December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga yapongezwa kwa makusanyo mazuri

Na Suleiman AbeidTimesmajira Online,Shinyanga

HALMASHAURI ya Wilaya ya Shinyanga imepongezwa kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.Kwa kipindi cha mwaka 2023/2024 imekusanya kiasi cha bilioni 3.288 sawa na asilimia 101 ya lengo la makusanyo kwa mwaka.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Vijijini,Edward Ngelela kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichoketi kwa ajili ya kupokea taarifa ya hesabu za mwisho kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2024.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Edward Ngelela, akizungumza na Madiwani na Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga(hawapo pichani) kwenye kikao cha Baraza la Madiwani

Ngelela amesema,mafanikio ambayo yamepatikana kwa mwaka wa fedha uliopita yanapaswa kuendelezwa badala ya watendaji kubweteka,kwani fedha nyingi inapokusanywa ndivyo Halmashauri hiyo inavyofanikiwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi wake.

“Halmashauri yoyote hapa nchini bila ya mapato haiwezi kufanya jambo lolote lile la kimaendeleo, pamoja na kwamba kuna maeneo wakati wa utekelezaji yanaweza kuwa na changamoto, lakini mmeonesha jinsi gani mmeweza kukabiliana nazo hadi kupata mafanikio,” ameeleza Ngelela.

Hata hivyo pamoja na pongezi hizo, Mwenyekiti huyo amewaomba Watendaji kuhakikisha wanaongeza bidii katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ya ndani,huku wakizingatia weledi na nidhamu wakati wakitekeleza majukumu yao kutoka kwa walipa kodi.

“Tukusanye kodi zetu hizi kwa ustaarabu, tusiwe tunanyanyasa watu na mkizingatie kauli za nyuma za Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan,aliagiza kodi zikusanywe kwa kuelimishwa watu na lengo liwe ni kufikia malengo tuliyojiwekea badala ya kuwakandamiza wananchi na kuwabambikizia faini zisizo sahihi,” ameeleza.

Mwekahazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Thobias Shija akiwasilisha taarifa ya hesabu za mwisho kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo

Kwa upande wake Mwekahazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Thobias Shija, amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2023/2024 Halmashauri ilipanga kukusanya kiasi cha bilioni 3.25,hadi kufikia Juni 30, 2024 ilikuwa imekusanya bilioni 3.288,sawa na asilimia 101 ya lengo la makusanyo.

“Halmashauri yetu katika kipindi hiki, ilipokea fedha za matumizi ya kawaida kutoka Serikali Kuu kiasi cha shilingi bilioni 29.3, sawa na asilimia 104 ya lengo lililokuwa limepangwa la kupokea kiasi cha bilioni 28.25,” ameeleza Shija.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Mboje Ngassa, amesema pamoja na mafanikio hayo hawapaswi kubweteka na badala yake waongeze bidii kwa kipindi cha mwaka huu wa fedha, ili mapato zaidi yaweze kukusanywa hali ambayo itaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri hiyo.

“Mkurugenzi umejitahidi kupeleka fedha katika miradi yote iliyopangwa kama ilivyo kwenye bajeti yetu,niwaombe muendelee na ‘spidi’ hii,mkizingatia kila mwezi na kila kota kupeleka fedha zilizobajetiwa kwenye shughuli zote ambazo zipo kwa mujibu wa bajeti.Ili tutakapomaliza mwaka tusije tukaingia na fedha nyingi ambazo zimevuka mwaka na tukasababisha baadhi ya miradi kucheleweshwa,” ameeleza Ngassa.

“Taarifa hii ni nzuri, maana imeonesha jinsi gani watendaji wetu,wamejituma katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ya ndani, hii itawezesha miradi yetu mingi ya maendeleo kutekelezwa kwa wakati, na sisi jukumu letu ni kusimamia kuona mapato haya yanatumika vizuri,” ameeleza Awadhi Mbarak Diwani wa Kata ya Solwa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Mboje Ngassa (katikati) akiendesha kikao cha Baraza la Madiwani kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dkt. Kalekwa Kasanga na kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri.

Naye Diwani wa Kata ya Nyida Selemani Segereti,ametoa wito kwa wakazi wa Halmashauri ya Shinyanga, kujenga utamaduni wa kulipa kodi na ushuru mbalimbali wa halmashauri kwa hiari bila ya kushurutishwa kwa vile fedha yote inayokusanywa inarudi kwao kwa njia ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.

Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wakifuatilia kikao cha Baraza la Madiwani.