Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Misungwi
WAJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) wamesema chama hicho kimefanya mengi ya maendeleo ya kujivunia katika kipindi cha miaka 47 pamoja na kuaminika kwa wananchi hivyo hakuna namna yoyote ya kukiondoa madarakani.
Pia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewafanyia wananchi mambo mengi mazuri ya maendeleo, hivyo hawana cha kumlipa zaidi ya kuchagua viongozi wazuri kutoka ndani ya CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu.
Hayo yameelezwa Februari 4,2024 na wajumbe wa NEC,Habiba Ali Mohamed (WAZAZI-Zanzibar) na Jamal Abdul ‘Babu’ mjumbe wa NEC Mkoa wa Mwanza, walipozungumza na wananchi wakiwemo wana CCM wa Wilaya ya Misungwi,katika maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa kwa chama hicho.
“Niaombe wananchi wa Misungwi,uongozi wa chama na serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,ametekeleza ilani ipasavyo,ametufanyia mengi mazuri na sote tunajionea miaka 47 sekta za afya,elimu,kilimo,maji na miundombinu ya barabara amefanya kwa asilimia 100, tumuunge mkono,”amesema Habiba.
Amesema Samia amefanya mambo mengi ambayo hawana cha kumlipa, hivyo utakapofika uchaguzi wa serikali za mitaa katika vijiji na vitongoji wasifanye makosa kura zote ziende kwa CCM.
“Tumfurahishe mama kwani ametufurahisha sana na katika uchaguzi wa 2025 tumpe mitano tena kazi iendelee,”.
Kwa upande wa Jamal amesema kazi nzuri iliyofanywa na CCM kwa miaka 47 inakifanya kiendelee kuaminika kwa wananchi na kushika dola,hakuna namna ya kukishinda katika uchaguzi mbalimbali.
“Miaka 47 kazi nzuri zimefanyika, wakati kinaanzishwa kilikuwa na vipaumbe vitatu vya kupigana na maradhi, ujinga na umasikini,kimeyafanya hayo na kusimamia demokrasia,hivyo tujipongeze kwa kushiriki kukikifikisha kilipofika bila kuwasahau Hayati Nyerere, Mwinyi,Ben Mkapa (Hayati),Jakaya Kikwete, Hayati Dkt. Magufuli na sasa Dk.Samia,”amesema.
Mjumbe huyo wa NEC amesema leo chini ya mwanamke shupavu Dkt.Samia CCM imeendelea kuimarika katika chaguzi kikitoka kuongoza wananchi milioni 17 na wanachama 500,000 mwaka 1977 , kimeendelea kuongoza Watanzania zaidi ya milioni 61.
Pia amefanya mabadiliko makubwa ya kadi za kielektroniki na kuwezesha wana CCM kutambuliwa na mfumo na hivyo sifa ya chama haiwezi kutenganishwa na serikali ambapo ilianzisha shule kupambana na ujinga, zahanati na hospitali (maradhi) na shughuli nyingine za uzalishaji kiuchumi kukabiliana na umasikini.
“Asiye shukuru watu hata Mungu hawezi kumsukuru, nawashukuru kwa kuja kuhudhuria miaka 47 ya kuzaliwa CCM,Misungwi kilio kikubwa kilikuwa maji ili hali Ziwa Victoria liko karibu, Mbunge wa zamani wa hapa (Kitwanga au Mawe Matatu) alifikia uamuzi wa kusema ‘tutalala barabarani na wananchi wangu tukanyagwe na magari serikali isipoleta maji,”amesema Jamal.
Ameleza kuwa Rais Samia ameleta fedha kiasi cha billion 38 za maji na anajenga mtandao wa matenki ya kuhifadhi lita milioni 3.5 yatakayohudumia kata tano ikiwemo Usagara,ameleta zaidi ya bilioni 77 za mradi wa maji Mbarika na Misasi na anajenga km 139 za barabara ya lami.
Amewataka madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa waliopo madarakani,waachwe wachape kazi na kuonya watu wenye chokochoko wanaotengeneza majungu dhidi ya wenzao na kuwapa matope.
“Wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu kunakuwa na maneno maneno ya kuwatengenezea wenzenu ajali na majungu.Utasimama vipi kumnadi wakati ulimchafua? Hatutaki mpasuko, nafsi ya mwenyekiti wa CCM Wilaya Misungwi tutampata,”amesema Jamal.
Ameonya wanaochafua wana CCM wenzao na wenye makundi wakubali kuyavunja pindi wagombea wao wakishindwa katika sanduku la kura lakini kabla wagombea wote watatendewa haki na kusisitiza kuwa kasi iongezwe ya kuyasema yaliyofanywa na serikali huku akiwataka madiwani kutoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ili penye kasoro parekebishwe.ssss
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua