November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hagila aitabiria makubwa timunya Pamba Jiji

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

MJUMBE wa Bodi ya timu ya Pamba Jiji FC,Evarist Hagila amesema Tamasha la Pamba Day ni chachu ya kuwafanya mashabiki kutambua timu yao imerejea Ligi Kuu.


Pia wamesajili wachezaji wa viwango,usajili uliosimamiwa kwa weledi na wataalamu wa soka chini ya Kocha Mkuu wa timu hiyo Goran Kopunovic,raia wa Serbia.

Hagila ametoa kauli hiyo Julai 22,2024 baada ya uzinduzi wa uuzwaji wa tiketi za kuingilia katika tamasha la Pamba Day, litakalotumika kuwatambulisha wachezaji wa kikosi hicho.

Hagila amesema baada ya Pamba Jiji Fc kufuzu kucheza Ligi Kuu anaamini kwa usajili walioufanya itaonesha maajabu kutokana na aina na viwango vya wachezaji mseto wa damu changa na wakongwe wachache.

“Tumefanya usajili mzuri uliosimamiwa na kocha na wataalamu wenye weledi,hatuwezi kuwa wachawi wala waganga wapiga lamli,tutaonesha tulichofaya katika usajili naamini tuna timu nzuri,”.

“Pia mpira ni hamasa,hicho ndicho anachokitafuta Mkuu wa Mkoa Said Mtanda,siku ya Pamba Day hapo Agosti 10,mwaka huu, tutakwenda kuujaza Uwanja wa CCM Kirumba,” amesema Hagila.

Mjumbe huyo wa Bodi ya Pamba Jiji amesema uzoefu walionao wa kucheza ligi ya Championship kwa miaka mitatu ni somo tosha kwao na hivyo ligi kuu lazima mpira uchezwe kwa vitendo si maneno.

Aidha amenunua tiketi za wadau na mashabiki walioambatana na kuiunga mkono Pamba Jiji katika vita ya kupanda daraja zilizomgharimu kiasi cha milioni Moja ziwawezeshe.

“Tiketi hizo nimenunua za wapambanaji wa Pamba Jiji waliojitoa kuipambania timu katika michezo mbalimbali tukiwa bega kwa bega hatimaye kupanda ligi kuu,”amesema.

Naye mchezaji wa zamani wa Pamba almaarufu Tour Poissant Lindanda (TP Lindanda),Abuu Seif Mazige amewaushauri viongozi wa timu hiyo kuwakumbuka kwa kuwafanyia dua wachezaji takribani 40 waliotumikia timu hiyo ambao wametangulia mbele ya haki ili ifanye vizuri.