Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam
HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam, imebaini uwepo wa leseni na utoaji wa risiti feki kwa baadhi ya wafanyabiashara, zinazodaiwa kutolewa na watumishi wasiokuwa waadilifu katika halmashauri hiyo.
Akizungumza jijini hapa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jomaary Satura amesema hali hiyo imekuwa moja ya chanzo kinachochangia upungufu wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, walipokutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo amesema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa na utaratibu wa kuagiza wengine kuwakatia leseni bila ya kujua watu hao si waaminifu.
“Leo peke yake Mkuu wa Wilaya na jana nimekutumia umeona.. leseni feki, na risiti za malipo feki, jambo ambalo nimemuona Rais akilizungumza na kukemea alipokuwa kwenye mkutano na viongozi wa mikoa Kibaha, wafanyabiashara hawa wa Kariakoo na Dar es Salaam kwa ujumla, hawana muda wa kufuatilia mambo yao au vibali vyao, kwani wanawaza biashara tu na wakati mwingine wanalazimika kuwatuma vijana kufuatilia kwa kuogopa pale Halmashauri mambo ya kushinda kutwa nzima kwenye foleni ,”ameeleza Satura.
Satura amesema, baada ya kubaini uwepo wa udanganyifu wa aina hiyo, waliamua kujiridhisha kwa kuingia katika mifumo na kugundua leseni hizo hazipo.
“ili tujiridhisha, tuliamua kuingia kwenye mfumo hatuoni leseni kumbe zimetengenezwa stationary, ninyi mnajua malipo yenu mmelipa na mnahitaji huduma lakini zaidi ya asilimia 50 ya leseni zinazoendelea hapa mjini ni leseni feki,” amesema Satura na kuongeza kuwa
“Lakini risiti mnazopewa kwa ajili ya malipo mbalimbali nazo ni feki, kwa hiyo mnajua mnatoa fedha kwa ajili ya maendeleo ya taifa hili, kumbe fedha hizo hazifiki serikalini,”.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akizungumzia hali ya udhibiti na ukusanyaji wa mapato katika Jiji la Dar es Salaam, amewataka wafanyabiashara kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha wanafuata taratibu za upatikanaji wa leseni halali.
Aidha katika kipindi hiki cha kuhuisha taarifa za wafanyabiashara aliwatoa hofu kuwa hakuna mfanyabiashara atakaye nyanyaswa au kubughudhiwa na maofisa wa kuchukua takwimu.
“Hakuna mtu atakayekwenda kunyanyaswa katika kipindi hiki,sisi tunakwenda kuhuisha taarifa zetu, tuanze sasa..kwamba ndugu yangu ulikuwa una duka na mtu aliyekupa leseni alikupa leseni feki sasa tunakupa wiki mbili nenda kajiandae ukate leseni halali na sasa tumeanzisha kanda kurahisisha huduma, hivyo nenda kanda iliyokaribu yako kakate leseni yako uweke dukani kwako,”amesema Mpogolo.
AidhaMpogolo amesema kuwa, zoezi la ukusanywaji na uhuishaji wa taarifa za wafanyabiashara katika Halmashauri ya Jiji hilo umeanza Septemba Mosi unatarajiwa kukamilika Septemba 14, mwaka huu zitasaidia kujua idadi ya wafanyabiashara waliopo ikiwa pamoja na kujua wenye leseni feki.
“Tunaomba wafanyabiashara wote na wananchi tuungane na tusaidiane, tunakwenda kukusanya hizo taarifa na katika hicho kipindi cha kukusanya data, tunategemea kuanza tarehe 1 Septemba mpaka tarehe 14 mwaka huu,”amesema Mpogolo.
Ameongeza kuwa, katika kipindi hicho cha ukusanyaji wa taarifa halmashauri itatumia watumishi kutoka serikalini ikiwemo walimu ambao watakuwa kwenye kipindi cha mapumziko, ili kuhakikisha wanapata data zote za wafanyabiashara kwa kila mtaa katika mitaa yote 159.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua