Na Mwajabu Kigaza , Kigoma
Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma imeandikisha wanafunzi wa elimu ya awali kwa asilimia 95.3 huku darasa la kwanza ikifikia asilimia 97.9 na hivyo kufikia lengo la uandikishaji huku miundombinu ya madarasa, madawati na idadi ya walimu ikionekana kuwa ni changamoto katika suala la ufundishaji na ujifunzaji kwa madarasa hayo.
Kwa mujibu wa sera ya elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inajumiisha elimu ya awali kuwa lazima na hivyo wazazi na walezi kutakiwa kuwaandikisha watoto wao wenye umri chini ya miaka mitano ili kuweza kufikia lengo la ujifunzaji kwa watoto hao kulingana na mtaala wa elimu ya awali.
Akizungumzia zoezi la uandikishaji wa elimu ya awali na darasa la kwanza kwa Manispaa ya Kigoma Ujiji kaimu Afisa elimu Manispaa ambaye pia afisa elimu taaluma msingi Kolineli Kisinga amesema kwa mwaka 2021/2022 uandikishaji wa watoto umeongezeka kwa kasi ukilinganisha na miaka ya nyuma uandikishaji ulikuwa chini na hivyo kushindwa kufikia lengo kwa muda uliokusudiwa.
Amesema awali wazazi na walezi walikuwa hawaoni umuhimu wa kuandikisha watoto wao waliochini ya umri wa miaka mitano wakihofia kuwa bado ni wadogo na uelewa wao ni mgumu kutokana na hali hiyo ililazimika kuwapatia elimu ili waweze kuona umuhimu wa watoto wao wenye umri huo kuanza shule mapema.
” Wakianza shule mapema inasaidia kumjengea mtoto msingi mzuri wa kutambua mambo mengi kwa vitendo kupitia kuona na kusikia pamoja na kutambua kusoma kwa kutumia vifaa vilivyo tengenezwa ama kuchora kupitia darasa linalozungumza , na pia inasaidia mtoto kutambua mazingira ya shule na kumfanya aipende shule akiwa na umri mdogo” amesemaÂ
Baadhi ya wazazi na walezi akiwemo Jackson Kisimbi na Edward Rusaka wamesema zoezi la uandikishaji kwa watoto wa elimu ya awali na msingi lilikuwa na changamoto kadhaa ambapo baadhi ya wazazi hawakuwa na nyaraka zozote ikiwemo cheti cha kuzaliwa mtoto wala risiti hivyo kuwa vigumu kuandikisha watoto kwa haraka , sambamba na hilo foleni ya wazazi ambao wameleta watoto imekuwa kubwa mno jambo lililosababisha zoezi la uandikishaji kuchukua muda mrefu.
Vivian Msindai ni mwalimu mkuu shule ya msingi Burega pamoja na Lau Phillimon mwalimu mkuu shule ya msingi wanaeleza kuwa ongezeko hilo la uandikishaji wa wanafunzi limekuwa na changamoto mbalimbali hususani kutokuwepo kwa uwiano unaolingana na ikama ya walimu, miundombinu ya vyumba vya madarasana madawati.
Wamesema hali hiyo inasababisha mwalimu mmoja kufundisha zaidi ya watoto 100 kwenye chumba kimoja cha darasa wengine wakiwa wanakaa chini na hilo linachangia hata uelewa wa watoto kuwa mgumu kutokana na kushindwa kumfikia kila mtoto.
Pepetua Mathias ambaye ni afisa taaluma wilaya ya Kigoma amesema serikali inaendeleq kupambana na changamoto zilizopo katika shule za msingi kwa kushirikiana na wadau wakiwemo EQUIP na P4R katika uboreshaji wa mindombinu ya vyumba vya madarasa, lakini pia serikali imeweza kujenga shule shikizi na lengo ni kuhakikisha changamoto ya vyumba vya madarasa inatatuliwa kama ilivyo kwa shule za sekondari
More Stories
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25