Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
HALMASHAURI ya wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora imepanga kuwapandisha vyeo watumishi wake 1,702 wa kada mbalimbali katika mwaka wa fedha 2023/2024 na wengine 17 kubadilishiwa miundo ya utumishi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Jerry Mwaga alipokuwa akiwasilisha mapendekezo ya makisio ya bajeti ya maendeleo ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha ujao.
Alisema ili kuleta mabadiliko chanya ya kiutendaji na kuharakisha utekelezaji shughuli za maendeleo ya wananchi katika halmashauri hiyo wamependekeza kupandishwa vyeo watumishi 1702 na 17 kubadilishiwa miundo ya utumishi.
Aidha wamependekeza kuajiriwa watumishi wapya 883 katika sekta mbalimbali zenye uhitaji mkubwa ikiwemo elimu, afya na nyinginezo ili kuboresha utoaji huduma katika sekta husika.
Mwaga alisema katika mwaka wa fedha 2023/2024 wamepanga kukusanya jumla ya sh bil 40.7 kwa ajili ya utekelezaji shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kupandishwa vyeo watumishi, kubadilisha miundombinu ya ajira na kuajiri wapya.
Alibainisha kuwa katika makisio hayo wanatarajia kukusanya mapato ya jumla ya sh bil 5.38 kutoka katika vyanzo vyake vya ndani na ruzuku kutoka serikali kuu ya kiasi cha sh bil 35.35.
Alifafanua kuwa katika vyanzo vya ndani wanatarajia kupata mapato yasiyolindwa ya sh bil 4.96 na mapato lindwa ya sh mil 415.2 yanayotokana na michango ya Bima ya Afya ya Jamii (iCHF), Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF), malipo ya papo kwa papo (user free), michango ya wahisani na mapato mengineyoserikali
Na ruzuku kutoka serikali kuu wanatarajia kupata sh bil 35.35, za mishahara zikiwa sh bil 24.16, matumizi mengineyo sh mil 983.7, ruzuku ya miradi (fedha za ndani) sh bil 5.48 na ruzuku ya miradi (fedha za nje) sh bil 4.71.
Mwaga alieleza kuwa sh bil 40.7 zitakazokusanywa zinatarajiwa kutumika ipasavyo kwa shughuli mbalimbali ikiwemo, mishahara, miradi ya maendeleo na matumizi mengineyo.
Aliongeza kuwa fedha za makusanyo ya ndani kiasi cha sh bil 5.38 zinatarajiwa kutumika kwa mishahara (sh mil 73.7), miradi ya maendeleo (sh bil 1.98), matumizi mengine (sh bil 2.9) na malipo ya bima ya afya na mengineyo (mil 415).
Alisisitiza kuwa mpango wa bajeti hiyo pia umezingatia kulipa stahiki na maslahi ya watumishi ikiwemo nauli ya likizo sh mil 299, madeni ya watumishi sh mil 28.9 na gharama za uhamisho sh mil 162.4.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti