March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmshauri ya Mji Korogwe wajipanga kuwa Manispaa

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe

MWENYEKITI mpya wa Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga Ali Mkwavingwa amesema dhamira yake ni kuona halmashauri hiyo inakuwa Manispaa baada ya kuwa Halmashauri ya Mji kwa miaka 20.

Amesema moja ya vigezo vya kuwa Manispaa ni halmashauri kuwa na uwezo wa ukusanyaji mapato, hivyo kwao hilo linawezekana sababu halmashauri hiyo ipo njia kuu ya kwenda mikoa ya Kanda ya Kaskazini na nchi jirani ya Kenya, hivyo kuwa na fursa nyingi za kibiashara.

“Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe, Zahara Msangi, akizungumza kwenye Baraza.”

Ameyasema hayo Februari 10, 2026 kwenye kikao cha Bajeti cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, ambapo aliwataka madiwani wenzake kutafuta fedha kwa udi na uvumba ili kuhakikisha, pamoja na mengine, wanamaliza viporo vya miradi yote ya afya, elimu na Ofisi za Kata majengo yake yanakamilika.

“Sisi tumepokea uongozi kutoka kwa wenzetu waliotutangulia huko nyuma. Wenzetu waliitoa halmashauri hii kwenye Mamlaka ya Mji Mdogo mwaka 2004/2005 ndiyo imepata kuwa Halmashauri ya Mji Korogwe. Baada ya ndani ya miaka 20 sisi tuseme itoshe kwamba tumepambana na mtoto huyu wa Halmashauri ya Mji ambaye alitoka kwenye mjukuu wa Mamlaka ya Mji, na sisi tuna dhamira ya kuipeleka Halmashauri ya Mji Korogwe kuwa Manispaa ya Korogwe.

“Kwenda Manispaa ya Korogwe ni lazima sisi viongozi tushikamane, tupambane, na kuhakikisha tunailinda halmashauri yetu kwenye ukusanyaji wa fedha na matumizi yake. Lakini pia tunawaleta Investors (Wawekezaji) kuwekeza kwenye maeneo yetu, sababu maeneo ya uwekezaji tunayo. Mji wetu ni Corridor hii (Ushoroba), sisi na Dar es Salaam na mikoa ya Kaskazini ni Corridor hii, ni mji wa kimkakati. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatuahidi Bandari Kavu, na sisi tunaendelea kuipambania, na kuna maeneo ya ardhi tunakwenda kuyapima kwa sababu ya viwanda, hivyo watu wajiandae kujitokeze kuja kuwekeza” alisema Mkwavingwa.

“Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe, Ali Mkwavingwa akizungumza kwenye Baraza.”

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mara baada ya kikao hicho, Mkwavingwa aliwekea mkazo aliyozungumza ndani ya kikao cha Baraza la Madiwani, kuwa wanahitaji fedha ili kwenda kutekeleza miradi ya ndani, na kuongeza kuwa kwenye miradi ya ndani kwenye kipindi chake cha miaka mitano hataki kuacha viporo, hivyo anataka maboma yote ikiwemo Ofisi za Mtendaji Kata ambapo ujenzi wake ulisimama kwa miaka 20, ujenzi wake lazima uendelee.

“Tunahitaji fedha kwa ajili ya kwenda kutekeleza miradi ya ndani. Miradi ya ndani hii, mimi katika uongozi wangu nahitaji tusiache viporo viporo, na ndiyo maana tumeingia na kusisitiza maboma yote hasa Ofisi za Kata ambazo zimejengwa kwa miaka 20 huko nyuma mpaka leo zimesimama, tuhakikishe zinakamilika kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Na ukiangalia kwenye bajeti ya mapato yetu ya ndani, ofisi nyingi tumezitengea fedha kwa ajili ya kwenda kuzikamilisha na kufanya ukarabati.

