Na Penina Malundo,TimesMajira Online
UPANDAJI miti na uhifadhi wa misitu miti ni moja ya hatua muhimu sana katika kukabiliana na tatizo la ukame katika nchi nyingi kusini mwa jangwa la Sahara.
Tanzania ni miongoni mwa nchi iliyojaliwa kuwa na Misitu au Miti mingi na miti hiyo imesambaa katika mikoa 21 Tanzania Bara na Visiwani kwa vijini na mijini.
Misitu au miti ni muhimu mno katika kuboresha hali ya hewa kutokana na uwezo wake wa kunyonya na kuondoa gesiukaa (carbon dioxide-Co2) kutoka angani, na hivyo kusaidia kupunguza ongezeko la joto duniani.
Asilimia kubwa ya eneo lenye misitu ya kutosha au miti mingi linakuwa na mandhari nzuri ikiwamo kubadilisha hali ya hewa kuwa hali safi na kuongeza gesi ya oksijeni kwa wingi na kufanya mazingira kuwa yakuvutia zaidi.
Misitu na miti kwa kiasi kikubwa husaidia kupunguza kasi ya upepo, kuboresha upatikanaji wa mvua na kuhifadhi wanyamapori ,makazi ya wanyama, uzuia mimomonyoka katika ardhi na usababisha ardhi kuimili mabadiliko ya tabia nchi.
Usimamizi na udhibiti wa shughuli za binadamu katika misitu na mapori umekuwa mdogo sana kiasi cha kusababisha hali ya misitu kutoridhisha na kutoweka kwa kasi sana nchini.
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaendelea kuhakikisha jamii inatunza na kulinda misity na miti iliyopo kwa kutokata hovyo na kwa kutumia kwa matumizi mabaya.
Ili kukabiliana na hali hiyo ni muhimu kwa Watanzania kupanda miti kwa wingi na kuhakikisha miti au misitu hiyo inatunzwa ipasavyo ili iweze kuendelea kutupatia faida ya vivuli,dawa,kukabiliana na Mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kusaidia kuhimili hali ya mmomonyoko ya ardhi.
Akizungumza hivi karibuni Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kampuni ya Green Conserves wazalishaji wa
mkaa wa taka ngumu, Mhandisi Baraka Machumu anasema kunasababu nyingi za ukatwaji wa miti ikiwemo ya Nishati ya kupikia,ambapo Nchini Tanzania zaidi ya asilimia 70 ya watanzania wanatumia kuni na mkaa kama chanzo cha kupikia.
Anasema hali hiyo upelekea uwepo wa ukataji wa miti mingi ili kukidhi hitaji hilo la nishati ya kupikia.
“Inasemekana jiji la Dar es Salaam tu utumia zaidi ya tani laki tano za mkaa kwa mwaka sawa na zaidi ya tani milioni moja za miti yenye ekari zaidi Maelfu ya miti,”Anasema na kuongeza
“Huku watu wengi wanaoishi kwenye vijiji nao kwa asilimia kubwa hawana shughuli nyingi za kuwaingizia kipato kwa hiyo wanatumia nafasi ya kukata miti kwa ajili ya kuuza kwa watu mbalimbali ili waweze kujipatia kipato chao cha kila siku,”anasema .
Machumu anasema miongoni mwa sababu ya watu kukata miti ni pamoja na shughuli za kiuchumi kama kilimo na ujenzi wa miundombinu.
Anasema hali hiyo uchangia ukataji wa miti mingi na uacha ardhi ikiwa haina nguo zake, hapa ndo usababisha changamoto nyingi za kimazingira.
Machumu anasema kuna mtazamo upo kwenye jamii tokea zama za kale, miti imekuwa ikikatwa lakini haiishi.
“Mtazamo kama huu ni hasi na hauna uhalisia wowote maana enzi hizo wingi wa watu walikuwa ni wachache,”anasema na kuongeza
“Tunahitaji tubadili mtazamo, tutafute fursa zingine za kujiongezea kipato kwa kuacha kukata miti ovyo,hivyo tuweze kurudisha miti baada ya kujenga miundombinu,”anasema
Kwa Upande wake Mtaalamu wa Masuala ya Mazingira kutoka Taasisi ya Jielimishe Kwanza,Henry Kazulla anasema suala la ukataji miti limekuwa likichangiwa na shughuli za kibinadamu katika nyanja ya kujiinua kiuchumi na suala la ujenzi.
