Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online, Tanga
MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kuhakikisha inatenga fedha ili kuweza kulipa madeni ya bilioni 2.306 inayodaiwa na watumishi pamoja na wazabuni jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hyesabu za Serikali (CAG).
Balozi Dkt Buriani ametoa maelekezo hayo wakati akiwa kwenye kikao cha Baraza maalum la kupokea taarifa za CAG kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo Halmashauri hiyo ilipata hati inayoridhisha ikiwa ni mwaka wa tano mfululizo.
“Pamoja na hati safi tuliyoipata na pamoja na kujibu hoja kuna mambo ambayo yametusababishia Halmashauri yetu kuwa na hoja hizi nyingi ambayo yako ndani ya uwezo wetu,tukikubaliana kwa pamoja tunaweza kuyapunguza, ni halmashauri pekee kushinda halmashauri zote yenye madeni mengi ya watumishi na wazabuni,”ameeleza na kuongeza kuwa
“Utayari wa kulipa hauonekani mna madeni ya bilion 2.306 na fedha mnayotenga ni milioni 24 hii tunaona kama ni takrima , tunaelekeza mtenge fedha za kulipa madeni ya watumishi na wazabuni haipendezi hawa watu wanakwenda mpaka kwa Waziri Mkuu kudai madeni jambo hili mkalisimamie,”.
Sambamba na hilo Mkuu huyo wa Mkoa ameitaka kulipa deni la kiasi cha milioni 17 ambalo linadaiwa na watumishi wastaafu katika halmashauri hiyo ambapo ameelekeza kabla ya kufika Juni 30 mwaka huu deni hilo liwe limeshalipwa.
Aidha Dkt Buriani amemelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Saitoti Zelote kuandaa na kufanya tathmini ya miradi yote viporo ambayo imeshindwa kumalizika kwa wakati ikiwemo ya tangu 2008 ambapo yote kwa pamoja inagharimu zaidi ya milioni 600 huku akitaka kuelezwa ni hatua gani zimechukuliwa ili kuikamilisha.
Awali akitoa taarifa ya CAG Hamu Mwakasola ambaye ni Mkaguzi wa nje wa Mkoa wa Tanga amesema katika mapendekezo 41 sawa na asilimia 71 yametekelezwa huku 17 yakiwa bado,hivyo ameitaka halmashauri hiyo kuendelea kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa.
“Nitoe rai kwa viongozi na watendaji kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji,”.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Handeni Vijijini Saitoti Zelote amesema kuwa watahakikisha yale yote ambayo yaliibuliwa kwenye taarifa ya hoja za CAG kwa mwaka wa fedha 2022/2023 wanakwenda kuyatekeleza kwa vitendo.
Amesema kuwa halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ilipangiwa kukusanya kiasi cha bilioni 2.561 huku wakiongezewa kiwango cha milioni 450 ambapo mpaka sasa imefikisha makusanyo ya asilimia 120.
Akizungumza kwa niaba ya Baraza la Madiwani Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mussa Mwanyumbu amesema mpaka kufika Desemba 2024 hoja zote ambazo zilitolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zitakuwa zimefutwa.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato