November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri zaagizwa asilimia 10 za mikopo kuanzisha vitalu miche ya parachichi

Na Esther Macha,Timesmajira Online, Busokelo

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameagiza halmashauri zote nchini asilimia 10 zinazotengwa kwa ajili ya mikopo kuelekezwa kwenye kuanzisha uzalishaji wa vitalu vya miche ya zao la parachichi na kusambazwa kwa wakulima bure ili kuongeza tija ya uzalishaji.

Majaliwa ametoa maagizo hayo wakati alipotembelea mashamba ya kilimo cha zao la parachichi katika kiwanda cha Kuza wilayani Rugwe Mkoa wa Mbeya na kuagiza Maofisa Kilimo wote, kwenda mashambani kwani wamekuwa wanakaa na kutokua na mashamba ya mifano.

Amesema Maofisa Kilimo si kazi yao kukaa maofisini na badala yake, kwenda mashambani kutoa elimu kwa wakulima kwani kazi yao ni kukaa vijijini na si maofisini.

Waziri Mkuu amesema Wilaya ya Rungwe, wananchi wake wamekuwa wakijikita katika kilimo cha zao hilo na kwamba kama serikali, itaboresha mifumo rafiki ya masoko ya uwekezaji mkubwa kwa wakulima wilayani humo na kupiga marufuku mfumo wa rumbesa wa mazao hususan viazi mviringo.

Pia amesema malengo ya ziara yake ni kuangalia utekeleza wa maagizo ya serikali katika halmashauri zote, ikiwa ni pamoja na kutatua kero na migogoro kwani ndiyo kazi yake kwa Watanzania.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo amesema wakulima wa Wilaya ya Rungwe wanalima mno mazao, lakini changamoto kubwa kwao ni ukosefu wa masoko.

Amesema mara nyingi wakulima wamekuwa jitihada kubwa za kilimo cha ndizi,viazi, maparachichi na matunda ya aina mbalimbali,tunaomba mtusaidie kiwanda ambacho kutasaidia wakulima kupeleka matunda yao badala ya kuharibika.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe amesema hivi karibuni watakaa na Wakuu wa Mikoa wote nchini ambako wanazalisha viazi, ili kuondoa tatizo la kuuza viazi holela.