Akitolea mfano kwa Mkoa wa Dar es Salaam,Kazula anasema matumizi ya mbao yameshika kasi kuwa sehemu ya mapambo katika maeneo ya biashara pia kutengenezea thamani.
Anasema kuna matumizi makubwa katika utumiaji wa mbao ambapo asilimia kubwa inatokana na miti.
“Ukataji wa miti katika matumizi ya mbao ndio sababu ya kufanya kuwepo na wingi wa ukataji wa miti na kufanya mabadiliko ya tabianchi kuweza kutokea,”anasema.
Aidha anasema upanuzi na matengenezo ya barabara yasiyozingatia urejeshaji wa ekolojia japo kwa asilimia chache unasababisha ukataji wa miti ovyo.
“Hali ilivyo sasa, utashuhudia maeneo ya mijini kuona miti inaondolewa kwa kasi ili kupisha matengenezo ya barabara bila kuzingatia kuirudisha au kuwa sehemu ya mipango,”anasema na kuongeza
“Inasikitisha kuona tunaondoa miti bila kuirudisha,ifikie mahali tunapokata miti tuhakikishe tunairudisha ili kuendeleza uoto wa asili,”anasema.
Kwa Upande wake,Mkurugenzi wa Adaptation hub ambaye pia niMkurugenzi wa Taasisi inayojishughulisha na Utoaji wa Elimu wa Mabadiliko ya Tabianchi(HUDEFO),Sara Pima anasema suala la upandaji miti ni vema lifatiliwe kwa undani zaidi na katika upandaji miti huko kuangaliwe ni namna gani miti inapandwa kitaalamu.
“Ifike wakati watu wanapaswa kuangalia miti inavyopandwa kitaalum na ijulikane inatakiwa kupandwa wakati gani,kujua aina ya mti unaopandwa ili kujua kama unaweza kustawi katika eneo husika unalopanda,”anasema.
Anasema taasisi yao ya HUDEFO,Adaptation hub kwa pamoja wameweza kushirikiana na Tanzania Forest Service ambapo wamekuwa wakiwapatia miti kutoka sehemu mbalimbali ili kusaidia kuwapa watanzania na kuwapa maelekezo ya namna ya upandaji wa miti hiyo.
Anasema hewa ya ukaa ni chanzo kikubwa ya mabadiliko ya tabia nchi hivyo upandaji miti ni muhimu kwa kupendezesha mazingira na kulinda mazingira ya jamii mbalimbali.
“Sisi kama Adaptation hub tumeweza kukutanisha wadau kutoka mikoa mbalimbali waweze kushiriki kwa njia ya mtandao katika mafunzo mbalimbali,tangu mwaka umeanza na sasa kuelekea kuisha tumekuwa tukitoa mafunzo mbalimbali kutoka kwa wataalamu wa mazingira ambapo utoa masomo ya Mazingira na mabadiliko ya tabianchi,”anasema
Aidha anasema wanaishukuru serikali kupitia wataalamu wake katika kutoa mafunzo hayo ili kuhakikisha jamii inalinda mazingira yanayowazunguka.
Pima anasema wanajipanga kikamilifu kuhakikisha mwaka 2021 katika siku ya mazingira kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wanapanda miti sehemu mbalimbali ikiwemo katika nyumba za ibada.
Naye Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Korogwe Mkoani Tanga,Abdallah Lungo anasema tayari wameweza kufikia shule mbalimbali na kuanzisha vitalu vya miche ya miti shule ikiwa na lengo la kufundisha umuhimu wa upandaji miti kuanzia ngazi za chini.
“Tunapoanzisha vitalu vya miche katika shule mbalimbali lengo letu kama serikali ni kuhakikisha vijana hawa wanakuja kuwa watu wanaojali na kuona umuhimu wa upandaji wa miti na wao kuwa mabalozi wazuri kwa watu wanaofanya uharibu miti,”anasema.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika