Na Lubango Mleka, Times Majira Online,Igunga
HALMASHAURI ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora imepokea fedha kwa ajili ya walengwa wa TASAF kiasi cha cha bilioni 1.5,ambazo zimelipwa kwa kaya 10,399.
Huku kiasi cha milioni 848.05,kikilipwa tasilimu kwa walengwa 6,019 na milioni 675.54 zimelipwa kwa walengwa 4,380 kwa njia ya mtandao kupitia banki na simu za mkononi.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa TASAF Wilaya ya Igunga Dina Madeje wakati akizungumza na gazeti la majira juu ya kuanza kwa malipo ya walengwa wa TASAF kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Februari,2024.
“Kati ya fedha zote hizo kiasi cha bilioni 1.07, ni ruzuku ya uzalishaji kwa walengwa 3,062 katika vijiji 57 vilivyoanza kutekeleza mpango huo kwa awamu ya kwanza na zoezi lilifanyika kuanzia Mei 14-20 mwaka huu ,”amesema Madeje.
Aliongeza kusema kuwa, mafunzo ya ushauri na uelekezi yametolewa kwa walengwa ili waweze kutekeleza miradi yao kwa usahihi na jumla ya walengwa 3039 wamefikiwa.
“Miradi ambayo inatekelezwa katika Halmashauri yetu ya Wilaya ya Igunga ni pamoja na mradi wa ufugaji nguruwe, kondoo, mbuzi,ng’ombe, kuku, bata pamoja na kuuza vitu mbalimbali ikiwemo matunda, vitenge,duka,mchele, kununua na kuuza mpunga, kuuza vyungu na biashara ya kuuza zabibu,”.
Pia wanamiradi ya saluni za kike, kilimo cha mbogamboga, utengenezaji sabuni, mama lishe, uuzaji wa dagaa na samaki, uuzaji wa vitunguu, mahindi, karanga, maandazi, vifaa vya ujenzi, vinu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, mashuka ya kimasai, mafuta ya taa na kupikia, uuzaji wa vinywaji na biashara ya vitambaa.
Hata hivyo ameeleza kuwa vijiji vyenye wanufaika wa ruzuku ya uzalishaji ni 57 ambapo amewasihii wanufaika wote wa TASAF kutumia mafunzo wanayoyapata kutimiza malengo ya fedha hizo kama ilivyokusudiwa na Serikali.
“Matarajio yangu ni kuongeza kipato zaidi na kuikuza biashara yangu, mpango huu wa kunusuru kaya masikini kwangu mimi nauona ni mpango mzuri sana, kwa kweli ushirikiano upo mzuri kati yetu na viongozi kuanzia ngazi ya kijiji waratibu na waelimishaji wanaotupatia mafunzo haya ya ruzuku ya biashara kama tulivyoomba,”ameeleza Daniel Juma mkazi wa kijiji cha Mangungu.
Pia Daniel ameishukuru serikali kwa kuzipatia familia masikini ruzuku ya kujikimu kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, ambapo aliomba ruzuku ya 350,000 kwa ajili ya biashara ya kibanda cha nguo za ‘spesho’ na amepatiwa kama alivyoomba.
Huku Sara Masimba mkazi wa kijiji cha Mangungu amesema kuwa, yeye aliandika andiko la kuanzisha saluni ya kike na aliomba ruzuku ya biashara kiasi cha 350,000.
Naye Teosifola Ngembe (43) mkazi wa kijiji cha Kalemela mnufaika wa ruzuku ya biashara aliomba kiasi cha 350,000 kwa ajili ya kufanya biashara ya mpunga anasema kuwa mradi wake unaendelea vizuri na ameanza kunufaika nao.
Kwa upande wake, Bahati Kanuti (47) mkazi wa kijiji cha Kalemela amesema niliomba ruzuku ya 350,000 akanunua nguruwe 6 ambao anatumaini kwa muda mfupi ujao wataleta tija kwake na kwa familia yake.
Naye Mtendaji wa kijiji cha Kalemela Clemensia Meteo amesema kuwa mwitikio ni mzuri na wanufaika wanafanya vizuri kama wanavyowapatia elimu juu ya makusudio ya ruzuku wanayoipata na maandiko yao.
“Hivyo tunafanya ufuatiliaji na hata hivi karibuni tumefuatilia maendeleo yao na kuona mafanikio kama tulivyowapatia elimu,”.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja