Na Esther Macha,Timesmajira, Online, Mbarali
WANANCHI wa Kijiji cha Mbuyuni Kata Mapogoro wilayani Mbarali mkoani Mbeya wameishukuru serikali kwa kurejesha hekta 33 za ardhi yao zilizokuwa kwenye mgogoro na Hifadhi ya Mpanga Kipengele.
Mgogoro huo ulitokana na muingiliano wa matumizi ya ardhi baina ya wananchi hao na shughuli za uhifadhi katika hifadhi hiyo ulikuwa kikwazo kwa wananchi hao kufanya shughuli zao za kiuchumi.
Wakizungumza naTimesmajira leo Juni 26,2023 , baadhi ya wananchi hao wamesema hatua hiyo ya Serikali itawawezesha kuendelea na shughuli za uzalishaji mali kama ilivyokuwa hapo awali.
“Kupitia hii changamoto wananchi tulikuwa tumebanwa lakini tunapenda kuishukuru Serikali kwa sababu imejaribu kutufikiria.” amesema Nelly Mjanga, mkazi wa kijiji cha Mbuyuni.
Wananchi hao wamesema kuwa mgogoro huo pia ulisababisha kukosa maeneo ya kulishia mifugo yao, hivyo uamuzi huo wa Serikali umeleta faraja kubwa kwao.
“Kuna nafasi tutapewa maana awali tulikuwa tunashindwa hata kusafisha tenki letu la maji lakini kwa sasa hali itakuwa tofauti.” amesema mkazi mwingine wa kijiji hicho, Peter Njoyo.
Naye Kamanda wa Uhifadhi Nyanda za Juu Kusini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Nyama Pori Tanzanzania, (TAWA), Joas Makwati, amesema hatua hiyo itasaidia kumaliza mgogoro uliokuwepo baina ya TAWA na wananchi hao ulioharibu mahusiano mema baina ya pande hizo.
“Siku hii ya leo tulikuwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali kwa ajili ya kutoa tamko la serikali ya zoezi la kuweka mpaka wa hifadhi ya Mpanga Kipengele uwekaji wa mpaka huu unafuatia maelekezo ya serikali kupitia kamati ya mawaziri nane wa kisekta iliyofanya tamthimini mwaka 2022, kwa ajili ya vijiji 975,” .
Amesema kuwa serikali imeamua maeneo ya hifadhi na maeneo ambayo wananchi walikuwa wanatumia kwa kazi zao sehemu ya ardhi zile zibaki kwenye vijiji hivyo na Mpanga Kipengele ni miongoni mwa maeneo ambapo sehemu ya ardhi ya imemegwa na kubaki kwenye vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo “amesema Kamishna Makwati .
Hata hivyo kamishna Makwati amesema kuwa eneo la Mbarali ambayo ardhi yake inachangia kwenye sehemu ya hifadhi ya Mpanga Kipengele hekari 4,200 zimemegwa kutoka ndani ya hifadhi ambazo sasa zinaenda kuachwa kwenye maeneo ya vijiji.
Ardhi iliyomegwa kwa maelekezo ya serikali ni kwamba serikali itaenda kupanga upya na kuvigawia vijiji kwa matumizi mbali mbali na hatua hiyo inaenda kuondoa migogoro ya matumizi ya ardhi kwa wananchi .
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Denis Mwila, amesema hekari hizo 33 zilizorudishwa zitakuwa chini ya usimamizi wa Serikali ambayo ndiyo itakayozigawa kwa wananchi ili kuepusha baadhi ya watu wasio waaminifu kuingilia ugawaji wa ardhi hiyo.
Aidha amesema kuwa hifadhi imerudisha kwa serikali hivyo utapangwa utaratibu mpya kuona kwamba ardhi hiyo inasawaidia wananchi kwa ujumla wao na sio mtu mmoja mmoja.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili