December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hifadhi Saccos yaleta neema kwa watumishi TANAPA

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

MFUKO wa Hifadhi Saccos Ltd unaojishughulisha na utoaji mikopo kwa watumishi wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) nchini umewezesha watumishi kupata mikopo nafuu ya zaidi ya sh bil 80 tangu kuanzishwa kwake.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Taasisi hiyo Ibrahim David alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea banda la Mfuko huo katika Viwanja wa Maonesho ya Ushirika Mkoani Tabora jana.

Amesema kuwa Taasisi hiyo iliyoko Jijini Arusha ilianzishwa mwaka 2000 hapa nchini na hadi sasa ina zaidi ya wanachama 1050 na imetoa mikopo nafuu ya maendeleo kwa watumishi walio chini ya TANAPA yenye thamani ya zaidi ya sh bil 80.

Amebainisha malengo makuu ya Taasisi hiyo iliyoko chini ya Wizara ya Mali asili na Utalii kuwa ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi Watumishi wa Mamlaka hiyo kwa kuwawezesha kuanzisha miradi ya maendeleo pasipo kutegemea mishahara.

David amefafanua kuwa mikopo inayotolewa huanzia sh mil 5 hadi 20 na hurejeshwa ndani ya miaka 3 na kuongeza kuwa mikopo hiyo imekuwa na manufaa makubwa sana kwani imewawezesha kupiga hatua kubwa kimaendeleo.

Ametaja malengo mengine kuwa ni kuwezesha mwanachama kujiwekea akiba katika mfuko huo au kununua hisa ili atakapostaafu awe na akiba ya kutosha ambayo itamwezesha kuendesha maisha yake vizuri pasipo hofu yoyote.

Ametaja mipango ya baadaye wa Taasisi hiyo kuwa ni kuanzisha miradi ya uuzaji viwanja kwa wanachama wake ili kuwasaidia kujenga nyumba zao kirahisi na kuwekeza katika taasisi nyingine za kifedha kama vile UTT Amis na nyinginezo.

‘Natoa wito kwa watumishi wote wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) ikiwemo TAWA na TFS kujiunga na mfuko huu ili kunufaika na fursa lukuki zilizopo, ili kujikwamua kiuchumi’, alisema.

Mwanachama wa Mfuko huo Abushi Shaibu amekiri kuwa tangu ajiunge na Taasisi hiyo amepata manufaa makubwa ikiwemo kujenga nyumba ya kisasa, kuanzisha duka kubwa la nguo, kununua gari zuri na sasa anataka kuanzisha mradi wa kuku.

Joseph Gombeni mkazi wa Arusha naye amesema kuwa Mfuko huo umempa manufaa makubwa sana ikiwemo kusomesha watoto kuanzia shule ya msingi, sekondari hadi chuo kikuu na maisha yake ni mazuri sana.

Meneja wa HIFADHI SACCOS Ibrahim David (wa kwanza kushoto) akiwa na wafanyakazi wenzake katika banda lao kwenye maonesho ya vyama ushirika yanayofanyika katika uwanja wa Nane Nane Ipuli Mkoani Tabora