December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri yatoa mikopo kwa vikundi 78 vya wajasiriamali

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeweza  kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi 817,400,000 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha kwa vikundi 78.

Mikopo hiyo ni pamoja na  vifaa mbalimbali kwa vikundi vya ujasiliamali ikiwa ni pamoja na lori aina ya fuso tani saba kwa ajili ya kubebea mchanga na matofali, ikiwa ni asilimia kumi ya mapato ya ndani ambayo yanatakiwa kurejeshwa kama mkopo kwa Vijana, Wanawake, na Watu Wenye Ulemavu.

Akikabidhi mikopo hiyo jiji hapa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Jabir Shekimweri amesema kuwa mikopo hiyo ni kwa ajili ya shughuli za viwanda,Guta 1,Lori moja la kubebea tofari na mchanga,fuso tani saba na mikopo kwa ajili ya biashasha ndogondogo, mikopo ya kilimo,mikopo ya mifugo na mikopo kwa ajili ya mama lishe na baba lishe.

“Mikopo hii itumike katika kuwaletea maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja,jamii inayomzunguka pamoja na Taifa kwa ujumla kwa kutimiza niya ya serikali ya kukuza uchumi wa mtu na uchumi wa vitu”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji hilo Joseph Mafuru amefafanua kuwa katika mikopo hiyo iliyotolewa vikundi 46 vya wanawake wamepata sh.395,000,000 ,vikundi 23 vya vijana wamepata sh.364,000,000 na vikundi 19 vya watu wenye ulemavu wamepata sh.58,400,000 na kufanya jumla ya vikundi 78 kupata jumla ya fedha sh.817,400,000.

Amesema hayo yote ni katika kutekeleza sera ya kutoa asilimia kumi katika makundi ya vijana,akina mama na makundi maalumu.

“Hata hivyo taarifa inaonesha kwamba shilingi 3,981,070,933.62 tu ndizo zimerejeshwa ambapo ni sawa na asilimia 44.9 ya kiasi kilichotolewa cha mikopo iliyotolewa”amesema.

Naye Mbunge wa jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde amewataka wanavikundi wote wanaonufaika na mikopo hiyo kuitumia kwa lengo lililokusudiwa huku akiimwagia sifa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutekelezwa kwa kiwango kikubwa takwa hilo la kisera la kutoa asilimia kumi ya  mapato ya ndani kwa makundi hayo.

Akitoa ushuhuda katika hafla hiyo, mwenyekiti wa kikundi cha Ilumbo Group ambacho kilishanufaika na utaratibu huo Monica Masado amesema kikundi hicho kimekuwa wanufaika wakuu wa mikopo kutoka katika halmashuri ya Jiji la Dodoma.

Monica amesema kuwa mikopo hiyo ambayo inatolewa na halmashauri ya Jiji imeweza kuinua maisha ya watu pamoja familia zao na kusema kuwa wakopaji wanaokopa wanatakiwa kuhakikisha wanakopa na kurejesha kwa wakati.

Naibu Meya wa Jiji la Dodoma Emmanuel Chibago amewataka wakopaji kufanya shughuli za maendeleo badala ya kukopa na kutumia fedha hizo kwa shughuli tofauti na makusudio ya kikundi jambo ambalo linaweza kusababisha kushindwa kufanya marejesho ili vikundi vingi zaidi viweze kukopeshwa na Halmashauri hiyo.