Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
SERIKALI imesema hadi sasa jumla ya Halmashauri Ishirini na 24 nchini tayari zimefikiwa na huduma ya Anuani za Makazi huku kazi ya kufikisha na kuunganisha nchi nzima na mfumo huo ikiendelea.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo na Naibu Katibu Mkuu wa Habari, Mawasiliano na TEHAMA Dkt. Jim Yonazi wakati akifungua Warsha ya Watoa Huduma za Posta iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Ameeleza lengo la serikali ni kuhakikisha kila mtaa,nyumba,njia na barabara zinatambulishwa kwa anuani maalum chini ya utaratibu wa postikodi ili kurahisisha utambuzi na utoaji huduma za posta nchini.
Amesema serikali imejielekeza katika kuhakikisha kwamba kunakuwepo na miundombinu rafiki katika usafirishaji na ugavi kama ambavyo serikali imewekeza fedha nyingi katika kuunda mfumo wa postikodi na anuani za makazi.
“Na napenda kuwashirikisha kwamba nchi nzima sasa ina postikodi zake”amesema
“Na kwasasa mfumo wa Misimbo ya Posta ya Tanzania (postikodi Tanzania) utakuwa katika ukamilifu na kuwezesha utoaji huduma sita za posta na ufikishaji wa vifurushi na vipeto katika maeneo ya makazi, ofisi na sehemu za biashara bali pia utoaji wa huduma nyingine za jamii zikiwemo huduma za kutoa taarifa kwa zima moto, polisi nakadhalika,”amesema
Pia amesema Mfumo huo wa msimbo wa posta Tanzania yaani postikodi ulianzishwa mwaka 2012 ambapo Msimbo wa posta ni namba iliyochaguliwa kwa kila kata nchini.
“Kila kata ina msimbo wa tarakimu tano lengo ni kuhakikisha kila barua au kipeto inayotumwa nchini Tanzania ionyeshe namba hiyo juu ya bahasha au kifurushi kwa ajili ya urahisi wa kufikisha mzigo au barua husika panapostahili,”amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Kuwe Bakari awali akitoa maelezo ya utangulizi kabla ya warsha hiyo kuanza ameeleza kuwa TCRA imejidhatiti kuhakikisha huduma za posta nchini Tanzania zinakuwa zenye ushindani kwa shabaha ya kuongeza ufanisi wa utoaji huduma badala ya kuachia huduma hizo kwa watumiaji wachache.
Amesema kuwa Mamlaka hiyo tayari imetoa Leseni za huduma za posta kwa watoa huduma 119 kote nchini ambao wanatoa huduma ya kusafirisha vipeto na mizigo isiyokuwa barua ndani ya mkoa, mkoa hadi mkoa, Afrika Mashariki na Kimataifa.
“Miongoni mwa watoa huduma wa kufikisha na kukamilisha huduma hizo ni Pamoja na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ambao hutoa huduma ya kufikisha vifurushi ndani ya nchi na TCRA inaamini ushindani utaiwezesha sekta ya posta kufanya vizuri ,”amesema Jabiri.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Posta katika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Haruni Lemanya akiwasilisha mada kwenye warsha hiyo amesisitiza umuhimu wa watoa huduma za posta hasa wanaosafirisha vifurushi na vipeto kuhakikisha wanatumia mbinu za kisasa na zenye weledi wakati wote wanapotoa huduma za posta.
“Ni muhimu mkazingatia matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma zenu; pia ni muhimu kuzingatia ubora wa huduma kwa wateja wenu, kwa mfano ni muhimu kuweka namba ‘tracking number’ inayomwezesha mteja wako kufuatilia mwenendo wa mzigo wake alioutuma kupitia kampuni yako”amebainisha Lemanya.
Hata hivyo Lemanya amewaasa watoa huduma za posta kuhakikisha wanakatia bima mizigo ya wateja wao ili kuzuia hasara kwa kila upande unaohusika katika mabadilishano ya biashara ya usafirishaji,huku akibainisha umuhimu wa watoa huduma kukagua mizigo inayosafirishwa ili kujiridhisha na usalama wa mizigo hiyo.
“Kuna baadhi ya bidhaa haziruhusiwi kusafirishwa kwa mfano vitu vya milipuko; na kuna vitu vingine vinaweza kudhuru mwili kwa mfano visu ambavyo havijapangwa vizuri; kwa hiyo mnapaswa kuzingatia ni vitu gani vinapaswa kutumwa na vitu gani havitakiwi kutumwa” ameelimisha.
Warsha hiyo iliyotanguliwa na ufunguzi wa duka la Posta-mtandao inafanyika katika Wiki ya Posta duniani ambayo kitaifa inaadhimishwa jijini Dodoma, kilele chake ni Oktoba 9 mwaka huu. Wiki ya Posta inaongozwa na kauli mbiu isemayo Ubunifu kwa Posta Endelevu.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato