Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo (Mb.) ameeleza kuwa Serikali imejipanga kuzisimamia na kuziwezesha Halmashauri hususan za mipakani kuwa kiungo muhimu kwenye masuala ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa za Mtangamano.
Mhe. Londo ameyasema hayo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tanga yakutembelea Kituo cha Utoaji Huduma kwa Pamoja Mipakani cha Horohoro/Lungalunga (Horohoro One Stop Boarder Post- OSBP)
Ziara hiyo ililenga kuangalia utekelezaji wa shughuli za Himaya Moja ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na hali ya miundombinu na uendeshaji wa OSBP hiyo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Londo amepata fursa ya kuzungumza na Wafanyakazi wa Taasisi mbalimbali zinazotoahuduma katika OSBP na kutoa wito kufanya kwa uadilifu na weledi ili kutimiza azma ya Serikali ya kuhamasisha mtangamano kwa lengo la kukuza muingiliano na bishara za mipakani.
Mhe. Londo ameahidi Serikali itaendelea kutatua changamoto za kiuendeshaji zinazozikabili OSBP hiyo pamoja na changamoto wanazokutana nazo wafanyabiashara katika mpaka huo na mingine nchini.
“Jumuiya ina fursa nyingi ambazo hazijatumika ipasavyo kwa manufaa ya wafanyabiashara wetu ni vema halmashauri zikabuni mbinu na mikakati ya makusudi kuwawezesha Wafanyabiashara hususan wadogo kuongeza thamani ya bidhaa zao ili ziweze kuuzwa bila vikwazo katika nchi za Jumuiya”, alisema Mhe. Londo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Londo alipata fursa ya kukutana na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Tanga akiwemo Mkuu wa Mkoa, Mhe. Balozi Batilda Buriani, Afisa Tawala wa Mkoa, Bi. Pili Mnyema, wawakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Wawakilishi kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Tanga pamoja na Wafanyabiashara na Mawakala wa Forodha wanaofanya shughuli zao katika mpaka wa Horohoro.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais