Na Suleiman Abeid
Timesmajira Online, Shinyanga
HALMASHAURI ya Wilaya ya Shinyanga imetumika kiasi cha zaidi ya milioni 103.4 kwa ajili ya kutekeleza afua ya chanjo ya polio kwa kipindi mwaka 2022/2023 kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Huku katika kutekeleza shughuli mbalimbali za uboreshaji wa sekta ya afya ya jamii na lishe kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 halmashauri hiyo imetumika! kiasi cha zaidi ya bilioni 1.2.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Simon Barege kwenye mkutano wa Baraza la Madiwani robo ya nne ya mwaka 2022/2023 amesema kati ya fedha hizo zilizo tumika katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za afya kiasi cha zaidi ya milioni 103.4 kimetumika kwa ajili ya utoaji chanjo ya polio kwa watoto.
Barege amesema fedha hizo zimetoka Serikali Kuu ambapo halmashauri hiyo imefanikiwa kutoa chanjo zipatazo 284,690 huku kiasi cha cha zaidi ya milioni 15.8, kutoka mfuko wa Global Fund kimetumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa katika Hospitali ya Wilaya, vituo vya afya na zahanati.
“Katika kipindi hiki cha mwaka 2022/2023 shughuli mbalimbali zimetekelezwa ikiwemo utoaji wa huduma za chanjo kwa ajili ya kinga ya polio lakini pia ununuzi wa vifaa tiba na dawa katika hospitali yetu ya wilaya, vituo vya afya na zahanati zetu,tunaendelea na ukamilishaji wa zahanati nne kwa thamani ya milioni 100 ambapo za Manyanda na Ngokolo ujenzi wake umekamilika na zile za Mwandutu na Mwamalulu zipo hatua ya ukamilishaji,” ameeleza Berege.
Berege amefafanua kuwa mbali na fedha hizo kutoka Serikali Kuu pia Halmashauri hiyo imetumia kiasi cha milioni 160, kutoka mapato ya ndani katika kukamilisha zahanati nyingine saba za Kizungu, Bukumbi, Pandagichiza, Ngokolo, Muongozo, Nyang’ombe na Isela na kwamba shughuli za ujenzi wake zipo katika hatua ya ukamilishaji.
“Pia kiasi cha zaidia ya milioni 554 kilichopokelewa kutoka mfuko wa Basket Fund kimetumika ili kuwezesha utoaji wa huduma mbalimbali katika vituo vya afya vya Tinde, Salawe, Samuye, Nindo na ngazi ya hospitali ya wilaya ikiwemo ununuzi wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi, vifaa vya hospitali na maabara,” ameeleza Berege.
Halmashauri hiyo pia imepokea kiasi cha zaidi ya milioni 31.4,kutoka mfuko wa kuchochea maendeleo katika zahanati za Nzagaluba, Ngaganulwa, Igalamya, Mwamalulu, Masengwa, Nyaligongo, Mwamkanga, Nshishinulwa, Bukiligulu, Lyamidati, Mwamanyuda, Bunonga, Ibanza, Kidanda na Mwabundala.
Kwa upande wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo halmashauri hiyo kwa mwaka 2022/2023 imepokea kiasi cha zaidi ya bilioni 2.2,ambapo kati ya hizo zaidi ya milioni 603 ni kwa ajili ya miundombinu ya shule mpya ya sekondari ya Puni.
Vilevile milioni 110,kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za walimu katika shule ya sekondari Igalamya kiasi cha zaidi ya bilioni 1.5, zitaekelezwa kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa 46, matundu ya vyoo 78 na majengo ya utawala mawili katika shule za msingi zilizopo katika Halmashaur hiyo.
“Katika utekelezaji wa miradi hii ya maendeleo, Halmashauri ilipata changamoto kubwa ya kukosekana kwa vifaa muhimu vya ujenzi (mabati) kutokana na mahitaji ya vifaa hivyo kuwa makubwa sana kuliko upatikanaji wake,hali hii ilimlazimu mtaalamu wetu wa Halmashauri kwenda kiwanda cha uzalishaji mabati cha ALAF kilichopo jijini Mwanza na kukaa kiwandani hadi pale mabati yanayohitajika kwa miradi ya ‘Boost’ yalipokamilika kutengenezwa ambapo changamoto hiyo hii kwa kiasi kikubwa ilichangia miradi kutokamilika kwa wakati uliopangwa,” ameeleza Berege.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba