December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hiki ndicho Kinachowaponza wanaume kupata zaidi magonjwa ya akili

Na Aveline Kitomary,TimesMajira online,Dar es Salaam.

MAGONJWA ya afya ya akili ni aina ya matatizo ambayo yanaathri hisia ,mawazo na kuleta mabadiliko ya tabia kwa mtu.

Magonjwa haya yanaweza kumpata mtu yoyote lakini kuna mambo yanayosababisha au kuleta uhatarishi wa kupata.

Mambo hayo ni kama uwezo binafsi wa kupokea na kuchanganua changamoto mbalimbali mtu anayopitia na endapo akishindwa matokeo yake mtu anaweza kuishia kupata tatizo.

Kitu kingine kinachoweza kusababisha magonjwa hayo ni mazingira ambayo mtu anaishi kama vile kutokupata amani baada ya kukumbana na unyanyasaji.

Jamii inayomzunguka muhusika kutokauwa karibu kumsikiliza inaweza kusababisha lakini pia tatizo hilo linarithiwa .

Na pia kuna magonjwa ya mwili kama malaria kupanda kichwani ,kupata ajali ,kupata tatizo la ubongo,Virusi vya VVU kuharibu ubongo na magonjwa mengine .

Lakini kuna magonjwa yanayoathiri mama mjamzito na mtoto kuzaliwa akiwa na tatizo mfano sonona kwa mama,pombe,dawa za kulevya ,sigara na mengine.

HALI YA UGONJWA ILIVYO

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Watoto Duniani (UNICEF), kila sekunde 40 mtu mmoja hufarikia dunia kutokana ugonjwa wa afya ya akili.

WHO pia wameainisha kuwa vijana asilimia 20 ulimwenguni kote wanashida ya afya ya akili na katika nchi za kipato cha kati na chini karibu asilimia 15 wamefikiria kujiua.

Hata hivyo kujiua ni chanzo cha vifo vya vijana wenye umri wa miaka 15-19 Duniani kote .

Hapa nchini takwimu zilizotolewa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) zinaonesha kuwa kunaongezeko la wagonjwa wa afya ya akili hadi kufikia asilimia 10.8.

Akitoa takwimu hizo mkuu wa idara ya magonjwa ya afya ya akili Dkt.Fileuka Ngakongwa anasema wagonjwa waliotibiwa kwa mwaka 2019/2020 Muhimbili -Upanga walikuwa 32,307 ukilinganisha na wagonjwa 21,183 walitobiwa 2018/19.

“Kwa upande wa Muhimbili Mloganzila 2019/2020 wagonjwa waliotibiwa walikuwa ni 980 wakati mwaka 2018/2019 waliotibiwa walikuwa 753 huku ongezeke likiwa ni asimilia 23 Mloganzila.

WANAUME KUONGOZA

Kwa mujibu wa Takwimu za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili za mwaka 2018/19 idadi ya wanaume wanaougua ugonjwa wa akili ni 18,535 huku idadi ya wanawake ikiwa ni 10,631.

Twamu hizo zinaonesha kuwa idadi ya wanaume wanaougua ugonjwa huo ni wengi kuliko wanawake huku mtaalamu akiaanisha sababu mbalimbali.

Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Chuo cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU), Cristian Bwaya akizungumza na Jarida la Majira ya Afya anasema ni kweli kuwa wanaume wanakubwa na tatizo hilo kutokana na mfumo wa maisha katika jamii.

“Wanaume wanaongoza kuwa na changamoto za afya ya akili ,hata wanaojaribu kujiua au kujiua ni wanaume ni kweli kuwa tatizo ni kubwa ingawa watu wengi wanaelewa kuwa mwanamke hawezi kustahimili changamoto ila kiuhalisia sio kweli.

“Kitu kidhaifu kwa mwanamke huwa inautatuzi mfano akikerwa atalia,akiwa na taarifa ya kusumbua moyo atasema wanawake wengi sio watu wa kuweka vitu akiwa na vitu atazungumza ataenda kwa watu kuwaambia.

