November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Hakuna mtumishi wa afya aliyepata COVID-19

Na Penina Malundo

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu, amesema hakuna mtumishi wa afya aliyepata maambukizi kwa kuwa wanazingatia miongozo ya Serikali wakati wa kutoa matibabu kwa wagonjwa wa Corona na pamoja na miongozo ya magonjwa ya kuambukiza.

Haya yalisemwa na Waziri Ummy jijini Dar es Salaam jana wakati akipokea msaada wa sh. bilioni 14.9 kutoka Global Fund, Airtel Tanzania, Rotary Club Tanzania ambazo sehemu kubwa zitatumika kununua vifaa kinga kwa watumishi wa afya na vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wenye maambukizi ya COVID-19.

Alisema kipaumbele cha Serikali ni kuwalinda watumishi wa afya kwa kununua vifaa kinga. “Kwa hiyo fedha tulizozipata hapa tutazielekeza kwenye ununuzi wa vifaa kinga. Niendelee kuwaisistiza Watumishi wa Afya wazingatie miongozo ya magonjwa ya kuambukiza,”alisema na kuongeza;

“Watumishi wa afya ambao wamepatiwa mafunzo katika vituo vya kutoa huduma kwa wenye maambukizi ya ugonjwa huo, hakuna aliyepata maambukizi kwa kuwa wanazingatia miongozo ya Serikali ya kutoa matibabu kwa wagonjwa wa Covid-19 pamoja na miongozo ya magonjwa ya kuambukiza,” alisisitiza

Waziri Ummy alifafanua kwamba Global Fund imetoa sh. bilioni 14, Airtel Tanzania sh. milioni 700 na Rotary Club Tanzania sh. milioni 250.

“Tumepokea sh. bilioni 14 kutoka Global Fund, sh. bilioni 9.6 tumezitoa kwa ajili ya kununua vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa Afya, lakini pia fedha zilizotolewa na Airtel na Rotary Club Tanzania tutazielekeza huko.

Kipaumbele chetu ni kuwalinda watumishi wa afya,” alisema na kuongeza;

“Natumia fursa hii kuwashukuru watumishi wa afya ambao wamekuwa wakijitoa usiku na mchana katika kutoa huduma kwa watu waliopata maambukizi ya virusi vya Corona (Covid-19) pamoja na wale wahisiwa,”alisema

Waziri alisema ushiriki wa kila mdau katika mapambano dhidi ya maambikizi ya virusi vya Corona ni muhimu na kwamba msaada uliotolewa na kampuni hizo ni mkubwa katika mapambano ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

“Napenda kurudia tena kwa niaba Rais Dkt. John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, nawashukuru Airtel Tanzania, Serengenti Breweries na Rotary Club kwa hiki mlichotupatia. Asanteni sana,” alisema Waziri Ummy.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Airtel Tanzania,Gabriel Malata alisema Airtel Tanzania imetoa shilingi milioni 700 ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na janga la Corona.

“Sisi bodi ya wakurugenzi wa Airtel na kwa niaba ya Airtel Tanzania, tunatambua juhudi za Serikali katika kupambana na ugonjwa wa Corona, lakini pia tumejitathimini na kutambua kuwa sisi kama Airtel hatuwezi kuendelea bila kuwepo watu wanaotumia huduma zetu. Watu hawa ndio mtaji wa Kampuni,” amesema Bw. Gabriel.

Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni ya Bia ya Serengenti, John Wanyancha alisema kuwa kampuni hiyo imetoa lita 1,250 ya vitakasa mikono nyenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na maambukiza ya virusi.

Mwenyekiti wa Rotary Club, Agnes Batenga alisema Rotary imetoa sh. milioni 250 kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID-19).

“Sh. milioni 183 zitatumika kutoa msaada wa vifaa vya kujikinga (PPE) vifaa vya maji safi ambavyo vitasambazwa katika vituo maalumu vya kuhudumia wagonjwa wa Corona jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Amana, Zanzibar, Hospitali ya Mawenzi na Hospitali ya Mount Meru,” alisema Agnes.

Alisema sh. milioni 67 zitatumika katika kutekeleza miradi ya kudhibiti ugonjwa wa Corona nchini kupitia Club za Rotary.