika kutekeleza shughuli na miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.

Msingi mkubwa wa uchumi ni kuwa na nishati ya uhakika ili kuhudumia kila sekta ya uchumi. Bila shaka ni wazi kuwa nishati ya umeme ndio uti wa mgongo katika safari ya kukua kiuchumi na ustawi wa jamii.

Mhandisi Athanasius Nangali, Meneja Mwandamizi Usambazaji na Huduma kwa Wateja.

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ndio lenye dhamana ya kuzalisha na kusambaza umeme nchini, shirika hilo linahakikisha muda wote miundombinu iko salama na vyanzo ni vya uhakika wakati wote. Ni wazi bila kujipanga na kusimamia kwa makini yote hayo hayatoweza.

Ili kutimiza malengo yake,TANESCO imejipanga na kujigawa katika maeneo makuu manne ambayo ni Kufua, Kusafirisha, Kusambaza Umeme na Uwekezaji katika miundombinu na vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme.
Mpaka kumfikia mlaji au mtumiaji wa umeme,nishati hiyo ikishafuliwa inabidi isafirishwe mpaka kufika eneo husika kwa ajili ya kusambazwa kwa wateja katika maeneo mbalimbali kulingana na mahitaji.

Baadhi ya watoa huduma katika kituo cha miito ya simu(Call Center) wakiwa kazini

Usambazaji inamaana kumfikishia mlaji nyumbani kwake kutoka katika kituo cha umeme ulipofikia.Hii ni tofauti na kusafirisha ambapo umeme ukishafuliwa katika chanzo cha uzalishaji,unasafirishwa hadi katika vituo vya kusambazia.

Kisha ndio husambazwa mpaka majumbani kwa ajili ya matumizi. Kuanzia kusafirisha mpaka kusambazwa umeme hutumia nyaya zenye ukubwa tofauti kulingana na kiasi cha umeme unaosafirishwa au kusambazwa.

Ili kutoa huduma ubora na kurahisisha utendaji wake TANESCO ina idara maalumu ya Kurugenzi ya Usambazaji na Huduma kwa Wateja ambayo imejipanga katika Kanda.

Kwa Tanzania Bara TANESCO imejipanga katika mifumo yake kwa kuunda Kanda 7, Mikoa 29 (tofauti na ya Serikali ambayo ni 26) na wilaya 132. Ili kuwasogelea karibu zaidi wateja, TANESCO imefungua ofisi ndogo 133 mpaka ngazi ya wilaya.

Meneja wa TANESCO Wilaya ya Tegeta jijini Dar es Salaam Mhandisi Josephat Joseph akitoa elimu kuhusu mita za umeme.

Mhandisi Athanasius Nangali, ambaye ni Meneja Mwandamizi Usambazaji na Huduma kwa Wateja,anasema shughuli kuu za kurugenzi hiyo ni kusambaza umeme hadi kwa wateja(walaji) kwa kujenga miundombinu (service lines), kutoa huduma za kila siku ikiwa ni pamoja na kupokea na kushughulikia malalamiko ya huduma zinazohusiana na umeme (customer complain), ili kutimiza hilo kwa wakati, kuna kitengo maalumu cha dharura ambacho kipo saa 24 kuhudumia wateja.

Sambamba na hilo, TANESCO inawajibika kuelimisha wateja,kwa ajili ya matumizi sahihi ya umeme hivyo kuepusha ajali na majanga mengine yanayoweza kusababishwa na umeme au matumizi mabaya ya umeme.

Mwisho ni kukarabati na kuimarisha miundombimu ya usambazaji umeme. Miundombinu hiyo ni ile inayoanzia kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti(kv) 33 kurudi chini hadi kwenda kwa mlaji.

USAMBAZAJI UMEME

Mpaka kufikia Januari, 2021 umeme umefika katika mikoa yote 26 ya kiserikali kwa Tanzania Bara ambayo ni mikoa 29 ya ki-TANESCO (ambapo katika jiji la Dar es Salaam,TANESCO imejigawa katika mikoa 4) ili kurahisisha utendaji na kuwafikia wateja wake kwa urahisi zaidi.

Kwa Mkoa wa Dar es Salaam,kuna Mikoa ya Temeke,Ilala,Kinondoni Kaskazini na Kinondoni Kusini.Mgawanyiko huo ni muhimu kutokana na ukubwa wa mtandao wa umeme pamoja na idadi kubwa ya wateja na mahitaji yao.

Mpaka kufika Januari 2021,TANESCO ilikuwa na idadi ya wateja 3,065,414 ambao wamegawanyika kulingana na matumizi ya umeme.Katika mgawanyiko huo, D1 ambao ni wateja wadogo wenye matumizi chini ya unit kWh 75 kwa mwezi wako 871,427 (hawa huchangia mapato kwa asilimia 28.4 kutokana na mauzo yote ya umeme TANESCO).

Wengine ni T1 ambao hutumia umeme zaidi ya uniti kWh 75 lakini hawazidi uniti 7,500 kWh kwa mwezi,idadi yao ni 2,189,983 (huchangia mapato kwa asilimia 72 ya mauzo ya umeme kwa TANESCO ambao ndio wengi zaidi ikilinganishwa na makundi mengine.

Wateja wa T2 ni viwanda vya kati wenye matumizi ya uniti 7,500 na zaidi ambao umeme wao unapimwa kwenye msongo mdogo wa volti,hawa wako 3,168 (na huchangia mapato kwa asilimia 0.001 ya mauzo ya umeme)

Pia kuna T3 ambao ni wateja wakubwa wenye matumizi zaidi ya unit 7,500 ambapo umeme wao unapimwa kwenye msongo mkubwa wa volti ambao jumla wako 836(asilimia 0.0003)

Kigezo kingine kilichotumika kuwagawa wateja ni kwa kutumia tarif ambayo inatokana na jinsi unavyotumia umeme.Unaweza kusema matumizi yako ya umeme ndio yanaamua uingie katika kundi lipi (au tarrif ipi) kati ya yaliyotajwa hapo juu.

Shirika la Umeme Tanzania limeweka utaratibu maalumu wa kuwafikishia umeme wateja wenye shughuli kubwa (yani Tarif 3-T3) za kibiashara na viwanda vikubwa hivyo hufikishiwa umeme moja kwa moja kwa msongo wa kilovoti 33 na kilovoti 11.

Na kwa wateja wenye viwanda vidogo na baadhi ya shughuli za kibiashara, taasisi za umma na makazi wanasambaziwa umeme kupitia kilovoti 0.40/0.23 ambao wanaingia katika T2(tarrif 2)

Mhandisi Athanasius Nangali anasema “mpaka kufikia mwisho wa mwezi Januari 2021,mtandao mzima wa usambazaji umeme nchini una jumla ya transfoma 25,866 (ambazo ziko mitaani zinazosambaza umeme)”.

Mtandao mzima wa kusambaza umeme una urefu wa kilomita 146,135.11. Ambapo msongo mkubwa wa kilovoti 33 una urefu wa kilomita 46,770.75. Msongo wa kilovoti 11 una urefu wa kilomita 12,432.82 na msongo unaoongoza kwa urefu ni wa kilovoti 0.4 ambao una kilomita 86,931.54, huu ndio unafika mpaka majumbani.

Mhandisi Nangali “unapokuwa na mtandao mrefu kiasi hicho pia kuna kuwa na changamoto nyingi za kuusimamia na kuhakikisha kuwa wateja wote waliounganishwa wanapata huduma sahihi kwa wakati”.

Hata hivyo kurugenzi ya usambazaji na huduma kwa wateja ndio inasimamia mauzo ya umeme TANESCO.Kutokana na mtandao na mgawanyiko huo mkubwa wa wateja, Shirika linauzia wateja wake umeme kwa mgawanyiko maalumu kwa kutumia unit.

MAUZO YA UMEME

Wateja wanaonunua umeme kuanzia unit 1 hadi 75 kwa mwezi hungizwa katika kundi la wateja wadogo wanaotumia umeme kidogo. Kundi hili ni D1 (domestic low consumption) ambapo huuziwa umeme shilingi 100 kwa uniti moja.

Wateja wa T1 hutumia zaidi ya uniti 75 kwa mwezi hulipa shilingi 292 kwa uniti moja. Kundi hili ndio lenye wateja wengi zaidi nchini kwani hawa ndio wanaotumia umeme nyumbani.

Kundi la T2(tarif 2) wanalipa mara mbili, yani kwa unit pamoja na kVA wanazotumia. Ambapo hulipa shilingi 195 kwa unit moja pamoja na shilingi 15,004 kwa kVA.

Hilo ni pamoja na wateja wakubwa zaidi ambao ni wa T3 wanaochukua umeme katika transmission kama Zanzibar, ambao wanalipa kwa shilingi 157 kwa unit( megavolti kwa kWh), Megavolti kVa shilingi 13,200 pamoja na High Voltage (kWh shilingi 152 kwa unit na HV (kVa) shilingi 16,550 kwa unit.

HUDUMA YA MANUNUZI YA UMEME

Mfumo unaotumika kwa sasa ni mita za LUKU(Lipa Umeme Kwa jinsi Unavyotumia).Ambapo mita sasa zimesambaa nchi nzima baada ya kubadilisha mita za zamani ambazo zilikuwa na changamoto nyingi ambapo ililazimu msoma mita wa TANESCO (Meter Reader) asome mita kisha iingizwe katika mchakato wa kompyuta ndio bili itolewe ili kusambazwa kwa mteja ili wakalipe.

Pamoja na mfumo wa kisasa wa LUKU, mteja anaweza kununua umeme kwa simu yake ya mkononi, pia kuna vituo vingi vya kuuza umeme katika maeneo mbalimbali.

Ili kupunguza gharama za ukusanyaji mapato na kuongeza ufanisi katika kuhudumia wateja, Shirika limejiunga na Mtandao wa Kielektroniki wa Serikali wa kupokea mapato (GePG – Government Electronic Gateway System) tangu Aprili, 2017. Shirika limefanikiwa kufikisha huduma ya kununua umeme nchi nzima.

Huduma zimerahisishwa na zinapatikana saa 24 mahali popote nchini. Hii inatokana na kuwezesha wateja kununua umeme kwa njia ya mitandao ya simu (Tpesa, Mpesa, Tigopesa, Airtel money na Ezypesa – Zantel), mifumo ya benki mbalimbali, vifaa vya malipo kupitia Point of Sales (POS) na Mawakala wa mauzo waliosambaa nchi nzima.

Anasema Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano wa TANESCO, Johary Kachwamba “hatua hiyo na nyingine nyingi za huduma ya manunuzi ya umeme imerahisisha ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo ofisi za TANESCO zilikuwa zinafurika misururu ya watu kwa ajili ya kulipa bili zao ili wasikatiwe umeme”.

HUDUMA YA MALALAMIKO YA WATEJA (CUSTOMER COMPLAIN)

Shirika la Umeme nchini lina kitengo maalumu cha huduma kwa wateja ambapo kuna vituo vya miito ya dharura. Huduma hizo zinashughulikiwa kupitia Kituo cha Miito ya Simu (Call Center), ambapo kuna National Call Center pamoja na madawati ya dharura yaliyopo mikoani na sehemu nyingine katika wilaya ambao hupokea malalamiko yanayotokana na changamoto za umeme.

Huduma kwa wateja haiishii kupokea na kutoa majibu kwa wateja, pia inatumika kuongeza uwazi katika mazingira ya kazi. Madai yote hupokelewa katika kituo cha TANESCO Ubungo (Umeme Park) pamoja na vitengo vya dharura katika mikoa yote.

Taarifa zinapelekwa katika vituo husika kupitia mtandao wa kompyuta kwa ajili ya kuzifanyia kazi kwa mujibu wa mkataba wa huduma kwa wateja.

ELIMU KWA WATEJA

TANESCO inawajibika kuelimisha na kuhamasisha wateja jinsi ya kutumia umeme pamoja na masuala ya usalama wa umeme. Pamoja na faida nyingi, umeme unahitaji nidhamu kubwa katika matumizi, kwani pia umeme ni hatari.

Hivyo kuna kitengo maalumu ambacho kinapita maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuelimisha jamii na baadhi ya maofisi nchini, ikiwa ni pamoja na taratibu za kupata umeme endapo mtu anahitaji kupata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.

Mhandisi Nangali “mwaka 2020, Shirika limeelimisha baadhi ya shule za msingi, sekondari, majeshi na hata jamii kupitia baadhi ya redio mikoani, hatua ambayo iliwapa wananchi wengi fursa ya kuuliza maswali na kufafanuliwa yale ambayo yamekuwa ni matatizo katika matumizi yao ya umeme kila siku.”

Shirika linaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii kuhusu matumizi bora ya nishati na usalama kupitia redio, TV, mitandao ya kijamii, magazeti warsha na mihadhara.

CHANGAMOTO

Pamoja na jitihada kubwa ya kuhakikisha umeme unapatikana kwa uhakika, shirika limekuwa na changamoto mbalimbali zinazochangia kupunguza jitihada za kuwahudumia wateja wake.

Katika mtandao mkubwa wa kilomita 146,135.11 ni wazi changamoto haziwezi kuepukika. Baadhi ya changamoto hizo ni uchakavu wa miundombinu ya kusambaza umeme katika baadhi ya maeneo.

Ili kupambana na changamoto hiyo Shirika lina mpango mahususi ambao umeshaanza utekelezaji wake wa kushughulikia miundombinu (POREP).

Changamoto nyingine ni ile ya mazingira ambayo inaleta mgongano wa maslahi katika jamii. Miti na njia za kusambaza umeme zinaingiliana. Katika hali ya kawaida miti inahitajika ili kulinda mazingira lakini pia umeme unahitajika katika maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.

Shida ni kwamba miti ikigusa nyaya za umeme, umeme unakatika, lengo la TANESCO ni kuhakikisha umeme unapatika kwa uhakika muda wote. Ili kuhakikisha mgongano huo wa maslahi unapata tiba, TANESCO imekuja na mbinu mbadala, haswa katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu.

Katika jiji la Dar es Salaam, TANESCO imeanza mfumo wa kupitisha nyaya ardhini (underground cable), baadhi ya maeneo badala ya nyaya za umeme kupita juu sasa zimepitishwa chini ya ardhi.

Maeneo ambayo nyaya hazijapita chini, shirika limeanza kubadilisha na kutumia nyaya zenye magamba (covered conductor). Nyaya zinakuwa na magamba hivyo kupunguza adhari iwapo mtu aatagusa waya bahati mbaya.

Kutokana na kuendelea kukua kwa mtandao wa umeme, mfano ni REA wanapokamilisha kujenga njia za umeme vijijini. Kwasasa vijiji ambavyo vimeshapata umeme ni 10,109 kati ya vijiji 12,268 nchini nzima. Hivyo mtandao mzima wa REA unapokamilika hukabidhiwa TANESCO kwa ajili uendeshaji.

Hivyo kutokana na kusambaa kwa umeme kwa haraka, baadhi ya maeneo yamekuwa hayafikiki kirahisi, hivyo Shirika la Umeme Tanzania limelazimika kufungua ofisi ndogo katika maeneo hayo ili kuwa karibu na wateja.