“Akifiwa atalia na akiwa na wasiwasi na kitu atasema hii kwa watu wengi wanaona ni udhaifu kama mwanaume akilia au kulalamika ni kwa sababu mwanaume amelelewa kuficha hisia zake, wamelelewa kutoonesha hisia kuwa ni uimara,halalamiki ,halii hata anapoumwizwa,”anaeleza Msaikolojia Bwaya.

Anasema hali hiyo ndiyo inayoathiri afya ya akili kwa wanaume wengi wanaponzwa na tabia zao za kuvumilia vitu ambavyo ndani yao havivumiliki.

“Mwanaume akifiwa halii anaugua ndani hata anaweza kukerwa akanyamaza ,kuna kitu kinamsumbua moyo hamwambii mtu atazungumza mambo mengine lakini vitu vya ndani hasemi .

“Anaweza kupitia changamoto hivyo wengine ni wapweke ambao unatengeneza tatizo kutokana na mtu wa kutokushirikiana nao .

“Tabia ya kutokuongea,kuogopa kudhalilika na ndio inasababisha kupata shida ,wanaume wanaamini wanawake ni dhaifu kwa sababu hawawezi kunyamaza ,wanahisia lakini hii ndio inasaidi hawajui kuwa kujiona imara,hatishwi na kitu ni tatizo,”anadadavua.

Isack Lema ni Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Afya ya Akili Tanzania anasema sababu kubwa ya ni tabia ya wanaume kutokuzungumzia au kulia matatizo yanayowakuba.

Lema ambaye pia ni Msaikoloji Tiba katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) anasema sababu zingine ni mtoto wa kiume kusahaulika katika malezi na uwezeshaji ndani ya jamii.

“Zipo sababu nyingi na hapa tunaagalia magonjwa yanayopatikana kwa kiwango kikubwa katika jamii ni pamoja na magonjwa ya sonona,magonjwa ya hisia (bypola), aina ya magonjwa ya akili ‘skizofeni’ na magonjwa ya matumizi ya vilevi .

“Sasa tukiangalia haya magonjwa makubwa mfano sonona mara nyingi pia sasa wanaume wanaonekana kuwa na dalili au viashiria vya ugonjwa huu na sababu kubwa ni wanaume hawaongei mambo yao hata wanapokubwa na matatizo hukaa kimya au mara nyingi unakuta wanaendana katika njia ambazo sio za kiafya na hizo njia ni matumizi ya vilevi .

“Ukiangalia kundi kubwa la wanaume wamejiingiza kwenye matumizi ya vilevi kama pombe,bangi na dawa za kulevya na kutokana na kujiingiza kwingi vilevi vinaathiri ule mfumo wa akili uliopo kwenye mwili wa binadamu na kupelekea mchocheo na mwamko wa magonjwa ya akili,”anabainisha.

Anasema matumizi ya vilevi yanachangia wanaume kukumbana na magonjwa ya akili.

“Lakini pia kuna magonjwa ambayo dalili yake mmoja wapo ni mtu kusitisha uhai wake ukiangalia vitu wanavyotumia wanaume kusitisha uhai wao unakuta mara nyingi huwa ni vigumu kwa upande wa wanawake ,Kwa hiyo anaweza kutumia mbinu ambazo zinaweza kukamilisha tatizo,”anaeleza Lema.

Kumsahau kijana wa kiume ni moja wapo ya sababu ambazo zinachangia wanaume kukumbana na magonjwa ya akili kwa kiwango kikubwa kuliko wanawake.

Lema anasema ni muhimu sasa jamii kushtuka katika hili ili kuokoa afya na maisha ya vijana wa kiume.

“Malezi ya mabinti yamebadilika kwa kipindi kirefu kumekuwa na kitu cha kumjengea uwezo binti na wanawake lakini ni nani anayewajengea uwezo vijana wa kiume ni nani anawajengea uwezo wa kuweza kuendelea kuyaona ni yapi yanafaa?anauliza.

Anaongeza “Mfumo uliobaki ni wakuonesha wanaume ni jasiri, ni mtu ambaye anatakiwa kuwa mkakamavu anaweza kuhimili yote lakini na yeye ni binadamu ,kwahiyo leo hii ukimruhusu mwanaume alie inaonekana kama umeruhusu udhaifu lakini naye ni binadamu anahisia kama wengine.

“Kwa hiyo ninachosema ni kwamba kumsahau mtoto wa kiume katika malezi na kumsaidia kumjengea uwezo baadaye ni changamoto pia hii husababisha wanaume kuwa kwenye matatizo.

SABABU ZA KIBAOLOJIA

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Afya ya Akili, Dkt.Fileuka Ngakongwa anasema zipo sababu ya takwimu hizo kupishana kwa kiwango kikubwa.

“Afya ya akili inamlenga kila mwanadamu na jinsia zote lakini ukiangali uwiano kati ya wanawake na wanaume unatofautiana mfano nitoe ugonjwa skizofemia(kichaa).

“Hapo uwiano kati ya mwanaume na mwanamke ni mbili ya moja kibaolojia wanaume wanaweza kupata mara mbili zaidi ya wanawake na pia wanaume wanawahi haraka kupata kwa umri mdogo kulinganisha na wanawake lakini ukija kwenye sonona uwiano unaweza kuwa sawa lakini kwa wanaume ni mkubwa zaidi,”anabainisha.

HII NI NAMNA YA KUJISAIDIA

Msaikolojia Bwaya anasema wanaume wakubali kuwa kuna vitu wakivishikilia kama alama ya uanaume vinaweza kuwaponza.

Anawataka wanaume kujenga mifumo itakayowasaidia kutoa sumu kwenye mioyo yao wasiogope kudhalilika.

“Wawe na watu wa karibu ambao anaweza kuwaambia vitu vyao bila kuogopa atakuona vipi,Kuwa na marafiki wa karibu kama wanawake wanavyofanya kuwa na marafiki na kuongea nao.

“La pili kujenga tabia ya kushughulikia vitu na sio kusubiri tatizo kuwa kubwa,mwanaume anapohisi anamaumivu atafute msaada wa wataalamu na kutokuamini kuwa tu yuko vizuri kuwa anavaa suti na tai lakini ndani anaugua lakini anajitenga na watu anakataa tamaa inabidia atafute msaada.

“Kingine wanaume waoneshe hisia pale unapoona kuwa unajisikia vibaya onesha hisia mfano kuhuzuni na kulia ni namna ya kukabiliana na tatizo ukikimbia hiyo unakuwa na tatizo ,Watu wasiogope kuonesha hisia hii inasaidia,”anashauri Bwaya.

Lema anasema kwasasa wanaendelea kuhamasisha wanaume wazungumze kuhusu matatizo wanayopitia.

“Wanaume tunazungumza kwa namna gani kuna vile vikao vya kiume ,vikao vya baba na kijana wake,kaka na mdogo hivi vikao tuzungumze kuelezea hisia zetu na wakati mwingine sio tu kuonesha uwezo tulionao lakini pia namna gani tunaweza kupambana na madhaifu yaliyopo.

“Ukiacha kuongea kitu kingine wanaume pia tusitumie vilevi kama sehemu mmoja wapo ya kuendana na maisha tunavyokabiliwa na changamoto tutafute maarifa ya kutatua kuliko kujiingiza kwenye kujiendana na matatizo kwa njia ya vilevi.

“Lakini kingine ninachoweza kusema ni vizuri wanaume wakajengewa uwezo wa kuhimili changamoto za sasa kwasababu changamoto wanazokutana na wanaume wa sasa ni tofauti na zamani nasema hivyo kwasababu mwanamke amewezeshwa yuko juu sasa na anakipato,”anaeleza Lema.

AINA ZA MAGONJWA YA AKILI

Dkt.Ngakongwa ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili anasema kuna aina nyingi ya magonjwa ya akili lakini kuna yaliyo maarufu ambayo ni haya.

“Kuna skizofenia wengine wanaita kichaa japo jina hili huwa hatulipendi linaleta unyanyapaa huu unachukua asilimia moja ,ugonjwa mwingine ni sonona unatokea sana kutokana na msongo wa mawazo huu unaenda hadi asilimia 25 mpaka 35 ni watatu kuleta uzito katika mabadiliko ya afya ya akili.

“Ugonjwa huo pia unaweza kutokana na kurithi mtu anakuwa na hulka za kuchangamka,uraibu wa dawa za kulevya,hofu ya kupitiliza na mengine ,”anaeleza Dkt.Ngakongwa.