“Nimefanya hivyo sababu asilimia kubwa kwenye kata, Watendaji wa Kata wanapata shida ya kutafuta fedha ili kulipa fedha kwa ajili ya majengo waliyogeuza Ofisi za Kata, ambapo kwa mipango yetu ya ndani, hiyo haileti heshima ndipo nikatenga fedha. Sasa fedha hizi lazima tuzitafute kwa udi na uvumba, sababu bajeti yetu hii ya safari hii imekuwa kubwa tofauti na huko nyuma sababu tunatenga zaidi ya asilimia 40 kwenda kwenye shughuli za maendeleo, tunapozungumzia asilimia 40 ni sawa na sh. milioni 800 ya bajeti yetu ya ndani” alisema Mkwavingwa.

“Mchumi wa Halmashauri ya Mji Korogwe, Anna Kiwelu, akisoma bajeti kwenye Baraza.”

Mkwavingwa alisema kwa muktadha huo, kunahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya Madiwani, Wakuu wa Idara na Vitengo kuhakikisha wanakusanya mapato ya kutosha ili kufikia malengo, na kusisitiza kuwa kazi ya kukusanya baadhi ya mapato ambayo inawafanya wapate hasara, hiyo watakusanya kwa kutumia Wazabuni.

“Vyanzo vinavyosuasua sisi tumetoa maelekezo, sababu kuna kipindi sisi tunatumia fedha nyingi kufanya operation (ukusanyaji). Na nazungumzia hilo, kwa mfano, utakuta chanzo tumekiwekea sh. milioni 50 kwa mwaka, lakini kwa mwaka operation iliyotumika kwa mwaka mzima labda imetumia sh. milioni 15. Ni zile timu zimetoka , hivyo zinatumia kati ya sh. milioni 15 hadi sh. milioni 20, lakini zinakusanywa sh. milioni 30, hata makisio ya kukusanya sh. milioni 50 hayakufikia, hivyo hakuna tija iliyopatikana.

“Kwa hiyo tuna haja kubwa kuhakikisha kwamba vile vyanzo ambavyo havileti tija basi tumeelekeza kwenye baraza kwamba Mkurugenzi aende akaangalie namna ambayo tunaweza kutafuta wazabuni ambao watatusaidia kukusanya fedha hiyo, sababu ukimpa mzabuni chanzo cha sh. milioni 30, yeye mwenyewe ndiyo atapambana kuona anawatafutia chanzo hicho, badala ya sisi tunakitafuta chanzo hicho, huku tunatumia tena mapato ya ndani kutafuta fedha ambayo haileti tija” alisema Mkwavingwa.

“Madiwani wakifuatilia usomwaji wa bajeti kwenye Baraza.”

Akizungumza kwenye Baraza hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Zahara Msangi aliwataka Madiwani, Wakuu wa Idara na Vitengo kushirikiana ili kuweza kufikia malengo ya ukusanyaji wa Mapato ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2026/2027, kwani bajeti hiyo kwa Mapato ya Ndani itakuwa sh. 3,433,697,000 ikiwa ni ongezeko la sh. 194,187,000 sawa na asilimia 5.99 ukilinganisha na ile ya mwaka wa fedha 2025/2026 ya sh. 3,239,510,000.

“Wakuu wa Idara na Vitengo wakiwa kwenye Baraza.”

Akisoma bajeti hiyo, Mchumi wa Halmashauri ya Mji Korogwe, Anna Kiwelu alisema kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Halmashauri ya Mji Korogwe inakisia kukusanya na kupokea sh. 34,752,078,000 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato. Mapato ya Ndani sh. 3,433,697,000, Matumizi mengineyo (Mishahara na other charges) sh. 24,445,498,000, na Miradi ya Maendeleo (Serikali Kuu na Wadau wa Maendeleo) sh. 6,872,886,000.

“Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe, Ali Mkwavingwa (katikati) akimkabidhi Kishkwambi Diwani wa Kata ya Majengo, Mustapha Shengwatu. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Nassoro Mohamed.”
“Madiwani wa Korogwe TC wakionesha Vishkwambi walivyokabidhiwa na halmashauri ili kurahisisha shughuli za Baraza na Kamati.”