November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri ya Kalambo yapongezwa kwa ubunifu teknolojia ya ukaushaji samaki,dagaa

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Mbeya

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Daniel Chongolo ameipongeza Halmashauri ya Kalambo mkoani Rukwa,kuanzisha teknolojia mpya ya ukaushaji wa dagaa na samaki kwa kutumia kaushio la kisasa (solar tent drier).

Teknolojia hiyo itawezesha upatikanaji wa samaki na dagaa wenye ubora na kuwezesha wavuvi kujikwamua na hali ya kiuchumi.

Ameyasema hayo baada ya kutembelea banda la Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kupitia maonesho ya wakulima Nanenane yanayofanyika kikanda jijini Mbeya

Ameeleza kuwa kuanzishwa kwa teknolojia hiyo pia itawezesha kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvuliwa hususani kipindi cha masika.

Awali akitoa taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Shafi Mpenda ,Ofisa Uvuvi wa Wilaya hiyo Abdul Balozi ,amesema sambamba na teknolojia hiyo pia wameleta bidhaa mpya ya unga wa samaki ambayo ni ya kwanza kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Bidhaa hiyo ambayo itasaidia kupunguza udumavu na utapia mlo kwa watoto kutokana na unga huo kuwa na virutubisho vyote.

‘’Unga huu utaweza kutumiwa na watu wote ikiwemo watoto wachanga na watu wazima na katika kuhakikisha huduma hii inapatika sehemu zote za mwambao wa ziwa Tanganyika kwa kushirikina na mradi wa FISH4ACP tumejenga makaushio makubwa matatu na jiko moja la kubanikia samaki katika vijiji vya Kasanga, Kilewani na Samazi,”ameeleza Balozi.

Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi Nicholas Mrango amesema Halmashauri hiyo imetenga fedha milioni 61,kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe ikiwemo kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya vyakula bora kwa lengo la kutokomeza tatizo la udumavu wilayani humo.