January 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wanaohatarisha usalama Mbeya

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya limesema litaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayekiuka sheria na kuhatarisha usalama wa Mkoa huo.

Kauli hiyo imetolewa Januari 17,2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga wakati wa sherehe ya siku ya familia ya Polisi mkoani humo (Police Family Day) iliyofanyika uwanja wa mazoezi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mbeya.

“Hatutasita kuchukua hatua za kisheria kwa mtu ambaye atabainika kuhatarisha amani katika Mkoa huu wa Mbeya,”amesema Kuzaga.

Adha Kuzaga alimpongeza na kumshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura, kwa kuendelea kuisimamia vizuri Jeshi hilo na kwa maelekezo ya mara kwa mara yanayopelekea kutenda kazi kwa Nidhamu, Weledi na Uadilifu wa hali ya juu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amepongeza utendaji kazi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.

“Sisi kama Serikali tunaunga mkono utendaji kazi wa Polisi kwa kuhakikisha tunawapatia vitendea kazi vya kisasa ikiwemo magari na vifaa vingine vya TEHAMA, ili kurahisisha na kufanikisha kuzuia uhalifu,”

Akiongea kwa niaba ya wenzake, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Emmanuel Nsajiwa,kutoka Wilaya ya Rungwe,ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia nidhamu, haki, weledi na uadilifu.

Katika sherehe hizo Askari nane akiwemo Mkaguzi wa Polisi mmoja,walitunukiwa vyeti vya sifa na zawadi kwa kufanya vizuri zaidi katika utendaji kazi kwa kipindi cha 2024/2025.

Sherehe za siku ya familia ya Polisi hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwakutanisha Askari, Watumishi raia, familia za Askari na wadau wa Jeshi la Polisi,ambazo uambatana na utoaji wa zawadi kwa askari waliofanya vizuri zaidi, michezo, burudani na sherehe ya kuwaaga na kuwakaribisha maofisa na Askari waliofanya kazi katika Mkoa husika.