Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Handeni
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga Mussa Mwanyumbu amesema bado wanahitaji huduma za Shirika la World Vision kwenye tarafa sita za halmashauri hiyo ili kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Amesema anajua, shirika hilo limeshahudumia tarafa zote sita za halmashauri hiyo za Magamba, Mzundu, Sindeni, Mazingira na sasa wanakamilisha Kwamsisi na Mkumburu, lakini kama wataweza kurudia kwenye tarafa moja ama mbili, itawasaidia sana wananchi wa halmashauri hiyo.
Ameyasema hayo Desemba 17, 2024 kwenye kikao cha tathimini cha utekelezaji wa miradi ya World Vision kwa mwaka wa fedha wa shirika hilo (Oktoba Mosi 2023 hadi Septemba 30), na kushirikisha madiwani, Wakuu wa Idara wa Halmashauri hiyo, watendaji wa World Vision, viongozi wa ngazi ya jamii kutoka Mkumburu AP na Kwamsisi AP, viongozi wa dini na wadau, na kufanyika Ukumbi wa Halmashauri mjini Mkata.
“Halmashauri yetu ina tarafa sita, na tunashukuru sana kwa hizo tarafa mbili mnazotoa huduma. Lakini basi kwa vile na ninyi mna ngazi zenu za juu, mtufikishie ombi letu kuwa msaada wenu kwetu bado unahitajika. Kwa hiyo endapo kuna mafikirio mengine, basi huku nako wasisahau kutuongezea angalau tarafa moja au mbili. Na kusema ukweli, huduma zenu bado tunazihitaji, pamoja na kwamba zilianza muda mrefu.
“Lakini tuwaambie World Vision tunawashukuru sana maana mmeanza kuisaidia hii jamii ya Wilaya ya Handeni miaka mingi, na kazi zenu zinaonekana, kwani wananchi wanaziona, Serikali inaziona, na hata Mungu anaziona. Na World Vision niwaahidi kwamba, pale mnapotaka ushirikiano na halmashauri tutatoa bila kusita, na tutatoa ushirikiano wa hali na mali” alisema Mwanyumbu.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni ambaye pia ni Afisa Tarafa ya Kwamsisi Lugaila Nkwabi, alisema kazi zinazofanywa na Shirika la World Vision ni kielelezo cha kumsaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutoa huduma za jamii kwa wananchi, hivyo kama Serikali, wataendelea kutoa ushirikiano kwa shirika hilo ili wasiweze kukwama katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.
“Niwapongeze World Vision kwa kumsaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutatua changamoto za wananchi kwenye suala la huduma za jamii. Ninachokitaka ni ushirikiano katika kutekeleza miradi ikiwemo ile ya maji, kwa ushirikiano huo kufanywa kati ya halmashauri na World Vision.
“Ni huzuni kuona tunaletewa miradi, lakini baadhi ya miradi hiyo inasinzia. Hivyo nataka viongozi wa miradi ngazi ya jamii (Mkumburu AP na Kwamsisi AP) muweze kushirikiana na viongozi wa Serikali ngazi ya kata, vijiji na vitongoji ili miradi hiyo isiweze kukwana, na iweze kuleta tija kwa wananchi. Ila niombe World Vision, wasisitishe kutoa chakula kwa wanafunzi shuleni, na niombe chakula hicho kiendelee kutolewa” alisema Nkwabi.
Akiwasilisha taarifa yake, Mratibu wa Mkumburu AP Daniel Chuma, alisema jumla ya sh. 411,296,245 zimetumika kwa ajili ya miradi iliyotekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja 2023/2024. Miradi hiyo imegusa kwenye maji, afya, usafi, lishe, na ufadhili (Mambo mtambuka- Utetezi, jinsia, haki za watoto), na Mradi wa Maishilio (THRIVE 2.0).
Naye Mratibu wa Kwamsisi AP Evodia Chija alisema katika kipindi hicho, sh. 700,144,832 zilitumika kwenye afya, lishe na usafi wa mazingira , elimu, pamoja na ufadhili kwenye ulinzi na utetezi wa mtoto.
More Stories
NIDA yawakumbusha wananchi kuchukua vitambulisho vyao
Dkt.Kafumu:Uteuzi wa Rais Samia umezingatia katiba
Kliniki ya sheria bila malipo yazinduliwa Kilimanjaro