September 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri Rungwe kujenga jengo la kuhifadhia mazao

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

KATIKA kuongeza thamani katika zao la parachichi ,matunda na mbogamboga Halmashauri ya wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya imeanza ujenzi wa jengo lenye baridi litakaloweza kuhifadhi mazao hayo ili yasiharibike na kuyaongezea thamani yaweze kuendana na soko la kimataifa .

Hayo yamesemwa leo Agosti 3,2024 na Mkuu wa idara ya kilimo ,mifugo na uvuvi wilaya ya Rungwe ,Agustino lawi wakati wa maonesho ya nane nane ya wakulima ambapo Kikanda yanafanyika mkoani Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale mkoani hapa.

Lawi amesema kuwa kwa kutambua umuhimu huo halmashauri ya wilaya ya Rungwe imetenga eneo lenye ukubwa wa hekari tano kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mazao ili yasiweze kuharibika.

“Jengo hili la baridi litakuwa msaada kwa wakulima wetu kwenye matunda hususani parachichi na mazao mengine ili yasiweze kuharibika kabla ya kufika sokoni na huu ndiyi mpango wa halmashauri”amesema Mkuu huyo wa idara ya kilimo na mifugo.

Aidha Lawi amesema kwamba katika kuendelea kujiongezea thamani zao la Parachichi halmashauri hiyo inakaribisha wawekezaji nje ya wilaya hiyo kuweza kuwekeza ili kuweza kuendelea kuyaongezea thamani mazao mbali mbali wilayani humo.

“Kwasasa mazao yetu haya yanapakiwa wilaya ya Njombe ambapo inaongeza gharama na kupunguza faida kwa mkulima ambayo angeweza kupata endapo wangeweza kuhifadhi ndani ya wilaya hiyo “amesema Lawi.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Idara amesema wilaya inaendelea kuwahimiza wawekezaji kuwekeza zaidi ili waweze kuhifadhi mazao na kuondokana na adha ya kuharibika kabla ya kuwafikia walaji.

Akizungumza katika viwanja vya maonesho ya nanenene vya John Mwakangale mkulima wa zao la parachichi kutoka wilaya ya Rungwe,Bryson Mbangula ameiomba serikali kujenga viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo mafuta na sabuni ili waweze kuwanusuru na hasara ya kuuza zao hilo kwa bei mbaya na mengine kukosa mahala pa kupeleka na kuishia kuoza.

Joyce Mkumbwa ni msindikaji wa mazao katika Halmashauri ya wilaya ya Rungwe ameishukuru halmashauri hiyo kwa kuwapatia ujuzi wa kusindika mazao.

“Ujuzi huu tuliopatiwa na halmashauri yetu tunaendelea kuufanyia kazi kama hivi unavyoona tumesindika haya mazao yanayotokana na kilimo cha mazao yetu ya Wilaya ya Rungwe tunayolima wenyewe ,mfano hapa tuna ndizi hizi tumetengeneza hapa , mbogamboga za majani kukausha na jua ,viazi,karanga na mazao mengine “amesema Mkumbwa.